Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
TANZANIA inaweza kunufaika zaidi na sekta ya mafuta na gesi asilia ikiwa wazawa ndio watakuwa na fursa ya kutosha ya ajira na kusimamia sekta hiyo.
Hali hiyo itategemea pia ufanisi katika programu mbalimbali za elimu ambazo serikali imezianzisha, ikiwa ni pamoja na kusisitiza kwa vitendo ufundishaji wa masomo ya sayansi ambayo yanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu pamoja na wanafunzi wengi kutoyapenda.
Tanzania imekuwa ikitafiti uwepo wa mafuta na gesi asilia kwa zaidi ya miaka 60 sasa na katika miaka yote hiyo, imefanikiwa kugundua uwepo wa gesi asilia kwa wingi na kuifanya kuwindwa na wawekezaji wa kimataifa.
Pamoja na ugunduzi wa rasilimali hiyo, bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalamu kwenye sekta hiyo, hali ambayo inaonyesha kwamba kuna mahitaji makubwa ya elimu ya ufundi ambayo inaweka msisitizo kwenye stadi maalumu na maarifa ambayo yanahitajika hasa kwenye shughuli mbalimbali za utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia nchini.
Kwa sasa Serikali inaendelea na mkakati kabambe kwa kuanzisha programu mbalimbali katika ngazi ya vyuo vikuu inayohusiana na sekta ya petroli ambayo inatolewa katika vyuo mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Mafunzo hayo yanapata msaada kama vile vifaa vya maabara, wahadhiri kutoka nje ya nchi, ufadhili wa mafunzo kwa wanafunzi na programu za mafunzo za ushirikiano.
Kwa sasa, shahada za kwanza nne (4), zikijumuisha shahada ya ufundi na shahada ya uzamili zinatolewa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Shahada ya Kwanza
Mnamo Oktoba 2013, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilianza kutoa shahada tatu za kwanza zinazohusiana na petroli.
Chuo kishiriki cha Sayansi Asilia (CONAS) kinatoa shahada ya kwanza katika Jiolojia ya Petroli (B.Sc. Petroleum Geology) na Chuo kishiriki cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) kinatoa shahada ya kwanza katika Uhandisi wa Petroli (B.Sc. Petroleum Engeneering) ambayo mtaala wake umeandaliwa kwa ushirikiano na Chuo cha Ufundi cha Norway cha Trondheim (NTNU).
Shahada nyingine ya kwanza katika Kemia ya Petroli (B.Sc. Petroleum Chemistry) inatolewa katika Idara ya Kemia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilianza kutoa shahada ya kwanza katika Uhandisi wa Petroli (B.Sc. Petroleum Engineering) ambayo inatolewa katika chuo kishiriki cha Sayansi za Ardhi kuanzia mwaka wa masomo 2012/2013.
Shahada hiyo inazingatia vigezo vya shahada kama hiyo zitolewazo nchini Marekani, Norway, Saudi Arabia na India.
Aidha, Chuo cha Madini Dodoma (MRI) nacho kilianza kutoa Stashahada (Diploma) katika sayansi ya petroli (Petroleum Geo-Science) mwaka huo huo wa 2012/13.
Shahada ya Uzamili
Kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi cha Norway cha Trondheim (NTNU), Chuo kishiriki cha Uhandisi na Teknolojia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CoET) kinatoa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Petroli na Uhandisi (M.Sc Petroleum Geo-Science and Engineering).
Shahada hiyo ni sehemu ya programu ya nchi ya Norway iitwayo ANTHEI (Angola, Norway, Tanzania Higher Education Initiative – Mkakati wa Elimu ya Juu nchini Angola, Norway na Tanzania) kwa shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu (PhD) tangu katikati ya mwaka 2013, iliyokuwa inagharamiwa na kampuni ya Statoil ambayo ilitenga Dola za Marekani milioni 2.3 katika mradi huo hadi mwaka 2017.
Shahada hiyo ni ya miaka miwili ambayo inampatia mwanafunzi nafasi ya kufanya masomo yake nchini Norway kwa mwaka mmoja na mwaka mmoja mwingine nchini Tanzania.
Uandikishaji wa wanafunzi
Hadi Oktoba 2013, mwanzoni kabisa mwa programu hiyo, wanafunzi 72 waliandikishwa katika shahada za kwanza zinazohusiana na sayansi ya petroli katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kila mwaka, wanafunzi 10 wanatarajiwa kushiriki katika shahada ya pili chini ya program ya ANTHEI.
Mwaka huo pia katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wanafunzi 115 waliandikishwa, na wanafunzi 110 waliandikishwa katika Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Ni wazi programu hii inaendelea hadi sasa miaka 10 baadaye, hii ikiwa na maana kwamba, vijana wa Kitanzania wengi wamekwishapata elimu ya mafuta na gesi asilia.
Mipango ya baadaye ilieleza kwamba, Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) kwa msaada wa kampuni ya Statoil ilikuwa imeanzisha programu kuhusu usimamizi wa fedha na uchumi katika sekta ya mafuta; program ya ANTHEI ikihamishiwa moja kwa moja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; na Idara ya Kemia na Uhandisi wa Madini ilikuwa na mpango wa kuzindua shahada ya pili katika mafuta na gesi (M.Sc. Oil and Gas).
Kwa upande mwingine, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) iliyopo Arusha ilikuwa imefanya majadiliano na kampuni ya BG Group Tanzania kabla kampuni hiyo ya Uingereza haijanunuliwa na kampuni ya Royal Dutch Shell ya Uholanzi, ili wanafunzi wa chuo hicho wapatiwe nafasi ya kufanya mazoezi kwa vitendo kwenye kampuni hiyo.
Pamoja na mpango huo, taasisi hiyo pia ilipanga kuanzisha ufadhili wa shahada ya juu kwenye eneo la Petroli. Haijajulikana baada ya kununuliwa kwake kama Shell inaendelea na programu hiyo au la.
Nacho Chuo cha Madini Dodoma (MRI) kilikuwa na mpango wa kujumuisha programu ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi pamoja na Jiolojia ya Petroli katika mtaala wake.
Aidha, Chuo kishiriki cha Sayansi za Ardhi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeanzisha shahada nyingine ikiwa ni pamoja na Shahada ya Sayansi katika Jiolojia ya Petroli, Shahada ya Uzamili katika Jiolojia ya Petroli, Uhandisi wa Akiba ya Petroli, na Uhandisi wa Uzalishaji wa Petroli.
Hata hivyo, utafiti wa hali halisi ya mafunzo ya mafuta na gesi uliofanywa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Norway (NORAD) unaonyesha kwamba elimu na mafunzo ya gesi na mafuta yanayotolewa na vyuo vikuu nchini unakabiliwa na changamoto kadhaa.
Miongoni mwa changamoto hizo ni Mafunzo kujikita sana kwenye eneo la utafutaji na uzalishaji, na kuacha maeneo mengine kama uhifadhi na usafirishaji; ukosefu wa walimu wenye ujuzi; ukosefu wa maabara na vifaa; na kuegemea kwenye nadharia zaidi kuliko vitendo.
Elimu ya Ufundi Stadi
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilianzishwa na Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 1994 ambapo VETA inaratibu, kusimamia, kufadhili, kuchochea na kutoa elimu ya ufundi nchini.
Kwa mujibu wa Ibara ya 4(c), VETA ina wajibu wa kuhakikisha uwepo wa uhakika wa wataalamu kwenye soko la ajira ili kuongeza uzalishaji na kuchochea uchumi.
Ugunduzi wa gesi nchini bila shaka umechochea mjadala kuhusu uwepo wa Watanzania wenye weledi wa kutosha kwenye sekta ya gesi nchini ambayo inahitaji wataalamu wengi kwenye eneo la utafiti, uchimbaji, uchakataji, na usafirishaji.
Orodha hiyo pia inajumuisha shughuli nyinginezo kama usalama wa afya na mazingira, ambazo pia zinahitaji watu wenye taaluma ambao kwa hakika hawapatikani kwa urahisi nchini.
Ugunduzi wa gesi mkoani Mtwara na Lindi ni fursa ya pekee kwa VETA kuandaa Watanzania wenye weledi wa kutosha unaohitajika kwenye sekta hiyo.
VETA iko katika nafasi nzuri ya kuandaa na kukuza nguvu kazi yenye weledi miongoni mwa vijana kutokana na ukweli kwamba ina miundombinu na vifaa vya ufundishaji katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambako gesi imegunduliwa, inapata msaada mkubwa kutoka serikali kuu na serikali za mitaa, ina mtandao mpana wa wadau takriban kila mkoa nchini, na pia ina uzoefu mkubwa wa kuendesha na kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwenye sekta mbalimbali nchini.
Kutokana na wajibu wake kisheria, tayari VETA ilianzisha mradi wa kukuza uwezo wa kuajiriwa kupitia elimu ya ufundi stadi mkoani Mtwara kwa kushirikiana na kampuni ya BG Group (sasa Shell Oil) na taasisi ya Volunteer Service Organisation (VSO).
Mradi huo ulikuwa wa miaka mitatu, ambao ulipata msaada wa kifedha wa Dola za Marekani milioni 1 kutoka kampuni ya BG Group, ulilenga kuimarisha uwezo wa kuajiriwa kwa wakazi wa Mtwara na Lindi pamoja na mikoa mingine kwa kuongeza kiwango cha ufundishaji katika kituo cha VETA Mtwara.
Malengo ya muda mfupi ya mradi huo yalikuwa ni pamoja na kukuza uwezo wa ufundishaji kwa walimu 24 wa VETA kwenye maeneo yao waliyojikita; kuwawezesha walimu 24 wa mafunzo ya ufundi kupata cheti cha ngazi ya pili cha kimataifa cha lugha ya Kiingereza; kuwawezesha walimu 7 wa VETA kupata elimu ya shahada ya kwanza kwenye maeneo mbalimbali; kuwawezesha wanafunzi 280 wa VETA kupata vyeti vya kimataifa kwenye maeneo mbalimbali ya kitaaluma na zaidi ya asilimia 50 miongoni mwao kujihusisha na shughuli za sekta ya mafuta na gesi; na wafanyakazi watawala 5 kutoka VETA Mtwara kupatiwa mafunzo ya utawala na stadi za uongozi.
Matokeo ya mradi huo yanajumuisha kukuza viwango vya ubunifu na ufundi stadi kwa ngazi ya kimataifa kwenye maeneo yafuatayo: useremala, utengenezaji na uunganishaji wa mabomba, uchomeleaji, utengenezaji magari, ufundi umeme, uzalishaji wa chakula, utaalamu wa maabara, na lugha ya Kiingereza.
Maeneo mengine ni kukifanya kituo cha VETA Mtwara kuwa kituo chenye ubora kwenye utoaji wa mafunzo yanayohusiana na sekta ya mafuta na gesi na shughuli nyingine zinazohusiana na sekta hiyo na kuhakikisha wahitimu wa VETA wanaajiriwa na kampuni za mafuta na gesi na kampuni nyingine zinazojishughulisha na sekta hiyo.
Aidha, wananchi wa Mtwara pamoja na Tanzania kwa ujumla wanapaswa kufaidika kutokana na kuongezeka uwezo wa kuajiriwa na kwa hiyo kuongezeka kwa kipato, ambapo kutokana na umuhimu wake, mradi huo pia utarejewa kwenye mikoa mingine kupitia mitandao ya VETA kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanafaidika.
Changamoto
Pamoja na jitihada nzuri za VETA za kuandaa wataalamu kwenye sekta ya mafuta na gesi, changamoto kadhaa zinaendelea kuwepo ukizingatia uchanga wa sekta hiyo nchini.
VETA inakabiliwa na uwezo mdogo wa kuandaa wataalamu kwa ngazi ya kimataifa kwenye sekta hiyo, shida ambayo baadhi ya wachambuzi wanaihusisha na “ukosefu wa mkakati wa kitaifa wa kuandaa rasilimali watu kwenye sekta ya gesi nchini.”
Changamoto nyinginezo ni pamoja na uwezo mdogo miongoni mwa walimu wa VETA; kukosekana uwiano kati ya mafunzo yanayotolewa na VETA kama ufundi wa kuchomelea, useremala na kadhalika na mahitaji halisi ya sekta ya mafuta na gesi.
Kwa ujumla, kozi zinazotolewa na VETA zinapaswa kuendana na viwango vya kimataifa, ingawa ni ukweli ulio wazi kwamba, Tanzania bado haijaweza kujenga uwezo wa kutoa mafunzo ya teknolojia ya kisasa kwenye sekta ya mafuta na gesi na kwa hiyo, vyuo vya ufundi stadi lazima vishirikiane na vyuo vinavyotambulika duniani ili kukuza mafunzo ya teknolojia.
Tanzania ina rasilimali nyingi za gesi na bado ina wataalamu wachache sana katika eneo hili. Kwa hiyo, ni muhimu serikali ikaanzisha vyuo maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.