Samia: Utalii ni utajiri wa Afrika

*Hotuba yake WTTC yatoa mwelekeo

*Asisitiza ushirikishwaji sekta binafsi

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, jana alishiriki na kutoa hotuba ya dakika 10 katika Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC) mwaka 2023 uliofanyika Kigali, nchini Rwanda.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia alisema ni muhimu nchi za Afrika kuweka mkakati wa pamoja ili kutangaza utalii wa Afrika, kufanya tafiti, uchambuzi wa takwimu za kiuchumi, kutunza, kuhifadhi utajiri wa sekta hiyo.

Alisema Afrika ina utajiri wa mkubwa wa vivutio vya utalii akitolea mfano Tanzania ina Hifadhi 11 za Taifa, kisiwa cha Zanzibar chenye vivutio mbalimbali.

“Sekta ya utalii imechangia asilimia 17.2 ya Pato la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya fedha za kigeni,” alieleza.

Akizungumzia mkakati wa kujitangaza, Rais Dkt. Samia alishairi sekta binafsi ipewe kipaumbele cha kushiriki katika uwekezaji ukiwemo wa filamu kwa kushirikisha watu maarufu duniani.

Pia kutumia simulizi za uzuri wa Afrika, kupiga vita maudhui yanayochafua Bara la Afrika ili kudhoofisha mchango wa sektta hiyo katika nchi husika.

Zaidi ya miaka 30 imepita tangu Baraza hilo lianze shughuli za tafiti juu ya athari za kiuchumi za usafiri na utalii katika nchi 185.

Lengo ni kutazama msongamano wa watu, kodi, utungaji wa sera ili kukuza mchango wa sekta hiyo kiuchumi.

Kwa upande wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, alishauri viongozi wa Afrika kushirikiana pamoja kukuza utalii wa Afrika,

Alisema kwa miongo ijayo, anaamini Afrika itakuwa kitovu cha utalii wa dunia hivyo ili kufikia mafanikio ya kuwa kituo kikubwa, wafanye kazi pamoja, hakuna sababu ya kupoteza fursa hiyo.

“Uhifadhi na utunzaji wa sekta ya utalii ni moja ya mikakati ya Rwanda kwa ajili ya kizazi kijacho baada ya kuimarika miundombinu, kuipenyeza katika sekta ya michezo mikubwa duniani,” alieleza Kagame.

Rais wa WTTC, Julia Simpson, aliwashauri viongozi wa Afrika kufanya mapitio ya sera ambazo zitawasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi katika shughuli za utalii duniani.

Alishauri matumizi ya magari ya umeme katika shughuli zote za huduma za utalii, nishati safi ya umeme, kupikia.

Alisema ripoti zinaonyesha mwaka 2019 sekta ya usafirishaji ilichangia asilimia 40 ya uzalishaji wa kaboni kwa uchomaji wa mafuta.

Kati ya kiwango hicho, asilimia 16 ilitokana na huduma za anga, asilimia 24 uasfiri wa ardhini.

Aliwataka Mawaziri wa sekta hiyo walioshiriki mkutano huo, kuitazama changamoto hiyo na kusisitiza, unahitajika uwekezaji katika magari ya nishati ya umeme kwenye usafiri wa ndani kutokana na hali mbaya iliyopo.

“Pia tutazame umuhimu wa matumizi ya nishati jadidifu…ni muhimu kulinda mifumo ya ikolojia katika sekta hii ili kulinda rasirimali, viumbe hai ambavyo vinahusika katika kukuza utalii,” alisema.

Aliongeza kuwa, takwimu zinaonyesha mwaka 2019 watu milioni 84 kutoka maeneo mbalimbali duniani walitembelea Afrika na kuchangia mapato ya dola za Marekani bilioni 186.

“Pamoja na uchangiaji huo, sekta hii ilichangia uzalishaji wa asilimia 8.1 ya kaboni duniani, ifikapo mwaka 2033, sekta hii inatarajia kuchangia dola milioni 50 na ajira milioni sita Afrika,” alieleza.

Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Mazingira la Conservation International linalohusika na huduma za mfumo wa ikolojia, asilimia 70 ya usalama wa duniana viumbe hai hutegemea bayonwai.

MWISHO

CAPTION

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutumia Mkutano wa Kimataifa wa 23 wa Baraza la Utalii Duniani (WTTC) uliofanyika Kigali, nchini Rwanda, jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *