UCSAF yatekeleza maagizo ya Samia

  • Shs. milioni 174 zatumika kufunga intaneti maeneo 6 ya wazi
  • Minara mipya 758 katika mikoa 26 kuifanya Tanzania ya Kidijiti
  • Asilimia 96 ya Watanzania watumiaji wa mitandao ya simu

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetekeleza kwa vitendo agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha maeneo ya wazi yanafungwa mtandao wa intaneti ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo bure.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justine Mashiba, amewaeleza wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Novemba 21, 2023 kwamba, mpaka sasa tayari maeneo sita ya wazi yamekwishanufaika na mradi huo uliogharimu Shs. milioni 174.

Aliyataja maeneo hayo ambayo mradi huo umekamilika kuwa ni Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Lungemba (Mafinga mkoani Iringa), Nyerere Square (Dodoma), Ndaki ya Habari na Elimu Angavu (CIVE) ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Soko la Tabora (Tabora), Kiembe Samaki (Unguja) na Soko la Buhongwa (Mwanza).

Mei 18, 2023, wakati alipozindua Mradi wa Minara ya Kurusha Matangazo ya Televisheni Ardhini (DTT) ya Kampuni ya Azam Media Limited uliogharimu Shs. bilioni 50, Rais Samia aliagiza kufungwa kwa intaneti katika maeneo ya wazi ili kuwapa fursa wananchi kutumia bure huduma hizo za mtandao.

Akabainisha kwamba, Serikali imejipanga kuja na Satellite ambayo itaweza kusaidia wananchi kupata mawasiliano na habari kwa haraka ikiwemo kutambua utekelezaji unaofanywa na Serikali na mengine yanayoendelea nchini na ulimwenguni kote.

“Wote tunakumbuka kuwa nchi yetu iliachana na mfumo wa analojia katika matangazo ya Televisheni na kutumia teknolojia ya dijitali tangu Juni 17, 2015, hatua hii ilikuwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa kutokana na faida nyingi kama vile ubora wa picha na sauti, matumizi bora ya masafa ya utangazaji, na nishati ya umeme, uwezekano wa kutoa huduma za ziada kama internet na matumizi ya runinga za mkononi na kwenye magari, Tanzania ilifanikisha mpango huu ndani ya muda uliopangwa,” alisema Rais Samia wakati huo.

Watumiaji wa mtandao

Mtendaji Mkuu wa UCSAF anasema kwamba, hali ya mawasiliano nchini imeimarika huku akipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia, kwamba zimewezesha kuwafikia Watanzania wengi.

Bi. Justina anasema, hadi kufikia mwaka 2009 wakati UCSAF inaanza rasmi, mtandao wa mawasiliano kwa idadi ya watu (population coverage) ambao walikuwa wakitumia huduma ya simu walikuwa ni asilimia 45 tu ya Watanzania wote.

“Kwa sasa watu wanaotumia huduma za simu ni asilimia 96,” anasema.

Akaongeza: “Wanaotumia teknolojia ya 2G ni asilimia 96, wanaotumia teknolojia ya 3G ni asilimia 77, na wanaotumia teknolojia ya 4G ni asilimia 65.”

Anasema, kwa upande wa maeneo ya kijiografia (geographical coverage), teknolojia ya 2G ni 69%, teknolojia ya 3G ni 62% na teknolojia ya ni 50%.

Mradi wa Tanzania ya Kidijitali

Tanzania haiko tayari kubaki nyuma katika mabadiliko ya ulimwengu hasa katika sayansi na teknolojia, ambapo inaendelea kutekeleza kwa kasi miradi mbalimbali kuhakikisha inakuwa ya kidijitali (Digital Tanzania).

Ndiyo maana hatika katika mwaka wa fedha 2022/23, serikali iliainisha vipaumbele takriban 13 katika utekelezaji wa mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali ambavyo ni pamoja na kujenga vituo vya kukuza taaluma bunifu katka Tehama; Kuwezesha ununuzi, ugavi na ufugngaji wa vifaa; Kuwezesha ununuzi wa ‘bandwidth’ kwa ajili ya matumizi ya intaneti ya Serikali; Kusimika mitambo kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Taifa cha Kanzidata (NIDC); Kukarabati vituo 10 vya Huduma Pamoja.

Vipaumbele vingine ni Kujenga mfumo wa kitaifa utakaorahisisha ukusanyaji wa takwimu za masuala ya Tehama; Kujenga, kupanua na kuboresha miundombinu iliyopo ya intaneti yenye kasi (broadband) inayomilikiwa na Serikali (GovNET) na kuunganisha taasisi 100 kwenye Miundombinu hiyo na kufikisha taasisi 390 zilizounganishwa; Kutekeleza programu ya uelimishaji umma kuhusu mradi; Kujenga maabara tatu (3) kwa ajili ya kufufua (refurbishment) vifaa vya Tehama katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza; Kujenga minara ya mawasiliano 150 kwenye Kata 150 ili kuwezesha huduma za mawasiliano nchini; Kufanya mapitio na kuhuisha Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali za Tehama; Kuwajengea uwezo wataalam wa Tehama nchini kwa kuwapatia watalaam 200 mafunzo ya muda mfupi na wataalam 10 mafunzo ya muda mrefu; na Kufanya tathmini ya kuainisha mahitaji na usanifu wa kujenga mfumo wa kuwezesha biashara mtandao.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, hadi kufikia Desemba 31, 2022 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilipokea jumla ya kiasi cha Shs. 10,261,846,606.50 sawa na asilimia 26.11% ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya Mradi tajwa ya Shs. 39,300,000,000 fedha za nje ziliombwa.

Shughuli mbalimbali zilitekelezwa kwa kipindi husika ambazo zinachangia kuleta manufaa na kuyafikia malengo ya Serikali hasa katika uchumi wa kidijitali.

Tafiti zinaonyesha kuwa uchumi wa kidijitali utachangia asilimia 30 ya pato la dunia huku ukiongeza ajira milioni 30 zaidi.

Uchumi wa kidijitali barani Afrika unatarajiwa kufikia thamani ya dola bilioni 712 ifikapo mwaka 2050 na wataalamu wanasema, upo uwezekano mkubwa kwa Bara la Afrika kuwa kitovu cha uchumi wa kidijitali katika miaka ijayo. Kwa sasa Pato la Afrika ni dola 3.1 trilioni na dijitali inachangia bilioni 200.

Sekta zinazoonyesha kukuza ukuaji huo ni kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa (AgriTech), viwanda, teknolojia ya huduma za fedha, usafirishaji, masoko mitandao na kutumia suluhu za kidijitali katika nyanja zote za kiuchumi ikiwemo akili mnemba.

Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazotajwa kuwa katika nafasi kubwa ya kunufaika na uchumi wa kidijitali kuliko nyingine kwa kuwa ina idadi kubwa ya vijana.

Tanzania ipo katika utekelezaji mfumo wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali unaolenga kuhakikisha sekta zote za uchumi zinatumia Tehama huku ikiwezesha mabadiliko ya kidijitali yanayojenga jamii jumuishi ya kidijitali kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Katika hotuba yake ya kwanza bungeni Rais Samia Suluhu Hassan alieleza nia ya Serikali yake katika miundombinu ya Teknolojia ya mawasiliano (Tehama) na kuongeza kasi ya kufikisha miundombinu ya mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi ya nchi ili kuwa na ujumuishi wa kidijitali.

“Kama inavyofahamika, dunia ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, ambayo yanaongozwa na sekta ya Tehama na kwa maana hiyo, Uchumi wa dunia pamoja na shughuli nyingi duniani, kwa sasa, zinafanyika kwa kutumia Tehama,” alisema Rais Samia Aprili 22, 2021.

Rais Samia alisema mbali na kuongeza upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini pia anakusudia kuongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.

“Tutaongeza watumiaji wa internet kutoka asilimia 43 ya sasa hadi asimilia 80 mwaka 2025 na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima,” alisema Rais Samia.

Tayari Serikali imeandaa mpango wa miaka 10 wa Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Kidijitali (National Digital Economy Framework 2023-2033) utakaosaidia kuongeza matumizi ya kidijitali kwa huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na Sekta binafsi.

Katika kuyafikia malengo hayo, ndiyo maana Mfuko wa Mawasiliano kwa wote inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kuwezesha wananchi kutumia mitandao hiyo kwa kujenga miundombinu bora na imara.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba, anasema kwamba jumla ya minara 758 itajenga katika Kata 713 kwenye Wilaya 127 za Mikoa 26 ambayo itawanufaisha wananchi milioni 8.5.

Anasema, kampuni ya simu za mkononi ya Airtel itajenga minara 169, TTCL minara 104, Honora (tiGO) itajenga minara 261, Halotel minara 34 na Vodacom minara 190.

Bi. Justina anasema, jumla ya Shs. bilioni 32.9 zimekwisha lipwa kwa watoa huduma na UCSAF kama Malipo ya Awali (Advance Payment) kwa watoa huduma wote.

“Kupitia ruzuku ya DTP, kiasi cha Shs. bilioni 12.96 zimelipwa kwa Vodacom na Airtel, vibali vya mazingira (Provisional Environmental Certificate) vimetolewa kwa minara yote 758, watoa huduma wanaendelea kufanya tathmini ya maeneo ya kujenga minara, na mpaka sasa Halotel ameanza ujenzi ambapo amesimamisha minara 5 tayari,” anasema.

Ujenzi wa Minara Vijijini

Anabainisha pia kwamba, USAF imeingia mikataba na Watoa Huduma ya Mawasiliano (kampuni za simu) kufikisha Huduma ya Mawasiliano katika Kata 1,974 zenye vijiji 5,111 kwa kujenga jumla ya minara 2,149, ambapo minara yote hiyo ikikamilika wananchi takriban 23,798,848 watapata Huduma hiyo ya Mawasiliano ya simu kwa uhakika.

“Mpaka sasa, jumla ya Kata 1,197 zenye vijiji 3,613 na wakazi takriban 14,572,644 wameshafikishiwa na Huduma ya Mawasiliano kwa jumla ya minara 1,321 iliyojengwa tayari katika Kata hizo.

“Utekelezaji unaendelea katika minara 828, vijiji 1,498 na wakazi 9,226,204, ambapo gharama (ruzuku) za utekelezaji wa mradi huu ni takriban Shs. bilioni 326,” anasema.

Tehama shuleni

Katika kukuza teknolojia ya mawasiliano kuanzia ngazi ya chini, UCSAF imekuwa ikipeleka vitendanishi katika shule na taasisi mbalimbali.

Mpaka sasa jumla ya shule 1,120 zimefikishiwa vifaa vya Tehama, ambapokwa wastani shule hupewa Kompyuta 5, Printa 1 na Projekta 1.

Katika mwaka wa fedha 2022/23, Shule 150 zilifikishiwa vifaa vya Tehamaambapo bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni Shs. 1,876,900,000.

UCSAF inatekeleza Mradi wa kupeleka vifaa maalum vya kujifunzia kwa shule zenye watoto wenye mahitaji maalum ambapo jumla ya shule 8 zilifikishiwa vifaa hivyo vya Tehama ambavyo ni pamoja na TV, Braille Machine (Nukta Nundu), Orbit Reader (Machine za Kisasa), Laptops, na Embosser (Printa ya Nukta Nundu).

Shule zitakazonufaika ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Mpwapwa (Mpwapwa-Dodoma), Sekondari ya Mkolani (Mwanza), Sekondari ya Kashaulili (Mpanda-Katavi), Sekondari ya Morogoro (Morogoro), Sekondari ya Shinyanga (Kishapu-Shinyanga), Sekondari ya Wavulana Songea (Songea), Sekondari ya Kazima (Tabora) na Sekondari ya Haile Selassie (Mjini Magharibi, Zanzibar).

Gharama za vifaa hivyo ni Shs. 575,000,000.

Mfuko huo pia mwaka huu umefanikiwa kufikisha mtandao wa intaneti katika Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa – Saba Saba jijini Dar es Salaam, ambako iliweka vituo 17 kwa gharama ya Shs. 200,000,000.

Mpango wa sasa wa UCSAF pia ni kufikisha mtandao wa intaneti katika vituo vya mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam (DART Awamu ya 1 & 2) ambao utekelezaji wa mradi huo uko hatua za awali za manunuzi.

Ujenzi wa vituo vya Tehama Zanzibar

Bi. Justina anasema, katika mradi huo juml ya vituo 11 vimejengwa Zanzibar, Pemba 4 na Unguja viko 7, ambavyo vinasaidia kutoa mafunzo ya Tehama.

“Kituo cha mwisho ni kilichojengwa Bwefumu Zanzibar na kuzinduliwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi Oktoba 26, 2022. Kituo hiki kiligharimu Shs. 147,000,000,” anasema.

Vituo vingine ni pamoja na Tunguu, Mwera, Kitogani, Mkokotoni, Kiembe Samaki, Mahonda, Wete, Machomanne, Micheweni, Jonza na Bwefumu.

Lakini pia UCSAF inafanya mradi wa kujenga vituo vya Tehama kwa Kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania ambapo jumla ya vituo 11 vimeanzishwa, huku UCSAF ikitoa kompyuta pamoja na Printa.

Uboreshaji huduma za utangazaji

Mfuko huo pia unafanya Mradi wa kuboresha Huduma za Utangazaji katika mikoa saba ya Tanzania Bara.

Inaelezwa kwamba, baada ya upembuzi wa kitaalamu, maeneo sita (6) yalibainika kuwa na uhitaji wa kujengewa vituo vya kurushia matangazo ya redio ambayo ni Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu, Same, Kilindi, Mbulu, Kondoa na Rufiji.

Katika mradi huo, UCSAF inatarajia kujenga mnara mmoja kwa kila Halmashauri kwa ajili ya Radio za Kijamii (Community Radio) na kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, mkataba kwa maeneo hao sita tayari umesainiwa.

“Ujenzi unaendelea katika maeneo matano (Same, Kilindi, Kasulu, Kondoa DC na Mbulu). Ujenzi katika halmashauri ya Wilaya ya Rufiji unasubiri kukamilika kwa barabara ya kupelekea vifaa eneo la mradi,” anasema Justina.

Uboreshaji usikivu wa TBC

Mfuko huo unatekeleza Mradi wa Kuboresha Usikivu wa Redio ya Taifa nchini ikiwa inashirikiana na Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC).

Katika mradi huo, jumla ya vituo 16 vimejengwa na utekelezaji wa miradi katika maeneo 16 umekamilika.

Maeneo hayo ni Kisaki mkoani Morogoro, Mlimba mkoani Morogoro, Ludewa mkoani Njombe, Makete mkoani Njombe, Ruangwa mkoani Lindi, Ngara mkoani Kagera, Mlele mkoani Katavi, Kyela mkoani Mbeya, Uvinza mkoani Kigoma, Ngorongoro mkoani Arusha na Mbinga mkoani Ruvuma.

Aidha, utekelezaji wa miradi unaendelea katika maeneo matano ya Lushoto-Mkinga mkoani Tanga, Kyerwa mkoani Kagera, Chemba mkoani Dodoma, Kiteto mkoani Manyara na Chunya mkoani Mbeya.

Kuongeza uwezo wa minara

Kwa upande mwingine, UCSAF imeingia makubaliano na Watoa Huduma kuongeza nguvu minara 127, mradi ambao tayari umekamilika.

Kupitia mradi wa DTP, Mei 13, 2023 watoa huduma (kampuni za simu) waliingia makubaliano na Serikali ambapo jumla ya minara 304 itaongezewa nguvu.

Mpaka kufikia Novemba 20, 2023, jumla ya minara 111 tayari imeshaongezewa nguvu kutoka kwa watoa huduma ambao ni Vodacom minara 30, Airtel minara 25 na Honora minara 56.

Katika miradi hiyo, gharama zilizotumika ni Shs. 5,149,164,696.

Utekelezaji wa maeneo yaliyobaki unatarajiwa kumalizika ifikapo Desemba 2023.

Mafunzo kwa walimu

Ili kuhakikisha vifaa vya Tehama vinavyogawiwa shuleni vinatumiwa kwa ufanisi, UCSAF inaendesha programu ya mafunzo kwa walimu, kwani imeonekana kwamba, vifaa vinapogawiwa, kwa kuwa walimu wanakuwa hawana uelewa wa matumizi, huvifungia na mwishowe vifaa hivyo huharibika.

Mafunzo yalianza 2016 ambapo mpaka sasa jumla ya walimu waliopatiwa mafunzo ni 3,465, kati yao 3,139 ni kutoka Tanzania Bara na 326 kutoka Tanzania Visiwani.

Mfuko huo haukuwa na bajeti ya mafunzo kwa walimu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, lakini UNICEF wamefadhili 42 kutoka mikoa ya Songwe na Tabora, ambayo yatagharimu Shs. milioni 50.

Mradi wa Tiba Mtandao

Kwa kuwa ulimwengu umekuwa wa kidijitali, UCSAF imekwenda hatua kadhaa mbele ambapo sasa inatekeleza mradi wa Tiba Mtandao (Telemedicine) kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia (DIT), Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa ya MOI na Hospitali nyingine kadhaa.

Hospitali zilizounganishwa katika mfumo huo ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, na zinazokamilishwa ni pamoja na Ruvuma, Tanga, Katavi, Nzega na Chato.

“Kwa upande wa Zanzibar tunaunganisha Hospitali ya Abdala Mzee iliyoko Pemba na Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja iliyopo Unguja ambapo utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho,” anafafanua Justina.

Kuboresha huduma za Posta

Katika kuboresha huduma za Posta, UCSAF imepanga kutoa vifaa 250 vya Tehama ambapo mradi huo UCSAF inashirikiana Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Inaelezwa kwamba, hatua za manunuzi zimekamilika na mkataba umeshasainiwa na mzabuni kwa ajili ya kuleta vifaa hivyo.

Mafunzo kwa wasichana

Katika kuendana na maadhimisho ya Siku ya Wasichana na Tehama, UCSAF kwa kushirikiana na wadau wamewapatia mafunzo ya Tehama jumla ya wasichana 954 tangu kuanzishwa kwa siku hiyo mwaka 2016.

Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, wasichana 110 watafanyiwa mafunzo katika mikoa ya Songwe (30), Tabora (40) na Kigoma (40) kwa kushirikiana na UNICEF.

Katika mradi huu UNICEF wametoa bajeti ya Shs. 90,000,000.

Kwa ujumla, haya ni mafanikio makubwa na yanaonyesha dhahiri namna Serikali ilivyodhamiria kuifanya Tanzania ya Kidijitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *