Uwekezaji Bandari na mkakati wa ajira milioni nane za Samia

Na Daniel Mbega,

Kisarawe

UWEKEZAJI wa kampuni ya DP World ya Dubai kwenye Bandari ya Dar es Salaam unatarajiwa kuzalisha takriban ajira mpya 42,917, idadi ambayo itafanya kuongezeka kwa ajira kutoka 28,990 za sasa hadi ajira 71,907.

Ongezeko hili linaleta matumaini makubwa ya namna Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inavyojitahidi kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira, ambayo imezikumba nchi nyingi duniani.

Wakati ambapo mataifa makubwa ulimwenguni yanawaza kupunguza ajira za mamilioni ya watu kwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI), Rais Samia anatafuta fursa mpya za ajira katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Itakumbukwa kwamba, Ripoti ya benki ya uwekezaji ya Goldman Sachs, ilisema kwamba, teknolojia ya akili bandia inaweza kuchukua nafasi za kazi za kudumu saa na milioni 300.

Ikaelezwa kwamba, AI inaweza kuchukua nafasi karibu robo ya kazi nchini Marekani na bara lote la Ulaya lakini inaweza kumaanisha pia kutengeneza nafasi mpya za kazi na kuongeza tija pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa na huduma kwa kila mwaka zinazozalishwa duniani kote kwa 7%.

Ripoti hiyo ikasema, akili bandia ya uzalishaji, yenye uwezo wa kuunda maudhui yasiyoweza kutofautishwa na kazi ya binadamu, ni “maendeleo makubwa”.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Uingereza ina nia ya kuongeza uwekezaji katika teknolojia ya akili bandia, ambayo inasema “hatimaye italeta tija katika uchumi wote”, na imejaribu kuwahakikishia umma kuhusu athari zake.

Kitu pekee ambacho hakijulikani ni kwamba hakuna njia ya kujua ni kazi ngapi zitaathiriwa na zitafanywa na akili bandia (AI) ya uzalishaji.

Waandishi wa habari watakabiliwa na ushindani zaidi, ambao unaweza kupunguza mishahara yao, vinginevyo labda kuwe na ongezeko kubwa la mahitaji ya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti uliotajwa na ripoti hiyo, asilimia 60% ya wafanyakazi wako kwenye kazi ambazo hazikuwepo mwaka 1940.

Lakini utafiti mwingine unaeleza kuwa mabadiliko ya kiteknolojia tangu miaka ya 1980 yamewahamisha wafanyakazi kwa kasi zaidi kuliko ilivyozalisha ajira.

Na ikiwa AI ya uzalishaji ni kama maendeleo ya awali ya teknolojia ya habari, ripoti hiyo inahitimisha kuwa, inaweza kupunguza ajira katika muda mfupi ujao.

Jitihada za Rais Samia

Wakati mabadiliko hayo yanafikiriwa kufanyika kwenye mataifa makubwa kabla ya kusambaa kwenye nchi zinazoendelea, Rais Samia na chama chake cha CCM wanafikiria namna ya kutengeneza ajira mpya kwa vijana na wanawake ili kukuza uchumi.

Hatua ya kuruhusu uwekezaji kwenye Bandari inamaanisha kwamba, kuna fursa nyingi zitakazopatikana, kuanzia ajira za kudumu hadi za muda mfupi.

Kwa mfano, ukiacha ajira hizo 43,000 zitakazozalishwa kwenye sekta hiyo, bado ziko fursa nyingine nyingi kwa jamii kupata ajira.

Fikiria ni ajira ngapi zitakazozalishwa wakati Zambia itakapoanza kujenga Bandari Kavu katika eneo la Kwala wilayani Chalinze baada ya Rais Samia kuipatia nchi hiyo jumla ya hekta 20 (ekari 50).

Zambia ni miongoni mwa nchi zinazoitegemea Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha shehena yake – iwe kutoka ama kwenda ng’ambo – hivyo kuwa na Bandari Kavu maana yake itaondoa usumbufu wa namna ya kuhifadhi mizigo yao kabla ya kusafirisha.

Kwa mujibu wa taarifa kutka serikalini, nchi nyingine kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Malawi na Rwanda zitapewa heka 10 (ekari 25) kila moja kwenye eneo la Bandari Kavu ya Kwala ili kuhifadhi mizigo yao.

Na kwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar ess Salaam baada ya uwekezaji wa DP World, maana yake ni kwamba, kutakuwepo na mizigo mingi ambayo inaweza kutoka kwa wakati mmoja bandarini lakini ikahitaji kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa, kwa sababu kuisafirisha kwa wakati mmoja nako kunaweza kuwa changamoto hata kama miundombinu inaruhusu.

Kwahiyo hapa unazungumzia ajira kwenye kampuni za wakandarasi watakaojenga, ambao watahitaji vibarua wa moja kwa moja, lakini pia wanajamii wa maeneo ya karibu watapata ajira nyingi ndogo ndogo, zikiwemo hata za mama na baba lishe, uuzaji wa nafaka pamoja na wanyama na ndege (ng’ombe, mbuzi na kuku) kwa ajili ya kitoweo, na kadhalika.

Ndiyo. Juzi Jumanne, Oktoba 24, 2023, Rais Samia akihutubia Sherehe za Miaka 59 ya Uhuru wa Zambia katika Ikulu ya Lusaka ambako alikuwa mgeni rasmi, alitoa zawadi kwa Zambia ya hekta 20 katika eneo la Kwala mkoani Pwani, kwa ajili ya kurahisisha uchukuaji wa mizigo bandarini.

Pamoja na hayo, Rais Samia akasema Tanzania imetengeneza mazingira mazuri ya ushirikiano na Zambia katika maeneo zaidi ya sita ikiwemo biashara, miundombinu na kujenga bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Zambia.

Maeneo mengine aliyotaja ni kwa pamoja nchi hizo kuhamasisha amani katika nchi za Afrika na Dunia kwa ujumla na kuendeleza miradi iliyopo ukiwemo wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).

Alisema kupitia mipango ya Tanzania ya kurahisisha zaidi biashara kati ya nchi hizo mbili, serikali imetenga eneo hilo la Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo inayopelekwa Zambia.

“Zaidi ya hayo, Zambia itawezeshwa kwa muda mrefu zaidi wa kuhifadhi bila malipo mzigo ambao unaenda hadi siku 45. Hatua hii itapunguza msongamano na ucheleweshaji, na hatimaye kupunguza gharama za kufanya biashara nchini Zambia,” alisema na kuongeza kwamba, hatua hiyo inatarajia kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili na kutengeneza fursa zaidi za kibiashara kwa wananchi wa pande zote mbili.

“Hii ni zawadi kutoka Tanzania unaposherehekea uhuru wako,” alisema Rais Samia na kushangiliwa na wananchi wa Zambia.

Akasema, Serikali yake imeanza uboreshaji wa mitambo ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuhakikisha bandari hiyo inafanya kazi kwa ufanisi, kwa wakati na bila vikwazo katika shughuli zake.

“Ningependa kutoa wito kwa jumuiya ya wafanyabiashara nchini Zambia kuchangamkia fursa hii ya kipekee,” alisema.

Kwahiyo basi, fursa hii ya Bandari Kavu ya Zambia pale Kwala inamaanisha kwamba ajira zaidi zitazalishwa, ikiwemo kwenye sekta nzima ya usafirishaji.

Hapo bado hujazungumzia kuhusu nchi nyingine kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Burundi na Rwanda ambazo nazo zinaitegemea Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha shehena zao za mizigo.

Sehemu ya ajira milioni 8

Uzalishaji wa fursa hizi za ajira ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita ambapo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 imeahidi kwamba, Serikali itazalisha ajira zaidi ya milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi hadi kufikia mwaka 2025.

Ipo miradi ya kimkakati inatarajia kuzalisha sehemu ya ajira hizi, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, Uwanja wa Mpira Dodoma, Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda sambamba na ajira za moja kwa moja serikalini.

Sekta ya kilimo itaendelea kuongoza katika kutoa ajira ikifuatiwa na Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ofisi ya Waziri Mkuu, Afya, Utumishi wa Umma, Uvuvi, Madini, Viwanda na Biashara na Maliasili na Utalii.

Hii inatokana na ukweli kwamba, ukuaji wa uchumi wa viwanda unategemea zaidi malighafi za kilimo, ambapo wananchi wengi wataendelea kujikita kwenye sekta hiyo kuongeza uzalishaji wa mazao yanayohitaji kuchakatwa.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba, utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha kuanzia 2016/17 hadi robo ya pili ya 2019/20 ulizalisha jumla ya ajira 12,602,526, ambapo kati ya hizo ajira 11,721,172 zilikuwa za moja kwa moja na ajira 881,354 zisizo za moja kwa moja.

Sekta ya kilimo ndiyo iliyoongoza kwa kuzalisha ajira 4,968,859 za moja kwa moja, ikifuatiwa na Tamisemi (ajira 2,473,647), Ofisi ya Waziri Mkuu (1,823,106), Afya (1,283,407), Utumishi wa Umma na Utawala Bora (627,676), Uvuvi (535,473 zikiwemo ajira 500,000 za muda), Madini (332,468), Mawasiliano (192,069), Ujenzi (104,844), Viwanda na Biashara (86,246), Maliasili na Utalii (61,296), Mifugo (36,238) na Uchukuzi (24,611).

Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2020-2025 imeainisha vipaumbele sita vikuu.

Vipaumbele hivyo vikuu kwenye Ilani ni; Kulina nda kuimarisha misingi ya heshima, usawa, haki na utawala bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa; Kukuza uchumi wa kisasa, mshikamano, jumuishi na shindani unaojengwa juu ya msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi; Kubadilisha kilimo, mifugo na uvuvi ili kuhakikisha usalama wa chakula na usalama wa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.

Nyingine ni; Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini; Kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na uvumbuzi kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi; na Kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 (milioni nane) katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa vijana.

Katika kukuza uchumi, Ilani hiyo inaeleza kuwa Serikali itaendelea kujenga na kukuza uchumi shindani hasa kupitia sekta za huduma za viwanda na uchumi zitakazowezesha ustawi wa wananchi wote.

Aidha, itaendelea kuimarisha miundombinu ya kimkakati ili kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli zao kwa ufanisi; kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kustawi pamoja na kuvutia wawekezaji kutoa mchango wa maana katika maendeleo ya nchi.

Serikali pia imedhamiria kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuhakikisha usalama wa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi.

Kwa msingi huo, mikakati iliyopo ni kuhakikisha tija inaongezeka katika uzalishaji wa chakula, mifugo na uvuvi kwa ajili ya usalama wa chakula na lishe; Kuongeza tija katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi hasa katika sekta ya viwanda na huduma; Kuimarisha ushirikiano ili kuongeza nguvu ya wazalishaji hasa katika kupata pembejeo na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi; na Kuimarisha miundombinu na kuongeza maeneo ya umwagiliaji katika kilimo ili kuzalisha mazao mengi kwa mwaka mzima.

Kwa upande wa ajira, Serikali ina mpango wa kuchochea ukuaji wa uchumi hasa katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi ikiwemo utalii.

Serikali ina mpango wa kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na taasisi za mikopo yenye riba nafuu na kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi wa Kitanzania.

Miradi mingi ya kimkakati inayotekelezwa imeendelea kutengeneza ajira nyingi kwa Watanzania, hasa vijana na wanawake, zikiwemo za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Kwa mfano, Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) katika Bonde la Mto Rufiji, umeajiri zaidi ya vijana 4,000 wa Kitanzania kutoka maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuzunguka eneo la mradi.

Aidha, mradi huo utakapofikia kilele, utaajiri zaidi ya Watanzania 6,000 na hivyo kuongeza ajira zisizo za moja kwa moja mfano chakula, malazi na mengineyo.

Hadi sasa wananchi wa Kijiji cha Kisaki kilichopo kilomita 60 kutoka eneo la mradi wamenufaika na mradi huo kwa kutafuta fursa za kufanya biashara na kukuza uchumi.

Ujenzi wa nyumba bora za kulala wageni pia umeongezeka Kisaki huku bei ya ardhi ikiongezeka maradufu.

Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pia umetoa ajira 18,000 kwa vijana wa Kitanzania hasa vijana wanaohusika moja kwa moja na mradi huo huku maelfu ya wengine wakinufaika kwa kufanya biashara kando ya mradi huo.

Utekelezaji wa Kanda Maalum ya Kiuchumi ya Bagamoyo (BSEZ) unatoa fursa ya ujenzi wa viwanda takriban 190 na baadaye 790, hatua ambayo siyo tu itaongeza ajira, bali kukuza uchumi wa Taifa kupitia ukusanyaji wa kodi za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, awamu ya kwanza ya mradi wa Bagamoyo SEZ itazalisha ajira 20,000 za moja kwa moja, ambapo mapato ya kodi ya Pay As You Earn (PAYE) yatakuwa makubwa kwa serikali kutoka eneo hilo hilo.

Wakati wa uzinduzi wa kampeni Program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) inayowahusisha vijana na wanawake, Rais Samia alisema program hiyo inatarajia kuzalisha ajira milioni 3.

Awamu ya kwanza ya program ya BBT imeshuhudia jumla ya vijana 812 – kati yao wanawake 282 sawa na asilimia 34.73 na wanaume 530 sawa na asilimia 65.27  – wakichaguliwa kujiunga na mafunzo na sasa wamepatiwa mitaji na maeneo ya kufanyia kilimo biashara kupitia mashamba ya pamoja (block farms).

Vijana hao walipatiwa mafunzo kwa kipindi cha miezi minne katika vituo 15 vilivyoandaliwa, ambapo Serikali iligharamia malazi, chakula na gharama za mafunzo.

Kwa maana hiyo, uwekezaji wa Bandari umekuja na fursa nyingi za ajira ambazo zinapita katika mkondo ule ule wa kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita kuzalisha ajira milioni 8 kufikia mwaka 2025 inatimia.

0629-299688

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *