Mitihani ya kujipima darasa la 4 kuanza leo

  • Kidato cha pili kuanza Oktoba 30, 2023

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

WATAHINIWA 1,692,802 wanatarajia kuanza mitihani ya kujipima kitaifa ya darasa la nne (SFNA) 2023 inayoanza leo katika shule za msingi 19,284.

Mitihani hiyo itafanyika leo na kesho ikihusisha wavulana  828,591 sawa na asilimia 48.95 na wasichana 864,211 sawa na asilimia 51.05.

Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani Taifa (NECTA), Dkt. Said Mohamed, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mitihani hiyo na kidato cha pili.

Alisema baraza hilo halitasita kufuta matokeo ya mwanafunzi ambaye atajihusisha na udanganyifu kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

Alieleza kuwa, wanafunzi 1,605,379 wa darasa la nne sawa na asilimia 94.84 watafanya upimaji kwa lugha ya Kiswahili na wanafunzi 87,423 sawa na asilimia 5.16 watafanya kwa lugha ya kingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika ufundishaji.

“Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wapo 6,402, kati yao 1,074 wenye uoni hafifu, 93 wasioona, 1, 240 wenye ulemavu wa kusikia, 2,209 wenye mtindio wa akili, 2,786 wenye ulemavu wa viungo vya mwili,” alisema.

Akizungunzia mtihani ya kidato cha pili, inayotarajiwa kuanza Oktoba 30,2023 hadi Novemba 9, 2023 kwa shule za Sekondari 5,546, Dkt. Mohamed alisema wanafunzi 759,573 wamesajiliwa kufanya upimaji huo mwaka huu.

Kati ya wanafunzi hao, wavulana 353,807 sawa na asilimia 46.58, wasichana 405,766 sawa na asilimia 53.42.

Wanafunzi wenye mahitaji maalum wapo 1,382, kati yao, 683 ni wenye uoni hafifu, 82 wasioona, 290 wenye ulemavu wa kusikia, 309 wenye ulemavu wa viungo vya mwili na 18 wenye ulemavu wa akili.

Alifafanua kuwa, hadi sasa maandalizi ya mitihani ya upimaji kwa watahiniwa wote yamekamilika ikiwemo kusambazwa karatasi za upimaji, nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji huo katika Halmashauru/Manispaa zote nchini.

Alitoa wito kwa wasimamizi walioteuliwa kusimamia upimaji huo, kufanya kazi yao kwa umakini, uadilifu wa hali ya juu.

“Wasimamizi wahakikishe wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi, kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake,” alisema.

Alieleza kuwa, wasimamizi wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wanafanya upimaji kwa muda uliopangwa  katika hali ya utulivu.

Alisema wamiliki wa shule hawapaswi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha upimaji huo.

Baraza hilo halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote ambaye atahusika kusababisha udanganyifu kwa mujibu wa sheria za nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *