Vigogo UDA warudishwa gerezani

*Kesi yao kutajwa tena Novemba 13

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

UPELELEZI wa kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Simon Bulenganija na wenzake William Kisena na Leonard Lubuye haujakamilika.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mashtaka hayo ni pamoja na kughushi mkataba wa kukodisha eneo la UDA kwa kampuni ya Simon Group Limited hivyo kulisababishia shirika hilo hasara ya sh. bilioni 14 katika kesi ya uhujumu uchumi 29/2023.

Washtakiwa wanadaiwa kughushi mkataba wa kukodisha eneo la UDA lenye ukubwa wa ekari 13 lililopo Kurasini kwa Kampuni ya Simon Group Limited.

Kampuni hiyo ilitakiwa kulipa sh. milioni 400 kila mwaka kwa miaka 10 wakati wakijua hati hiyo ya mkataba ni ya uongo.

Jana wakili wa serikali, Fatma Waziri na mwenzake Veronica Chimwanda, waliieleza mahakama hiyo kuwa inaendelea na upelelezi dhidi ya washtakiwa.

Shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kutajwa hivyo waliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika.

Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate anayesikiliza shauri hilo, baada ya kusikiliza maelezo hayo aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 13, 2023.

Washtakiwa walirudishwa gerezani kutokana na shtaka kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *