*DCPC yakoshwa na uongozi wake
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), kimempa tuzo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakiunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali anayoingoza na kutambua mchango wake katika kuboresha tasnia ya habari.
Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia wakati wa Mkutano wa mwaka wa chama hicho mwishoni mwa wiki.
Chalamila alisema Mkoa unawategemea waandishi wa habari kufanya maendeleo, kumpa ushauri wa nini wangependa kuona kinafanyika ili Mkoa uwe wa kuvutia.
Alisema Mkoa huo umeomba sh. bilioni 8 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme ili biashara katika eneo la Kariakoo ifanyike kwa saa 24.
Alieleza kuwa, fedha zilizoombwa ni za kubadilisha nyaya kwani zilizopo ni za zamani, kufunga swichi za kielekroniki ili umeme utakapokatika eneo hilo uendelee kuwaka.
Aliongeza kuwa, wiki ijayo, Uongozi wa Mkoa utakutana wadau mbalimbali kulingana na namna watakavyoweza kufanya biashara hiyo.
Akizungumzia sababu za kumpa Rais tuzo hiyo, Katibu wa DCPC, Fatma Jalala, alisema chini ya utawala wake, Rais Dkt. Samiaa amefanya maboresho mbalimbali.
Mamboresho hayo ni pamoja na kuiunganisha Wizara ya Habari na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuleta tija na ufanisi.
“Ametimiza ahadi ya kurekebisha sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016, tunaamini ataendelea kuiboresha ili kukidhi mahitaji ya wadau na kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji,” alieleza.
Awali akimkaribisha Chalamila, Makamu Mwenyekiti wa DCPC, Salome Gregory, aliahidi chama hicho kuendelea kumpa ushirikiano ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na Mkoa, Taifa kwa ujumla.