- Uzalishaji wa gesi asilia wafikia futi za ujazo bilioni 53.19
- Wazawa waongezeka kwenye ajira utafutaji mafuta, gesi
Na DanielMbega, Dar es Salaam
UONGOZI mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) kuokoa kiasi cha Shs. bilioni 189 zilizorejeshwa kwenye Mfuko wa Ugawanaji Mapato kati ya Serikali na waendeshaji wa vitalu vya uzalishaji gesi asilia nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Eng. Charles Sangweni, aliwaeleza wahariri wa vyombo vya habari nchini Novemba 6, 2023 kwamba, fedha hizo zimerejeshwa kutokana na kuimarika kwa shughuli za Kaguzi za Gharama katika Mikataba ya Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA Audit).
Mbali ya kurejeshwa kwa fedha hizo, pia limekuwepo ongezeko kwa wastani wa uzalishaji wa gesi asilia kufikia futi za ujazo bilioni 53.19 kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Februari 2023 ukilinganisha na futi za ujazo bilioni 46.96 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 14.
“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan, Pura katika kutekeleza majukumu yake imewezesha kupatikana kwa mafanikio mengi,” alisema Eng. Sangweni.
Alisema, mbali ya kurejesha fedha hizo, pia mafanikio mengine ni kuimarika na kuongezeka kwa ushiriki wa wazawa katika miradi ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini ambapo wastani wa ushiriki wa wazawa katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli kupitia ajira ni asilimia 85.
Eng. Sangweni alitaja mfanikio mengine kwamba ni kushauri Serikali na kufanikisha kuongezwa kwa muda wa leseni ya utafutaji katika Vitalu vya Tanga, Ruvu, Mtwara na vitalu Namba 1, 2 na 4 vilivyopo baharini.
“Tumefanikiwa kushauri Serikali na kufanikisha utiaji saini kwa mkataba wa nyongeza wa uzalishaji na ugawanaji mapato ya gesi iliyogundulika Ntorya katika Kitalu cha Ruvuma. Mkataba huo ambao utekelezaji wake utawezesha kuendeleza gesi asilia ya Kitalu hicho ya takriban futi za ujazo trilioni 1.6 ulisainiwa baina ya Wizara ya Nishati, TPDC na Kampuni ya ARA ya Oman,” alisema.
Akaongeza: “Tumefanikisha durusu ya Mkataba Kifani wa Uzalishaji na Ugawanaji wa Mapato (MPSA) kwa lengo la kuhuisha ili kuendana na mazingira ya uwekezaji wa sasa katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia. Kukamilika kwa mapitio ya MPSA ni hatua muhimu kuelekea zoezi la kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
“Kukamilika kwa maandalizi ya rasimu ya Ramani ya Kidijitali (Interactive Digital Petroleum Reference Map) kwenye Mfumo wa Taarifa wa Kijiografia (Geographical Information System – GIS) inayotoa taarifa za Vitalu vya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini,” alisema.
Akielezea historia ya utafutaji wa gesi asilia nchini, Eng. Sangweni alisema, shughuli hizo zilianza mwanzoni mwa miaka ya 1950 na hadi sasa mafanikio makubwa yameyopatikana.
Alisema mpaka sasa jumla ya visima vya utafutaji wa mafuta vilivyochimbwa nchini ni 96 ambapo kati ya visima hivyo, visima 59 vipo maeneo ya nchi kavu na visima 37 vipo maeneo ya baharini.
Akaongeza kuwa, gesi asilia imegunduliwa katika visima 44 kati ya visima 96 vilivyochimbwa, ambapo kati ya visima hivyo 44 vilivyogundulika gesi, visima 16 vilichimbwa nchi kavu na 28 vilichimbwa baharini.
“Gesi asilia imegunduliwa katika maeneo ya Songo Songo (mwaka 1974); Mnazi Bay (1982), Mkuranga (2007), Kiliwani Kaskazini (2008), Ntorya (2012), Ruvu (2016) na Kina Kirefu cha Bahari (kuanzia miaka ya 2010),” alisema.
Aliongeza kwamba, gesi asilia iliyogunduliwa nchi kavu na kina kirefu cha bahari ni futi za ujazo trilioni 57.54 (nchi kavu trilioni 10.41 na baharini trilioni 47.13).
Eng. Sangweni alibainisha pia kwamba, uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2004 kwa upande wa Songo Songo na mwaka 2006 kwa upande wa Mnazi Bay.
Aidha, alisema, ugunduzi na uzalishaji wa gesi asilia iliyogunduliwa umewezesha itumike maeneo mbalimbali, hususan kwa kuzalisha umeme, kutumika viwandani, majumbani na kwenye magari.
“Hadi sasa kiasi cha gesi kinachozalishwa kinachangia karibu asilimia 70 ya umeme unaozalishwa hapa nchini,” alisema.
Aliongeza kwamba, hadi sasa kwa kupitia usimamizi wa Pura maeneo ambayo yamefanyiwa tafiti ni kiasi cha kilomita za mraba 534,000 ambapo kati ya hizo kilomita za mraba 394,000 ni nchi kavu na km 140,000 baharini.
Hata hivyo, alisema, maeneo mengi yameshafanyiwa tafiti za awali ambapo data, taarifa na takwimu (Gravity/Magnetic and 2D seismic) zake zipo.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, mafanikio mengine ni kuimarika kwa mifumo ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi nchini, ambapo kumekuwa na Sheria ya Petroli ya mwaka 1980, Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, na Sheria ya Udhibiti wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015, mifumo ambayo imewezesha kuanzishwa kwa Pura na Ewura.
Alisema, licha ya harakati za utafutaji na uchimbaji wa gesi kukumbwa na changamoto nyingi, lakini changamoto hizo zilipatiwa ufumbuzi na hatimaye kufikia hatua iliyopo ambapo kumefanyika ugunduzi wa gesi asilia nyingi ambayo matumizi yake yana manufaa makubwa kwa Taifa na hasa kwenye kuinua uchumi.
“Kipekee kabisa nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa usindikaji wa gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (yaani LNG project), mradi ambao utaliletea Taifa manufaa makubwa kwa kuanzia fedha, ajira, uanzishwaji wa viwanda vinavyotumia gesi kama malighafi pamoja na uuzaji wa bidhaa mbalimbali,” alisema.
Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa miongozo na maelekezo ambayo yamewezesha ustawi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini.