Na Zahoro Mlanzi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Klabu ya Yanga kwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya watani zao wa jadi, Simba katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo ambao uliochezwa jana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, umeifanya Yanga kulipa kisasi cha mwaka 2013 ambapo walifungwa 5-0.
Ushindi huo, umeifanya Yanga ambao wameshatwaa ubingwa wa ligi hiyo mara mbili mfululizo, kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 21 ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 19 na Simba alama 18.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X, Rais Dkt. Samia aliandika: “Hongereni Yanga kwa ushindi dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Amesema upinzani wenu wa jadi wa zaidi ya miaka 85 sasa ni sehemu muhimu ya burudani ya Watanzania.
“Mnawaleta pamoja na kwa namna kipekee, mamilioni ya Watanzania ndani na nje ya nchi yetu,” ameandika Dkt. Samia.
Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yalifungwa na Max Nzengeli mawili, Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI na Pacome Zoazoua.
Bao pekee la Simba lilifungwa na Kibu Denis ambaye hakumaliza mechi kutokana na kutumia kifundo cha mguu.