*Ujerumani yakoshwa na demokrasia
*Wafungua fursa ushirikiano kiuchumi
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS wa Ujerumani, Frank -Walter Steinmeier, amesema uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeendelea kujenga uchumi, kufuata utawala wa sheria hasa katika suala zima la demokrasia.
Alisema urafiki wa maraifa hayo umedumu muda mrefu, utaendelea kwa sababu ya uaminifu na upendo uliopo katika mataifa hayo.
Rais Steinmeier aliyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya kufanya mazungumzo na Rais Dkt. Samia.
Alisema Wajerumani wameona namna Rais Dkt. Samia anavyojenga uchumi wa Tanzania, kufuata utawala wa sheria hasa katika suala zima la demokrasia.
“Tunakuhakikishia sisi watu wa Ujerumani tunaendelea kuwa mshirika wa Tanzania kwa karibu,” alisema.
Aliongeza kuwa; “Hatupo hapa kwa ajili ya kujenga mahusiano lakini tupo hapa kuahidi tutaendelea kuwekeza katika ukanda huu, nimefurahishwa na moyo wako wa kuendelea kudumisha uhusiano huu na kuufanya uwe mzuri zaidi hata kwa ajili ya kesho yetu,” alieleza.
Alisema wamejadiliana na Rais Dkt. Samia namna ya kujenga mahusiano ya karibu zaidi katika maeneo mengine ya ushirikiano.
Pia wamejadiliana suala la uwekezaji, rasilimali , kilimo, afya na nishati mbadala ambayo ni sekta muhimu.
“Kule Ujerumani tupo katika nmchakato wa kubadili na kuangalia namna gani ya kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ili tufikie lengo la kupunguza matumizi makubwa ya kaboni katika masuala ya nishati,” alisema.
Alieleza kuwa, watashirikiana katika sekta ya nishati kwa kubadilishana uwezo, ziara hiyo italeta matunda katika masuala ya kiuchumi na sekta zingine mbalimbali.
“Nina uhakika tutaendelea kusimama na kutumia zaidi fursa zilizopo kutokana na mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili, katika safari mbili nilizokuja Tanzania nimejifunza mengi, natamani kukutana na wabunifu ambao ni vijana wa Kitanzania.
“Nimefurahishwa sana, tutaweza kusimama na wabunifu vijana katika hili, suala la ushirika wa kiuchumi na namna gani ya kutoa mitaji zaidi itakayowasaidia katika uzoefu ili kuwa na watu wenye maarifa katika masuala ya kidigitali,” alisema.
Pia wamekubaliana kufanya utafiti kwa mambo yaliyotokea ezi za ukoloni, kuanzisha ukurasa mpya na walioathiriwa na vita vya maji maji, kukutana na wahanga na kuzungumza nao kwa kuwa walipitia kipindi kigumu.
“Yote ambayo watanieleza nitakwenda kuyawasilisha Ujerumani, kuangalia namna gani ya kurudisha mabaki ya watu yaliyopo Ujerumani,” aliongeza.
Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia alisema licha ya Tanzania na Ujerumani kuwa na ushirikiano mzuri wa muda mrefu katika shughuli mbalimbali za maendeleo, bado kuna fursa kubwa ya kukuza ushirikiano wa kibiashara, uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Ujerumani na Tanzania zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya afya, elimu, usambazaji wa maji safi na salama, hifadhi ya mazingira, ulinzi na usalama, haki za binadamu na utawala bora na hifadhi ya maliasili.
“Katika mazungumzo yetu, tumeelekeza timu za pande zote mbili kukaa, kufanya majadiliano ya mara kwa mara ili kubaini maeneo mapya ya ushirikiano ambayo yatatusaidia kupiga hatua haraka zaidi katika kukuza biashara, wekezaji kwa manufaa ya watu wetu,” alisema.
Pia wamekubaliana kufungua majadiliano katika masuala kadhaa ya kihistoria ikiwemo suala la mabaki ya kale ya Tanzania yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani.
Alimuhakikishia Rais huyo kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo yajayo ya ushirikiano wa maendeleo yanayotarajia kufanyika 2024.
Akizungumzia biashara, mahusiano ya uwekezaji, Rais Dkt. Samia alisema waliweka msisitizo katika uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tuna miradi si chini ya 100 ya Ujerumani katika ngazi mbalimbali imewekezwa Tanzania, tumekuwa tukifanya baishara na Ujerumani ingawa kuna uwezekano mkubwa wa kukuza biashara na hilo tutalielekeza katika mazungumzo yajayo,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa ikipata watalii kutoka Ujerumani licha ya uwezekano wa kupata idadi kubwa ya watalii zaidi, kushirikiana katika uhifadhi wa mbuga hasa Selous na Serengeti.
Rais Dkt. Samia alisema Tanzania ilikuwa chini ya utawala wa Ujerumani, ipo tayari kufungua majadiliano ili kuona namna ya kukubaliana mambo mbalimbali.
Alisema Tanzania inaangalia usawa wa jinsia na uwezeshaji kwa wanawake kiuchumi kupitia mradi ambao nchi ingependa kushirikiana nao.
“Masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora , Rais ametupongeza kwamba Tanzania tumetulia kwenye utawala wa sheria na utawala bora ndiyo maana wamevutika kufanya biashara Tanzania, kuangalia fursa za uwekezaji,” alisema.
Rais Dkt. Samia alisema mazungumzo yajayo ni kujenga uwezo wa vijana kwenye uchumi wa kidigitali.
Ziar a hiyo inathibitisha dhamira ya serikali kuimarisha, kukuza ushirikiano na urafiki kwa lengo la kunufaisha watu wa nchi hizo mbili.
Aliongeza kuwa, ujio wa kiongozi huyo utachangia kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo kibiashara, kiuchumi kwa kuzingatia kuheshimiana, kuthaminiana.