Mchengerwa aitaka TARURA iendeleze Wakandarasi wazawa

Na Sarah Moses, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, ameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kuwaendeleza Wakandarasi wazawa waweze kufikia viwango vya kimataifa vya ubora na usalama.

Mchengerwa aliyasema hayo juzi jijini Dodoma katika kikao kazi cha watumishi wa TARURA.

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inawanyanyua Wakandarasi wazawa na kusisitiza, TARURA wanalo jukumu la kuwaendeleza Wakandarasi wazawa.

Aliongeza kuwa, TARURA inapaswa kuzishika mkono kampuni 20 za wazawa kila Mkoa ili kufungua uchumi na kuifanya mikoa yote istawi, kuimarisha kazi za Wakandarasi hao kwa kila Mkoa.

“Mikakati ya TARURA ni kuhakikisha ifikapo 2025 wawe wameboresha barabara za vijijini na mijini kwa asilimia 85, wakati tunaenda kuyafikia mafanikio hayo lazima tujiulize tumewakuza, kuwajenga Wakandarasi wangapi wazawa”

“Lazima tujue tumewanyanyua kiasi gani ili kufikia viwango vya kuwafanya washindane kimataifa, pamoja na majukumu mengi yanayoikabili TARURA, katika uongozi wangu jukumu la kukuza, kuwaendeleza wakandarasi wazawa nitalipa kipaumbele.

“Niwapa jukumu TARURA mnisaidie katika hili ili tunakokwenda tuwe tumewajenga Wakandarasi angalau kila Mkoa kampuni za wazawa 20, tutakua kumekuza Kampuni 520 katika mikoa yote 26,” alisema.

Mkakati huo umelenga kuziwezesha kampuni za wazawa za ujenzi ili ziweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi inayotangazwa na TARURA.

Lengo kuu la mpango huu ni kuboresha mazingira ambayo mjasiliamali wa Kitanzania anaweza kufaulu, kukua, kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.

Pia mpango huo umelenga kuijenga Tanzania yenye nguvu inayojitegemea ambayo inaweza kukabiliana na changamoto za karne ya 21 kwa kutumia uwezo wa Wakandarasi wa ndani.

Pamoja na hayo, Mchengerwa aliiagiza TARURA kuandaa utaratibu wa wazi wa namna ya kuzichangua kampuni 20 kwa kila mkoa, kusisitiza mchakato wa haki.

“Kuna tuhuma za Wahandisi kuwa na kampuni ya ujenzi na kujipa kazi wenyewe au kuuza vifaa vya ofisi, naomba mjiepushe na mgongano wa kimaslahi na rushwa,

“Hii ni moja ya sababu ya Bodi za Zabuni za TARURA kulalamikiwa katika ngazi mbalimbali wakiwemo Wabunge,” aliopngeza Mchengerwa.

Changamoto nyingine ni baadhi ya Wataalamu kutosimamia kazi kwa weledi, kuzingatia masharti ya mikataba jambo ambalo husababisha kazi kutokamilika kwa wakati na ubora ulioanishwa katika mikataba.

Pia kutofanya usanifu kwa ukamilifu hivyo kusababisha ongezeko la kazi wakati wa utekelezaji, kutozingatia vipengele muhimu vya mikataba.

Vipengele hivyo vinataka Makandarasi kuwasilisha dhamana za malipo ya awali, dhamana ya utendaji.

“Jambo hili linaweza kuifanya Serikali ishindwe kurejesha fedha zake hivyo kupata hasara pale Mkandarasi anaposhindwa kazi.

“Mnapaswa kuhakikisha nyaraka halali za dhamana kwa ajili ya malipo ya awali zinawasilishwa, dhamana za utendaji kazi, kufuatilia zinapomaliza muda wake wakati muda wa mradi haujakamilika zihuishwe,” alisema

Baadhi ya wataalam kutofanya mapitio ya usanifu unaofanywa na Wataalam Washauri (consultant) hivyo kuwepo makosa, kusababisha madai ya ziada (variations).

“Ni wajibu wa watalaamu wa ujenzi kupitia usanifu (design review) pale usanifu unapofanywa na wataalamu wa nje ili kujiridhisha na usahihi kabla ya kazi kuanza,” alisema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, alisema wataendelea kuyafanyia kazi maagizo yote ili kutimiza malengo yao.

Alisema watashirikiana na Bodi ya Wakandarasi nchini, taasisi za kifedha ili kukuza Wakandarasi wazawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *