Mando Women: Wanawake waliogeukia useremala, ujenzi

Na Mwandishi Wetu, Geita

“NILIPOKUWA nafundisha sekondari nilikuwa nafanya biashara ndogondogo, nilinunua mashine nikawa nakwenda na fundi vijijini nauliza huu ni mti gani, nachana nauza napata fedha…hakuna mti ambao siujui na hakuna kitu ambacho fundi anaweza akafanya nisijue au akanidanganya,” anasema Nkwimba Hilu ambaye ni Mkurugenzi wa Kikundi cha Wanawake cha Mando.

Nkwimba anaongoza wanawake wengine wanne ambapo wameunda kikundi kijulikanacho kama Mando Women Group kilichopo mkoani Geita ambapo kimejikita kufanya shughuli za useremala na nyingine za ujenzi kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Ubunifu na uaminifu ndio unaowabeba wanawake hao kwenye soko hasa ikizingatiwa kuwa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya ujenzi.

Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Mando Women Group, Nkwimba anasema baada ya kufundisha kwa miaka mitano aliamua kuacha kazi hiyo na kuanza kufanya kazi ya useremala.

“Tulianza mwaka 2021, nilikuwa mwajiriwa wa Serikali lakini ilifika mahala nikaamua kuacha kazi, nika – organize hiki kitu tukaungana na kuanza kufanya shughuli mbalimbali. Tulifanya utafiti kwanza na tumejikita kufanya kazi nyingi ambazo zimezoeleka kufanywa na wanaume,” anasema Nkwimba.

Nkwimba anasema ujuzi wa useremala unatokana na kukaa karibu na watu wanaofanya shughuli hizo lakini pia wameajiri vijana waliopitia mafunzo ya useremala.

Anasema mtaji wao wa kuanzia hawakukopa bali walichangishana kutokana na kazi walizokuwa wakifanya awali kisha kuanza kutengeneza samani mbalimbali ambazo baada ya kuuza ziliwaongezea mtaji.

Kwa sasa anasema biashara imekua kwani wanapokea oda nyingi kutoka kwenye kampuni, taasisi na watu binafsi.

Kazi wanazofanya

Kikundi hicho kinamiliki kiwanda cha kutengeneza samani mbalimbali ambapo wanatumia miti migumu pia wana kiwanda cha matofali na duka la vifaa vya ujenzi ambapo wametoa ajira kwa vijana 30.

“Tunafanya kazi na Mgodi wa Geita (GGML), mara nyingi wanapokuwa wanatekeleza ile sera ya CSR (kurudisha sehemu ya faida kwenye jamii inayowazunguka) wamekuwa wakitupa kazi. Tunawatengenezea samani kama vile milango na kuwasambazia vitu mbalimbali,” anasema Nkwimba.

Anasema pia wamenufaika kupitia miradi mbalimbali ya Serikali kama ya ujenzi wa shule ambapo wamekuwa wakipata zabuni za kusambaza vifaa vya ujenzi.

“Mama (Rais Samia) anavyotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule tunapata tenda mbalimbali, wanatuambia tuletee mabati, saruji na vitu vingine.

“Tunazishukuru taasisi za Serikali, mgodi wa GGM wametufikisha mbali, tunaishukuru na jamii ya Geita kwa kutufikisha hapa tulipo.

“Tuna uwezo wa kufanya kazi kwahiyo tunaomba wadau mbalimbali, taasisi za serikali na binafsi watupe kazi zaidi. Hata wenye migodi watupe mikataba mikubwa sisi tuna uwezo wa kufanya,” anasema Nkwimba.

Changamoto

Nkwimba anasema kabla hawajaingia katika biashara hizo mwaka 2017 walijaribu kuchimba madini lakini kutokana na kutokuwa na vifaa walipata hasara ya Sh milioni 70 na kuamua kuacha.

Anasema kwa sasa changamoto kubwa inayowakabili ni mtaji kwani wanataka kufanya vitu vikubwa lakini mtaji wao bado ni midogo.

“Taasisi za kifedha ziweke mazingira rafiki kwa ajili ya kutuwezesha wanawake wajasiriamali kwa kutupatia mikopo mbalimbali ikiwezekana kupunguza masharti na riba,” anasema Nkwimba.

Anasema changamoto nyingine ni baadhi ya wateja kutowalipa kwa wakati na wakati mwingine kudhulumiwa.

“Tuliwahi kudhulumiwa tuliagiza mzigo Mwanza tukadhulumiwa shilingi milioni sita, tukaungana tena na mtu kwenye kazi akatudhulumu shilingi milioni 40 tukarudi nyuma.

“Kuna kipindi tulipata kazi ya madawati tukadhulumiwa kwahiyo tumekutana na changamoto nyingi,” anasema.

Kuhusu mfumo dume anasema; “Mara ya kwanza ulikuwa unatuathiri lakini kwa kuwa tumeonyesha juhudi na jamii ya Geita imeona wanabaki tu kusema kumbe wanawake wanaweza. Kwasasa wanatutazama kwa jicho lingine na tunaona mabadiliko makubwa.

Anasema licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali wameweza kupenya na hivi sasa kazi zao zinasikika kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Namshukuru Mungu kwa sababu licha ya changamoto mbalimbali lakini tumepokelewa vizuri, tumekuwa wabunifu kwa kubuni vitu vipya ambavyo vitaivutia jamii” anasema.

Malengo ya baadaye

Anasema matarajio yao ni kuendelea kuongeza vitega uchumi vingi zaidi kwa sababu wanataa kuendelea kukua na kuwa kampuni kubwa.

“Tuna mpango wa kusajili ukandarasi na kwa sasa tuko kwenye mchakato kwa ajili ya kufanya kazi za ujenzi kama za barabara.

“Tunataka kufika kwenye viwanda halisi, mfano tunafanya ‘hardware’ tunakwenda mara nyingi kutafuta lakini tunakutana na madalali, ingekuwa viwandani tungepata vitu kwa bei nafuu kufanya biashara kubwa zaidi,” anasema.

Kikundi hicho pia kina malengo ya kurudisha shukrani kwa wanawake wenzao ambapo wanatarajia kujenga kituo kuwasaidia wanawake na wasichana wanaoishi kwenye mazingira magumu ili waweze kunyanyuka kiuchumi.

“Lengo letu kwa siku za baadaye ni kuwasaidia wanawake na wasichana wanaoishi kwenye mazingira magumu, kuwatia moyo na kuwafundisha vitu mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi,” anasema Nkwimba.

Mkurugenzi huyo anasema wamekuwa wakirudisha sehemu ya faida wanayopata kwenye jamii inayowazunguka ambapo wametoa msaada wa kuwalipia ada wanafunzi watano.

Ushauri kwa wanawake

Nkwimba anasema hajawahi kujuta tangu alipoanza kufanya shughuli hizo na moja ya mafanikio makubwa anayojivunia ni kupokelewa vyema kwenye jamii huku akiamini katika kujishughulisha zaidi.

“Mwaka 2021 nilipata tuzo ya uongozi katika biashara na ujasiriamali, pia mwaka huu Benki ya NMB Geita imenipa cheti katika Wiki ya Huduma kwa Wateja nikajikuta ni mwanamke pekee niliyepata,” anasema Nkwimba.

Anawashauri wanawake kuthubutu kufanya shughuli mbalimbali kwa sababu hata wao wakati wanaanza walivunjwa moyo lakini hawakurudi nyuma.

Mkurugenzi huyo wa Mando Women Group anawahamasisha Watanzania kujumuika pamoja nao ili wafurahie kazi zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *