Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
JUMUIYA ya Wafanyabishara Tanzania (JWT), imesema fursa aliyoitoa Rais Samia Suluhu Hassan ya kustawisha wafanyabishara kwa kusikiliza kero zao, hawataipoteza.
Mwenyekiti wa JWT, Hamis Livembe aliyaeleza hayo jana Novemba 8, 2023 mjini Bagamoyo mkoani Pwani, wakati akizungumza na wafanyabishara katika ziara ya kusikiliza kero, kusajili wananchama na kuimarisha umoja wa jumuiya hiyo.
Alisema kila serikali inayoingia madarakani inakuja na sera zake na kwasababu serikali inayoongozwa na Rais Samia iliona vyema kukaa meza moja na kundi hilo muhimu kusikiliza wana nini na wanataka nini kwa maslahi mapana ya Taifa letu, hawana budi kufanya hivyo.
Alieleza zaidi kuwa, kupitia mgomo wa wafanyabishara wa soko la Kariakoo, Rais Samia aliona inafaa viongozi wa jumuiya kuzunguka nchi nzima kuwasikiliza changamoto zao kama zipo mpya na zile zilizopokelewa na kamati iliyondwa awali ya kuzunguka nchi nzima kwa muda mfupi.
Alisema baada ya kamati ile kuna kero ambazo zilitafutiwa ufumbuzi na kuna ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi hivyo ni wakati wafanyabishara kutumia vyema fursa ya kuwasilisha zile ambazo hazikukusanywa.
“Hatupo tayari kupoteza fursa hii muhimu adhimu, kila sekta ina majukumu yake na wajibu wake kwa Taifa nasi tuna wajibu wetu na Rais Samia ametusikiliza ni muhimu kuwa wawazi kueleza kero zetu ili tusipoteze fursa hii,” alisema Livembe.
Naye Katibu Mkuu wa JWT, Abdallah Salim Mohamed, alisema Pwani ni mkoa wa 14 kutembelea tangu wameanza ziara nchini na bado wana kazi kubwa kukamilisha ziara hiyo kwenye mikoa mingine iliyosalia.
Aliwataka wafanyabishara kutumia fursa hiyo adhimu aliyoitoa Rais Samia ya kusikiliza kero zao kwa kuwa amewaonyesha thamani kubwa.
“Huko nyuma tumeitwa majina mabaya, wakwepa kodi, wezi na mengine mabaya, lakini Mama (Rais Samia) akasema hapana hawa mbona wanachangia kwenye pato la Taifa, akasema akae na sisi atusikilize hivyo hivi sasa tunatembea nchi nzima kusikiliza kero zote ili tukae pamoja kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Salim.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Uongozi ya JWT na Katibu wa JWT mkoa wa Tanga, Ismail Masoud, alisema wafanyabishara walipitia kipindi kigumu cha kuonekana wezi na watu wasiyo na thamani kwa Taifa lao lakini Rais Samia ameona wana umuhimu ndio sababu amewakaribisha kuka meza moj ya mazungumzo.
“Mama ametuthamani sana wafanyabishara, leo hii ameruhusu tufike maeneo yote nchini tukusanye kero zote ili zifanyiwe kazi. Sisi tunasema anayekuwekea mchuzi kwenye wali ndio mwenzako, hatuna sababu ya kupoteza fursa hii muhimu lazima tusimame naye hatua kwa hatua,” alisema Ismail.
Naye Mjumbe wa Bodi wa JWT na Makamu Mwenyekiti Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Hemed, aliwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kujenga jumuiya hiyo ili kuwa kitu kimoja na kusimama kama ambavyo taasisi nyingine zimesimama na kuwa imara zaidi.