Na Mwandishi Wetu, katavi
WAZIRI Mkuu mstaafu na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri kwa Rais katika masuala ya Kilimo na Chakula, Mizengo Pinda amewaonya viongozi, nakampuni zilizopewa dhamana ya kusimamia, kusambaza mbolea za rukuzu kwa wakulima akiwataka waache matumizi mabaya ya madaraka wanaposimamia zoezi hilo.
Pinda aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wadau wa kilimo katika ‘Wiki ya Mwanakatavi’ inayoendelea mkoani Katavi.
Alisema ili kufikia asilimia 10 ya sekta ya kilimo kuchangia pato la taifa ifikapo mwaka 2030, matumizi ya mbolea, mbegu bora, uhifadhi bora wa mazao lazima uzingatiwe.
Alieleza kuwa, hivi sasa kwenye sekta ya kilimo matumizi ya mbolea yako chini kutokana na baadhi ya wasimamizi waliopewa dhamana na serikali kusimamia utoaji mbolea kwa wakulima kutumia madaraka yao vibaya, kuhujumu usambazaji mbolea kwa wakulima.
“Yapo matumizi mabaya ya madaraka katika usambazaji mbolea kwa wakulima, waliopewa dhamana na serikali wanawadanganya wakulima kuwa mbolea hazipo kwa lengo la kuzipeleka mahali pengine kwa watu fulani.
“Hali hiyo kusababisha kero kwa wakulima kushinda asubuhi hadi jioni wakitafuta mbolea bila mafanikio yoyote,” alifafanua Pinda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Mwanamvua Mrindoko akitoa hali ya maandalizi ya kilimo kwa msimu ujao wa kilimo 2023/2024, alisema umefika wakati kwa taasisi zinazosimamia matumizi bora ya mbegu kuongeza usimamizi ili kudhibiti, kutokomeza tabia hiyo ambayo ni chanzo cha uzalishaji mbaya wa mazao.
“Kuna baadhi ya watu wanatabia ya kuchukua mbegu za kawaida na kuzipaka rangi kisha kuzifunga kwenye mifuko vizuri, kuwauzia wakulima kumbe ni mbegu feki,” alisema.
Raymond Kamtoni ambaye ni miongoni mwa wadua wa kilimo walioshiriki, alisema ili kufikia asilimia 10 ya sekta ya kilimo kuchangia pato la Taifa ifikapo 2030 serikali inapaswa kudhibiti mbolea zisizo na ubora pamoja na viuatilifu.