Na Daniel Mbega, Lindi
SERIKALI inakusudia kujenga vituo nane (one-stop centres) nchini vya ubunifu wa teknolojia vitakayowezesha vijana na wananchi kwa ujumla kuvitumia kuboresha kazi zao za kibunifu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, ameyasema hayo Novemba 14, 2023 mjini Lindi wakati wa Mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri nchini.
Amesema vituo hivyo vinatarajiwa kujengwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Tanga, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.
“Huu ni mpango wa awali, lakini mkakati uliopo ni kujenga vituo katika mikoa yote na wilaya zote, ili wananchi waweze kuvitumia na kujifunza suala zima la teknolojia,” alisema.
Aidha, alisema, vituo hivyo vitajengwa katika maeneo ya shule ambavyo vitasaidia vijana nchini kuendelea kuibua vitu mbalimbali vinavyuohusiana na teknolojia pamoja na kuendeleza, ambapo vitakuwa na uwezo wa kuingiza watu 200 kwa wakati mmoja.
Amewaomba wadau mbalimbali kushirikiana katika kuanzisha vituo hivyo, lengo likiwa ni kukuza vipaji tofauti.
Dkt. Mwasaga alisema, watu wengi wamekuwa na hofu na akili bandia au akili mnemba (Artificial Intelligence – AI) kwamba inaweza kuwakosesha kazi, jambo ambalo alisema siyo kweli, kwani AI inaleta tija na kwamba watu wakipewa ujuzi mpya kuhusu teknolojia hiyo itasaidia.
Alisema watajenga kituo cha Artificial Intelligence kwa ajili ya kuendeleza wataalam wa Tehama pamoja na kuwezesha mafunzo maalum ya wataalam wa Tehama 500 ili kukuza na kuendeleza ujuzi wa Tehama nchini.
Inaelezwa kwamba, ujenzi wa vituo hivyo ni sehemu ya vipaumbele 13 vya ICTC ambavyo vina lengo la kuleta mapinduzi ya teknolojia na ubunifu nchini.
“Tunatarajia kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya Tehama (ICT Refurbishment and Assembly Centre) na vituo vya majaribio vya ubunifu Tehama (District ICT Startups Innovation Hubs) katika wilaya 10,” alisema Dkt. Mwasaga.
Aidha, alisema watafanya tafiti za maendeleo ya Tehama nchini na kufanya tathmini ya kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Tehama.
Aliongeza kwamba, wataratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za Tehama ndani na nje ya nchi.
“Tutashirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za Tehama ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za Tehama hapa nchini,” alisema
Alisema, majukumu mengine watakayoyafanya ni pamoja na kukuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogo ndogo “startup” kwa kushiriki maonesho na makongamano yanayohusu fursa za startups duniani.
ICTC pia inakusudia kuratibu na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa utekelezaji wa Sera ya Tehama na kufanya tafiti za kuweza kufanya maboresho ya sera kulingana na mabadiliko ya teknolojia.
Mikakati mingine ni pamoja na kujenga Metaverse Studio kwa ajili ya kutengeneza maudhui ya metaverse na pia kuboresha maudhui ya mitandao ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti za maendeleo ya Tehama kwa kila wilaya na kuanzisha Kituo cha Resilience Academy hapa nchini.