‘Watanzania tuyakubali mabadiliko teknolojia duniani’

Na Saidi Salim, Arusha

WAKATI maendeleo ya teknolojia yakienda kasi duniani, Watanzania wametakiwa kuondoa hofu juu ya ujio wa teknolojia hiyo.

Kutokana na hali hiyo, jamii haina budi kukubaliana na mabadiliko hayo hivyo wawe tayari kujifunza mabadiliko ya teknolojia ili kuinua uchumi wa jamii na Taifa.

Mwakilishi na Mfanyakazi wa Kampuni ya Apple Inc ya  Marekani, Mtanzania Aboubakar Ally aliyasema hayo juzi katika ufunguzi wa wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) wakati akitoa mada ya maendeleo ya teknolojia duniani.

Aboubakar ambaye ni miongoni mwa Watanzania wachache wabobezi katika teknolojia amesema yeye na wenzake wameanzisha shamba la mbogamboga hekari 20 katika Mji wa Boston.

Pia wameweza kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia gesi kutokana na mji huo kuwa na baridi kali hivyo inawasaidia kuongeza hewa ya oksijeni.

“Teknolojia imetusaidia kuanzisha shamba eneo ambalo haliwezi kulimwa kutokana na hali yake ya hewa, bado tunaendelea kumalizia ujenzi wake.

“Tayari tumepata wateja wa mazao yetu, ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tunaingiza faida ya dola za Marekani milioni saba,” alisema.

Mkurugenzi wa Muungano wa AZAKI  (FCS), Francis Kiwanga, alisema kutokana na kasi ya mabadiliko yaliyopo katika sayansi na teknolojia Watanzania wanapaswa kubadilika, kuendana na kasi hiyo. Lengo ni kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, utoaji huduma na kujua aina bora ya teknolojia ya kuendana nayo, kujiepusha na athari zake.

“Mabadiliko ya teknolojia yanakuwa kwa kasi lakini  vijana wanapaswa kuangalia namna bora ya kuyaakisi bila kuathiri jamii ndio maana tunakuwa na mijadala kama hii ili kuchagua ni teknolojia gani inafaa na ipi haifai,” alisema Kiwanga.

Kwa upande wake, Mrajisi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Zanzibar, Ahmed Abdulah, alitoa rai kwa asasi za kiraia kuwa mstari wa mbele katika kubeba maono ya jamii kuwa na matumizi bora ya teknolojia.

“Ni jukumu letu kama asasi kuona jamii inachagua matumizi sahihi ya teknolojia, matumizi yanapokuwa sahihi yanaleta mtazamo chanya katika jamii,” alisema.

Tanzania imeendelea kushika kasi katika matumizi ya teknoloji, kukubaliana na mabadiliko hayo ili kuwa na mifumo bora yenye kurahisha utoaji huduma nchini kwa maendeleo ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *