Rais Samia aipa heshima Zambia

* Awapa zawadi eneo la hekari 20 Kwala

* Avunja ukimya maboresho Bandari Dar

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania itatoa eneo la hekta 20 kwa Zambia katika Bandari Kavu ya Kwala iliyopo katika Mkoa wa Pwani.

Eneo hilo litatumika kama kituo cha usafirishaji bidhaa kwa ajili ya Zambia ikiwa ni zawadi kwa Watanzania katika sherehe za Uhuru wa nchi hiyo.

Rais Dkt. Samia alitoa zawadi hiyo jana alipohotumia katika Sherehe za Miaka 59 ya Uhuru wa Zambi.

Alisema uamuzi huo utapunguza gharama za biashara katika Taifa hilo, kukuza biashara kwa nchi hizo.

Alieleza kuwa, Tanzania itaipa Zambia fursa ya kuhifadhi mizigo muda mrefu ili kupunguza gharama za biashara nchini humo, kuimatisha biashara baina ya nchi hizo.

“Tanzania na Zambia zitaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kunakuwa na usafiri, usafirishaji rahisi wa watu, bidhaa kutoka mataifa haya.

“Nazikaribisha jumuiya za wafanyabiashara wa Zambia katika kikao changu ninachotarajia kukifanya leo jioni,” alisema Rais Dkt. Samia.

Aliongeza kuwa, serikali yake imeweka juhudi za kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili iweze kuwa na ufanisi katika shughuli zake.

Aliziomba jumuiya za wafanyabiashara zione fursa hiyo ambayo ni ya kipekee sana.

Aliihakikishia Zambia kuwa, Tanzania itaendelea kuwa mshirika wake kama ilivyokuwa wakati wa mapambano ya Uhuru wa mataifa hayo mawili.

Kuhusu sherehe hizo, alisema zinakumbusha juhudi za waasisi wa mataifa ya Afrika jinsi walivyojitoa mhanga kuhakikisha Uhuru unapatikana.

Naye Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, alisema amani na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia ni jukumu la wakuu wan chi hizo na wananchi wake.

Alisema jukumu hilo haliepukiki, nchi hizo zina wajibu wa kuhakikisha zinadumisha amani na mahusiano yao kwa maslahi ya watu wote.

“Jambo hili linapaswa kusimamiwa, kuhakikisha amani, mahusiano yanakuwepo hata katika Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” alisema.

Rais Hichilema alitoa wito kwa viongozi wa nchi mbalimbali duniani kudumisha amani, umoja, kuepuka machafuko akirejea kinachoendelea Israel na Palestina.

“Kuhusu Israel na Gaza, kila kiongozi duniani ahakikishe anafanya kila namna kulinda amani katika nchi yake, ukanda na duniani,” alisema.

Aliongeza kuwa; “Tufanye hivi ili tujielekeze katika uwekezaji wa kibiashara, uchumi na maendeleo ya jamii,” aliongeza Rais Hichilema.

Alisema Serikali yake itaendelea kutumia rasilimali zake ili kuhakikisha zinaimarisha uchumi na maisha ya wananchi wake.

Rais Hichilema alisema, kwa sasa serikali yake inaendelea kubeba jukumu la kuboresha uchumi na uhuru wa kijamii, kuongeza viwango vya mishahara.

Pia kugawa rasirimali zilizopo kwa ajili ya uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi, kutengeneza ajira kwa watu wake, kutoa elimu bure.

Alisema tangu waanze kutekeleza sera ya elimu bure, madarasa yamejaa wanafunzi waliokuwa nje ya shule.

“Tutawahudumia wagonjwa, wenye ulemavu, wazee na wastaafu, tunaweza kufanya hivi vyote kwa kutumia rasirimali ambazo Mungu ametupa,” alisema.

Zambia ilipata uhuru wake Oktoba 24, 1964 kutoka kwa Waingereza na aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Kenneth Kaunda aliapishwa kuwa Rais wa kwanza wa Taifa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *