* Siku za usafiri bila viza kuongezwa
* Hati sita zasainiwa, ujenzi wa mpaka
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, jana amelihutubia Bunge la Zambia akitoa hotuba iliyowakosha wabunge wakati akihitimisha ziara ya siku tatu nchini humo.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia alisema Serikali ya Tanzania inatarajia siku za usafiri bila viza kwa wananchi wa Zambia wanaoingia nchini kutoka siku 90 hadi 190.
Uamuzi huo utatoa uhuru wa usafiri kwa rais wa Zambia kuingia nchini, kukaa siku 190 bila kununua viza.
Rais Dkt. Samia alisema lengo la uamuzi huo ni kurahisisha usafiri na usafirishaji watu kati ya nchi hizo na hatimaye kufungua milango ya biashara.
“Ninayo furaha ya kulitaarifu Bunge hili tukufu kuwa, Serikali ya Tanzania inajiandaa kuwezesha usafiri wa watu bila viza kwa kuongeza muda wa kuingia nchini kutoka siku 90 hadi 190,” alieleza.
Aliongeza kuwa, Tanzania ipo tayari kusaidia ujenzi wa mpaka wa Zombe ili kurahisisha usafiri wa watu pamoja na usafirishaji bidhaa kati ya mataifa hayo.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo na watu wake kwa ujumla.
“Ni muhimu wabunge wa mataifa haya ambao ndiyo wawakilishi wa wananchi, kuhakikisha wanapitisha mipango ya bajeti zinazowasilishwa na serikali kwa manufaa ya umma.
“Kama wabunge hawatashawishika au wakiamua kufanya siasa dhidi ya mipango hii, wataathiri maendeleo tuliyofikia Watanzania na Wazambia,” alisema.
Alifafanua kuwa, mrejesho unaopatikana kutoka kwa watu mbalimbali ni kwamba, mifumo ya kisheria baina ya nchi hizo itakuwa rafiki kwa biashara kama mataifa hayo hayataingiza siasa katika mipango yao.
Alisema Serikali zinapowasilisha mapendekezo ya kuondoa vikwazo vya kikodi au ushuru, wabunge wanapaswa kujua msaada wao unahitajika.
Rais Dkt. Samia alisema mipango ijayo ya serikali ni kujengwa miradi mipya ya miundombinu kwa ushirikiano ambapo biashara kati ya Tanzania na Zambia itakuwa kutokana na juhudi mbalimbali ikiwemo kuboreshwa Bandari ya Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa, uhusiano uliopo kati ya mataifa hayo ni wa kihistoria uliobebwa na waasisi wake Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda wa Zambia.
Alisema upo muendelezo wa uhusiano baina ya mataifa hayo kwa kuwa yapo mambo yaliyobaki kama alama likiwemo bomba la mafuta la Tazama na Reli ya Tazara.
Serikali za nchi hizo zinafanya juhudi za kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili reli ya Tazara ili kurahisisha usafirishaji na kuongeza kuwa, ziara aliyoifanya nchini humo itaimarisha uhusiano.
KUSAINI HATI/MIKATABA
Katika hatua nyingine, Tanzania na Zambia zimesaini hati sita na mikataba miwili ya ushirikiano ikilenga kuboresha uwekezaji na biashara baina ya mataifa hayo.
Rais Dkt. Samia na mwenyeji wake, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema walishuhudia uwe kaji saini katika hati hizo, upande wa Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, Zambia ikiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Stanley Kakubo.
Hati zilizosainiwa ni ushirikiano kuhusu mradi wa usafirishaji gesi asilia kutoka Tanzania kwenda Zambia, hati ya makubaliano kati ya mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania na Wakala wa Maendeleo Zambia.
Zingine ni ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Maendeleo Zambiana hati ya ushirikiano kati ya Tanzani na Zambia katika sayansi, teknolojia na ubunifu.
Pia ulisainiwa mkataba wa utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu program ya kubadilisha wanafunzi wa kozi ya ukandarasi na unadhimu.
Akizungumza baada ya kushuihudia utiaji saini, Rais Hichilema alisema Serikali yake itafanya linalowezekana kuhakikisha makubaliano hayaishii katika makaratasi.
Alitumia fursa hiyo umshukuru Rais Dkt. Samia kwa zawadi ya hecta 20 za ardhi na kuahidi kuwa, eneo hilo litatumika vizuri katika kukuza, kuendeleza biashara ndani ya nchi hiyo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa nchi ya Zambia kuitumia Bandari ya Dar es Salaam ili waweze kuondokana na gharama za kuhifadhi mizigo badala yake itahifadhiwa katika bandari kavu yao.
Naye Rais Dkt. Samia alisema kupitia ziara hiyo Tanzania na Zambia zimepata njia ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo utatuzi wake utasaidia kukuza biashara na ushirikiano wa kiuchumi.