Tulia: Siri ushindi IPU ni Rais Samia

*Aeleza jinsi alivyomuunga mkono

*Zungu asema Dkt. Tulia alijiongeza

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye shujaa wa safari ya ushindi wake wa Urais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Alisema asingegombea nafasi hiyo bila Rais Dkt. Samia kuridhia na kumuunga mkono kuanzia mwanzo wa safari, wakati wa kampeni hadi kupata ushindi huo.

Dkt. Tulia aliyasema hayo jijini Dodoma jana kwenye kwenye hafla ya mapokezi yake akitokea jijini Luanda, nchini Angola baada ya kushinda nafasi hiyo.

Alieleza kuwa, ili uweze kugombea nafasi hiyo lazima nchi yako ikuruhusu na mtu anayeruhusu ni kiongozi wa Taifa husika kama alivyofanya Rais Dkt. Samia.

“Kama Rais Dkt. Samia asingeridhia, ushindi huu usingekuja Tanzania, ilikuwa nirudi kesho (leo) lakini kitendo cha Rais Dkt. Samia kuridhia ushindi wangu, nimeweza kurejea leo (jana),” alisema.

Alilishukuru Bunge la Tanzania kwa kumtia moyo kipindi chote cha mchakato huo na kumwezesha kuingia kwenye historia ya dunia Tanzania ikitoa Rais wa IPU.

“Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kurudhia nigombee nafasi hii, sisi sote tuliopo hapa na wengine ambao hawapo, kila mmoja ameshiriki kwa nafasi yake.

“Wengine wameshiriki kwa kutoa michango ya maoni, wengine wametoa michango ya maombi, wengine fedha, kututia moyo.

“Pia wapo waliotukatisha tamaa ambao nao nawashukuru kwa sababu walitufanya tupige hatua kwa haraka zaidi ili tuhakikishe tunalifikia lengo tulikuwa nalo,” alisema.

Akizungumzia safari yake ya uspika, alisema aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Spika katika kipindi cha utawala wa Rais Dkt. Samia.

“Nimshukuru Rais Dkt. Samia kwa imani ya kunichagua kuwa Spika na sasa nimeenda kugombea nafasi ambayo leo imetukusanya hapa.

“Namshukuru sana kwa sababu bila yeye hii nafasi nisingeweza kwenda kugombea,” aliongeza.

Dkt. Tulia alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa namna alivyoweza kutengeneza rekodi ya kipekee ya uongozi wake katika mambo makubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi cha uongozi wake madarakani.

“Hatumpongezi Rais Dkt. Samia kwakuwa ni mwanamke bali ni kwa ujasiri na uwezo wake binafsi, tukisema kazi inaendelea chini ya uongozi wake, matokeo yake yanayonekana,” alieleza.

Alisema Rais Dkt. Samia amefanikiwa kuimarisha ujenzi wa miundombinu, uwekezaji, kukuza demokrasia nchini.

Alimtaja Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro kwa kumshika mkono akiwa mwanafunzi wake kuanzia chuoni akisoma mwaka wa pili, baadae kufundisha pamoja hadi kufika nafasi ya kuteuliwa katika ujumbe wa Bunge la Katiba.

“Sijawahi kumtaja katika hadhara, Dkt. Migiro amekuwa na mchango mkubwa sana wa mimi kufika hapa kuanzia nikiwa chuoni, naomba nimshukuru sana,” alisema.

Aliahidi kuandaa kitabu cha kuelezea historia ya maisha yake na safari yake ya kuingia kwenye siasa hadi kuwa Rais wa IPU.

NAIBU SPIKA

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Azzan Zungu, alisema kilichomfanya Dkt. Tulia achaguliwe kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ni uadilifu, kujiamini, nidhamu yake, hatua ya Rais Dkt. Samia kuimarisha diplomasia ya mataifa ya nje.

Zungu aliyasema hayo jana katika hafla ya mapokezi ya Dkt. Tulia aliyewasili nchini akitokea nchini Angola ambako uchaguzi ulifanyika Ijumaa iliyopita.

“Sifa ya mtu kushinda, hashindi kwa sababu ya kujua, kuna vitu vitatu…uadilifu, kujiamini, nidhamu ambapo maswali aliyokuwa akiyajibu yamewafanya watu waingiwe na aibu.

“Wenzake walikuwa kama wanaharakati, wakiulizwa swali la maana hawana majibu…kubwa zaidi ni Mungu na msaada kutoka kwa Rais Dkt. Samia.

“Dkt. Tulia alijiongeza, majibu ya mazingira anayo, haki za binadamu yapo, demokrasia duniani iko kichwani, isingekuwa rahisi kukosa ushindi,” aliongeza.

Katika uchaguzi huo, Dkt. Tulia alishinda kwa kura 172 dhidi ya 303 zilizopigwa na wajumbe wa IPU.

Washindane wake Catherine Hara kutoka Malawi alipata kura 61, Margane Kanoute wa Senegal kura 59 na Abdibadhir Hagi wa Somaria kura 11.

RAIS DKT. SAMIA

Baada ya kushinda nafasi hiyo, Rais Dkt. Samia alipongeza Dkt. Tulia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Raia Dkt. Samia alisema kuchaguliwa kwake kunaonesha ushuhuda wa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, imani ya wajumbe juu yake na taifa kwa ujumla.

“Kuchaguliwa kwako pia ni matokeo ya miaka mingi ya kazi, weledi na kujituma katika utumishi wa umma, mfano bora kwa watoto wa kike katika nchi yetu, Afrika hata nje ya mipaka ya bara letu.” aliandika Rais Dkt. Samia kwenye mtandao wa X.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *