NEEC yawatonya wajasiriamali wanawake mikopo ‘kausha damu’

Na Mwandishi Wetu, Dar es Saslaam

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’I Issa amewataka wanawake na vijana hapa nchini kuachana na mikopo umiza maarufu kama kausha damu kwani haileti afya kwaukuaji wa uchumi binafsi badala yake wajielekeze   kwenye mifuko wezeshi kupata mitaji.

Akizungumza kwenye Mkutano mkuu wa nne wa taasisi ya Open Mind and Thoughts Organization (OMTO) Jijini Dar es Salaam, Bi. Issa alisema serikali imendelea kuweka mazingira wezeshi na himilivu kwa wanawake na vijana kupata mitaji na kuwataka wajitokeze kwa wingi kutumia fursa hiyo,

“Mikopo ya kausha damu imekuwa nitatizo kubwa kwa watanzania hususani wanawake ambao wanataka kupata mikopo ya urahisi bila kujua ukikopa unaweza kujikuta unarudisha mara tano ya kiwango ulichochukua, mikopo hiyo ni hatari kwani haileti afya kwaukuaji wa uchumi binafsi,” alisema Bi. Issa.

Alisisitiza kuwa kabla ya kusaini mkataba hakikisha unausoma na kuuelewa kwani watu wengi wamekuwa wakipewa mikataba nakusaini pasipo kusoma na hivyo kupelekea kuingia hasara kubwa hivyo kurudi kwenye dimbwi la umasikini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa OMTO, Bi. Anna Haule, alisema taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2019 ikiwa na kikundi kimoja chenye watu 20 ambapo hadi mwaka 2023, kikundi kimefikisha vikundi  89 nakufisha wanachama 2,330 katika mikoa mitatu na wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam.

Bi. Haule mbali ya kuishukuru taasisi ya CRDB Bank Foundation, kupitia programu yao ya imbeju alisema mkutano huo wa nne wa mwaka umejipambanua katika kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo kuhusu namna bora ya kuweka akiba.

“Kiukweli watanzania wamekuwa na mwaamko wa kujiunga kwenye vikundi kwani wamefahamu ndiyo sehemu sahihi ya kutimiza malengo yao,” alisema Bi Haule akipongeza juhudi na kazi zinazofanywa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Uendeshaji wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, Bi. Joycelean Makule, amesema kupitia mtaji wezeshi, taasisi yake imetoa kiasi cha shilingi milioni 35 pamoja na bajaji moja yenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa wanachama wa OMTO ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

“Mtaji huu wezeshi chini ya mwavuli wa programu ya imbeju uliotolewa kwa wanachama mkautumie vyema kwenye malengo yaliyokusudiwa ili mrejeshe kwa wakati na fedha hizo ziwasaidie wengine,” alisema Bi. Makule na kuongeza kuwa mtaji huo wezeshi sio mkopo kwani una gharama ndogo za uwendeshaji na unatolewa chini ya taasisi kuanzia shilingi 200,000 hadi milioni 30.

Bi Makule alisema, Imbeju ni programu iliyojipambanua kuwawezesha wanawake na vijana katika kukuza biashara zao ili waweze kujikwamua kiuchumi wao na familia zao huku wakitoa mchango stahiki katika kukuza Pato la Taifa.

NEEC imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maona na matarajio ya serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifuko wezeshi inatoa mchango stahiki ikiwemo utoaji wa mitaji wezeshi kwa makundi hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *