Na Badrudin Yahaya
Kocha wa Klabu ya soka ya Yanga, Miguel Gamondi, amesema hana presha kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Simba.
Gamond amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuelekea mchezo huo ambao utapigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha huyo raia wa Argentina, amesema maandalizi waliyofanya ni ya kawaida kama ambavyo huwa wanafanya kwenye mechi nyingine na kwamba kikubwa anachoamini mechi itakuwa nzuri kwa pande zote mbili.
Gamondi amesema muhimu katika mchezo wa kesho ni kuepuka kufanya makosa kwani kosa dogo linaweza kuamua mechi.
“Sina presha yoyote tumejiandaa kama tunavyofanya kwenye mechi nyingine, kikubwa kesho ni kujiepusha na makosa kwani makosa madogo yanaweza kuamua mechi,” amesema.
Aidha Gamondi alipoulizwa kuhusu rekodi ya Yanga kushindwa kupata ushindi dhidi ya kocha wa Simba, Robertinho kwa mechi kadhaa, amesema yeye hajawahi kufungwa na Simba kwani katika mechi ya Tanga walitoka sare hivyo amesema hana rekodi yoyote anayotakiwa kuivunja.
Mchezo wa kesho utachezeshwa na Mwamuzi Ahmed Arajiga kutoka Manyara kama ilivyotangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).