Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Tanzania inayo haki ya kujivunia kwa kuwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni kiongozi makini, mweledi na muadilifu.
Profesa Kitila aliyasema hayo Bungeni jijini Dodoma jana, Novemba 6, 2023 wakati akiwasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2024/2025.
“Sisi kama nchi tunaye kiongozi mkuu wa nchi makini aliyeonesha weledi na kuthibitisha uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake. Zaidi ya yote amethibitisha kuwa kiongozi muungwana na mpenda haki,” alisema.
Alisema, kupitia falsafa yake ya 4R, amejenga maridhiano mapana ya kijamii na kisiasa na kuweka mazingira sawia ya kufanya siasa kwa vyama vyote nchini (R1 =Reconciliation).
“Ametoa uhuru wa kutosha wa kutoa maoni bila woga wala vitisho huku akionesha ustahimilivu wa hali ya juu (R2=Resilience).
“Kiongozi wetu ameleta mageuzi makubwa katika kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji (R3 = Reform).
“Amefufua sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na madini na kuwapa matumaini mapya mamilioni ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini. Hakika anaijenga upya nchi yetu (R4 =Rebuilding) na kupitia uongozi wake, Serikali na nchi yetu ipo salama,” alifafanua.
Akaongeza: “Ni wazi kuwa sisi kama nchi tuna mahitaji mengi lakini raslimali tulizo nazo zina kikomo. Kwa sababu hii tunawajibika kuchagua tufanye lipi leo na lipi tulifanye baadaye. Hii ndiyo maana ya kupanga. Kupanga ni kuchagua. Katika kupanga tutazingatia vipaumbele vya kimkakati kwa kuzingatia dunia inataka nini na sisi tunaweza kutoa nini.”