Tanzania kushiriki Uchumi Madini ya Bahari – Mavunde

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Tanzania iko tayari kushiriki uchumi wa madini yaliyopo chini ya sakafu ya Bahari Kuu.

Lengo ni kuongeza vyanzo vingine vya madini katika mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.

Mavunde aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Wakandarasi waliowekeza kwenye Madini yanayopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu.

Alisema mkutano huo wa siku tatu ulioanza Oktoba 22 na kumalizika jana umelisaidia taifa kuongeza fursa nyingine katika uchumi wa madini, Tanzania itakuwa mshiriki mkubwa katika mnyororo mzima wa madini hayo.

“Wataalamu wa Serikali yetu kutoka Wizara na taasisi zinazohusika na uchimbaji madini wamepata fursa ya kuwaongezea ujuzi wa shughuli za madini ya bahari kuu,.

“Hili linaonyesha imani ya ISA (Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Bahari Kuu), Wakandarasi kwa Serikali yetu kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa sehemu ya 11 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS) pamoja na Mkataba wa 1994,” alisema Mavunde.

Aliongeza kuwa, Tanzania inasubiri kukamilika Sheria ya Kimataifa itakayopelekea kuanza uvunaji wa madini hayo kwa kuzingatia athari za kimazingira kwa viumbe hai wanaopatikana chini ya Sakafu ya Bahari Kuu.

“Mkutano huu umeifungua macho Tanzania kuhusu uwepo wa fursa hiyo, tunaipokea kwa mikono miwili kwa sababu ni wanachama wa ISA sambamba na kuitangaza sekta ya madini ya Tanzani,” aliongeza.

Mavunde alitumia fursa hiyo kuwakaribisha washiriki wa mkutano huo katika Mkutano wa Uwekezaji katika sekta ya madini Tanzani.

Mkutano huo una kaulimbiu inayosema; “Kufungua Uwezo wa Kuchimba Madini Tanzania kwa Baadaye” utafanyika kwa siku mbili, kuanzia Oktoba 25-26, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usimamizi wa Sakafu ya Bahari Kuu (ISA) Dkt. Marie Bourrel-MacKinnon alisema Tanzania itakuwa na mchango mkubwa katika uchumi utokanao na madini yaliyopo chini ya sakafu ya Bahari Kuu baada ya kukamilika kwa sheria.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali alisema kufanyika mkutano huo nchini ni matokeo ya uongozi na nzuri ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kulifungua taifa na fursa za uwekezaji nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David, alisema ni fahari kubwa kwa Tanzania kupewa nafasi ya kuandaa mkutano huo.

Mkutano huo utasaidia kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya madini nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *