YST yakuza maendeleo ya sayansi, teknolojia nchini

Na Janeth Jovin, Dar es Salaam

DESEMBA 05, 2023, Jiji la Dar es Salaam linategemewa kuwa mwenyeji wa maonesho ya bunifu za kisayansi za wanafunzi wa sekondari kutoka shule mbalimbali nchini ambazo zina lengo la kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.

Kazi hizi za sayansi zitaoneshwa kupitia mashindano yanayoandaliwa na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) iliyojikita katika kukuza uelewa wa maswala ya sayansi na ubunifu wenye kuleta tija katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye jamii.

Akizungumza kuhusu maonesho hayo Mwanzilishi wa YST, Joseph Clowry anasema kuwa mashindano hayo yatafungua fursa kwa wanafunzi wa sekondari kuweza kuonesha vipaji vyao vya kubuni tafiti mbalimbali za kisayansi zenye kuleta tija kwenye jamii.

Anaeleza kuwa mashindano hayo yatashirikisha wanafunzi wapatao 90 kutoka shule mbalimbali 45 za sekondari nchi nzima watakaojumuika kuonesha bunifu zao zitakazotumika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Anasema miradi ya kisayansi itakayooneshwa wakati wa maonesho hayo itakuwa imegusa sekta ya fizikia, hesabu, kemia, teknolojia na sayansi ya kompyuta, mabadiliko ya tabia ya nchi na sayansi ya mazingira, sayansi ya kilimo na sayansi ya jamii.

“Tangu mwaka 2011, YST imekuwa imefanya kazi kubwa ya kuwajengea wanafunzi uwezo na ujuzi katika nyanja ya sayansi na teknolojia pamoja na ujuzi wa kuwa wabunifu,” anasema

Anaongeza kuwa dira ya YST ya kukuza sayansi inaenda sambamba na malengo ya Serikali ya kukuza uelewa wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari.

Katika kufanikisha hili, YST imejikita katika kutoa mafunzo ya sayansi kwa waalimu wa sayansi ili kuwawezesha kutoa ujuzi sahihi wa sayansi ya vitendo kwa wanafunzi ipasavyo…

Kupitia programu ya kuwajengea uwezo, YST imekuwa ikitoa mafunzo ya ujuzi wa kisayansi na maarifa kwa waalimu na wanafunzi wa sekondari ili kuwaimarisha kuelekea kwenye mashindano ya mwaka.

Kupitia ushirikiano mkubwa kutoka kwa Taasisi ya Karimjee Foundation, YST imefanikiwa kuinua shauku ya wanafunzi kupenda masomo sayansi na kuwa wabunifu wa kufanya tafiti mbalimbali zenye kuleta tija kwa wananchi.

Clowry anasisitiza kuwa programu ya kuwajengea uwezo wanafunzi inatoa mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya elimu ya sayansi nchini ambayo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza sekta ya elimu hususani katika sayansi ya vitendo.

Kwa upande wake Dk. Gozibert Kamugisha Mwanzilishi Mwenza wa YST anasema kuwa jitihada hizi za YST zinaenda sambamba na Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo pamoja na Mkakati wa Elimu wa Bara la Umoja wa Afrika (2015 – 2025) unaolenga kuongeza wigo wa maendeleo ya sayansi kwa wanafunzi na walimu.

Dk. Kamugusha anasema kwa miaka 13 iliyopita, YST imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuwekeza kwenye maarifa ya sayansi na ujuzi wa teknolojia kwa wanafunzi na waalimu wa sekondari.

“Tumechagua kuwekeza elimu na maarifa kwa vijana wetu kwa sababu tunaamini wana uwezo na ubunifu wa kutumia teknolojia kubuni miradi ya kisayansi yenye kuleta tija na kuleta suluhu dhidi ya changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii,” anaeleza Dk. Kamugisha.

Meneja miradi wa YST, Nabil Karatela anasisitiza kuwa programu ya kuwajengea uwezo wanafunzi na waalimu imesaidia kuibua wimbi la vijana wabunifu na kuchochea upatikanaji wa tafiti zenye kuleta suluhisho dhidi ya changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.

Anasema Jitihada hizo za YST za kuwekeza katika sayansi sio tu zinalenga katika kunufaisha waalimu na wanafunzi bali zinalenga moja kwa moja katika kukuza maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji kutoka Taasisi ya Karimjee Foundation, Caren Rowland anaeleza kuwa nia ya Karimjee ni kuwekeza katika jitihada zinazolenga kuwaandaa vijana watakaokuwa wanasayansi mashuhuri na watakaochagiza maendeleo ya kiuchumi nchini.

Karimjee inaamini kuwa sayansi ni msingi mkubwa wa kukuza maendeleo ya kiuchumi kwenye jamii pamoja na kuwanoa wanafunzi kwenye ujuzi wa kisayansi.

“Ni furaha yetu kuwa sehemu ya jitihada hizi za YST za kuwekeza katika ubunifu wa kisayansi kwa vijana watakaotumika kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda kupitia teknolojia,” anasema.

“Kupitia programu hii, Karimjee imefanikiwa kuwezesha vijana 41 kwenye masomo ya sayansi kuanzia mwaka 2022 ambao wamekuwa wabunifu na kupatiwa zawadi za ufadhili wa masomo ya chuo ili waweze kuendeleza vipaji vyao vya kisayansi,” anasema Caren.

Anaongeza kuwa kwa mwaka huu, maonesho ya wanasayansi yatahusisha miradi mbalimbali ya kisayansi iliyochaguliwa mashuleni na zenye ushindani mkubwam kwa pande zote.

Hamasa na shauku kubwa inazidi kuongezeka kwa wanafunzi wakati siku zikikaribiana za mashindano makubwa ya mwaka ya Wanasayansi yanayotarajiwa kufanyika tarehe 03/12/2023.

Maonesho haya yatawakutanisha wanafunzi 90 wa sekondari kutoka kwenye shule zaidi ya 45 nchini nzima watakaojumuika kuonesha bunifu zao za kisayansi zinazolenga kuleta suluhisho dhidi ya changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii yao.

Watu 5000 wameshiriki na kati ya hao 3000 ni watanzania na 2000 waliobakia ndio waliotoka nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *