Yanga SC hakuna kulala kimataifa

Na Badrudin Yahaya

Licha ya timu zingine kuwapa mapumziko wachezaji wao, Klabu ya Yanga, imeonekana haipumziki baada ya kuendelea na mazoezi ya gmy.

Ligi ya Tanzania Bara kwa sasa imesimama kupisha mechi za kufuzu Kombe la Dunia ambapo timu yao ya Taifa ‘Taifa Stars’, imeingia kambini kujiandaa na mechi dhidi ya Niger na Morocco.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika mtandao wa klabu hiyo kwa njia ya video, imewaonesha wachezaji wao wakiendelea na mazoezi ya gmy.

Yanga imeendelea na maandalizi hayo ikiwa inajiandaa kwa mechi yao ijayo ambayo itakuwa ni dhidi ya CR Beluizdad ya Algeria.

Mchezo huo wa kwanza hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika utafanyika Novemba 25 nchini Algeria.

Mbali na Beluizdad, Yanga imepangwa na Al Ahly ya Misri pamoja na FC Medeama ya Ghana katika Kundi moja la D.

Kikosi cha timu hiyo chini ya Kocha, Miguel Gamondi, kinawakosa baadhi ya nyota wao Bakari Mwamnyeto, Abdallah Abdullah, Aboutwalib Mshery, Dickson Kibabage, Clement Mzize na Dickson kutokana na majukumu yao ndani ya Taifa Stars.

Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na alama 24 ikifuatiwa na Azam FC na Simba SC zenye alama 19 kila moja ila zinatofautiana kwa mabao.

Mara ya mwisho kushuka uwanjani ilikuwa ugenini dhidi ya Coastal Union na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *