Ziara ya Samia nchini Zambia inaakisi uwekezaji Bandari Dar

Na Daniel Mbega,

Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yuko nchini Zambia kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, lakini leo hii atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa taifa hilo.

Zambia ilipata uhuru wake siku ya Jumamosi, Oktoba 24, 1964 kutoka kwa Waingereza, harakati ambazo ziliongozwa na Dkt. Kenneth David Kaunda, mwalimu aliyejiingiza kwenye harakati za siasa.

Rais Hakainde Hichilema ndiye aliyempokea Rais Samia jana, kuadhimisha kumbukumbu muhimu ya kujitawala kwa taifa hilo ambalo enzi za ukoloni wa Mwingereza lilijulikana kama Northern Rhodesia (Rhodesia ya Kaskazini). Jina la Zambia lilipatikana baada ya uhuru kwa kufuata Mto Zambezi, mto mkubwa unaomwaga maji yake katika Bahari ya Hindi.

Hichilema, aliyegombea urais na kushindwa mara tano (2006, 2008, 2011, 2015, na 2016) kabla ya kushinda alipogombea mara ya sita mwaka 2021, yuko katika kipindi cha kujenga uchumi wa taifa hilo ambalo, kama mataifa mengine, linakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za ukame na mfumuko wa bei unaotokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Ziara hii ya Rais Samia nchini Zambia ina umuhimu mkubwa kiuchumi kwa mataifa yote mawili, ndiyo maana pamoja na mambo mengine, inalenga kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu.

Tunaambiwa kwamba, katika ziara hiyo Rais Samia na mwenyeji wake watajadili namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la Tazama, Reli ya Tazara na Barabara ya TanZam.

Aidha, Rais Samia atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia, lakini pia amepewa heshima ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia Oktoba 25, 2023 na anakuwa kiongozi mashuhuri wa nne kuhutubia Bunge hilo.

Mwenendo wa ukuaji wa biashara baina ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022, yaani baada ya miaka sita.

Hii ni ziara ya kwanza ya Kitaifa ya Rais Samia kufanya nchini Zambia tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022.

Jambo jingine muhimu katika ziara hiyo ni kwamba, nchi hizo mbili zimelenga kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.

Hili la uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam linabeba dhima kubwa ya ziara ya Rais Samia nchini Zambia, ambayo imekuja takriban siku moja tu baada ya kusainiwa kwa mikataba mitatu Oktoba 22, 2023 baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai kwa ajili ya uendeshaji wa sehemu ya Bandari hiyo.

Zambia ni miongoni mwa mataifa matano yasiyo na bandari (landlocked countries) ambayo yanaitegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo yao. Nchi nyingine ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Malawi na Rwanda.

Hata hivyo, pamoja na Serikali kuchukua hatua mbalimbali za kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam, ufanisi wake katika utoaji wa huduma bado hauridhishi na haujafikia viwango vya kimataifa.

Hali hiyo ndiyo iliilazimu Serikali, kwa kuzingatia Mpango wa Maboresho ya Bandari wa mwaka 2009 kama ulivyorejewa mwaka 2022, kutafuta mwekezaji na kukasimisha shughuli za uendeshaji huku yenyewe ikibaki kuwa msimamizi mkuu.

Siyo siri kwamba, hali ya sasa ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda kama Mombasa nchini Kenya, Beira nchini Msumbiji na Durban nchini Afrika Kusini.

Ufanisi huo mdogo katika Bandari unaongeza gharama ambapo meli zinasubiri nangani muda mrefu na kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Plasduce Mbossa, gharama ya meli kusubiri nangani kwa siku moja ni takribani Dola za Kimarekani 25,000 ambayo ni sawa na Shs. milioni 58 kwa siku, maana yake kwa meli 30 zilizopo sasa nangani maana yake ni kwamba kwa mwezi mmoja TPA inalipa Dola milioni 22.5 (takriban shilingi bilioni 56.25) kutokana na meli kusubiri nangani.

Taarifa zilizopo zinasema, kwa sasa meli zinasubiri nangani hadi siku 10 bila kuhudumiwa, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji na kupunguza hata mapato kidogo yanayopatikana. Ongezeko la gharama hizo mwisho wake linakuwa mzigo kwa mwananchi wa kawaida, kwa sababu bidhaa zinaongezwa bei na wafanyabiashara ili kufidia gharama za kusubiria nangani.

Uwepo wa DP World kwenye Bandari ya Dar es Salaam unaweza kupunguza gharama hizo, kwani meli zinaweza kutumia muda wa siku 1.25.

Ufanisi huu mdogo, na changamoto ya kupanda kwa gharama za kusubiria nangani, siyo tu umefanya meli kubwa zisitie nanga kwenye Bandari ya Dar es Salaam, bali pia umewakimbiza wafanyabiashara kutoka nchi nyingine.

Wafanyabiashara wa kutoka Zambia ni miongoni mwa walioikimbia Bandari ya Dar es Salaam na kugeukia Bandari ya Lobito nchini Angola ili kukwepa gharama kubwa.

Lakini kutokana na mikataba ambayo Serikali imeingia na DP World, ufanisi kwenye Bandari ya Dar es Salaam utakuwa mkubwa na wa viwango vya kimataifa.

Hapa ndipo tunapoona kwamba ziara ya Rais Samia huko Zambia inakwenda sambamba na uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam, kwani ni muda muafaka wa kuwaeleza wafanyabiashara wa Zambia kwamba, mambo yamenoga sasa ‘warejee nyumbani’.

DP World itanunua mitambo ya kisasa ya kutosha ya kuhudumia shehena ambayo teknolojia yake inabadilika mara kwa mara.

Hili litapata nguvu katika Kongamano la Biashara ambalo Rais Samia atakuwa mgeni rasmi.

Utatuzi wa changamoto

Ziara ya Rais Samia inakuja takriban wiki mbili tangu Tanzania na Zambia zilipokubaliana kutatua changamoto 8 kati ya 24 za kibiashara na 16 zilizobaki zikawekewa utaratibu wa kuzitatua ifikapo Desemba 31, 2023 ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Zambia, ikiwemo kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma.

Oktoba 9, 2023 Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Tanzania, Dkt. Hashil Abdallah, alikutana na ‘pacha wake’ Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zambia, Bi. Lillian Bwalya, katika Mkutano wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara kati ya Tanzania na Zambia, kikao kilichofanyika katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani-Tunduma, Songwe.

Nchi hizo mbili zilikubaliana kuwa, bidhaa zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine kupitia Zambia zikiwa na vibali vyote vinavyohitajika ziruhusiwe kupita nchini humo kwenda nchi husika bila kizuizi kulingana na Makubaliano ya Kibiashara chini ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Vilevile, taasisi zote za umma zinazohusika na utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara wa huduma ya usafirishaji baina ya nchi hizo kuhakikisha hawawakwamishi bila sababu za msingi bali kuwasaidia kutatua changamoto zao hususan upatikanaji wa vibali kulingana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika makubaliano ya kibiashara chini ya WTO na SADC.

Kwa maana nyingine, ili kufikia malengo hayo, ni vyema wafanyabiashara ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanapata vibali vyote vinavyohusika kabla ya kuanza safari ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hizo bila vikwazo na kuzifikisha katika nchi husika kwa wakati.

Katika makubaliano hayo, Serikali ya Tanzania ilikubali kufanya mapitio na marekebisho ya Tozo ya Maendeleo ya Reli kama inavyotekelezwa katika Itifaki ya Biashara ya SADC na kuharakisha mchakato wa urazinishaji wa kanuni za usafirishaji ili ziendane na kanuni za usafirishaji zinazotekelezwa katika Eneo Huru la Biashara la Utatu (Tripatite Transport Regulations).

Kwa upande wake, Bi. Bwalya alisema, Zambia imekubali kutatua changamoto hizo ili kurahisisha na kukuza biashara za mpakani baina ya nchi hizo.

Katika makubaliano hayo, Zambia ilikubali kuboresha changamoto za miundombinu ikiwemo upanuzi wa barabara na kutekeleza mfumo wa upatitanaji wa vibali kabla ya kufika mpakani ili kuboresha mtiririko wa magari mpakani na kuondoa msongamano wa magari uliopo mpakani Tunduma.

Aidha, Zambia ilikubali kutumia mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo kwa njia ya elektroniki unaotekelezwa nchini Tanzania, au kuharakisha mchakato wa ununuzi wa mfumo unaopendekezwa kutumiwa na Mamlaka ya Mapato ya Zambia (ZRA).

Vilevile, Zambia ilikubali kuharakisha urazinishaji wa ada na tozo za barabara kwa Dola za Marekani 10 kwa kilomita 100 unaotekelezwa katika SADC.

Zambia pia ilikubali kuangalia uwezekano wa kutumia mfumo wa kisasa wa ufuatiliaji wa magari barabarani ili kuondoa na kupunguza vizuizi vya ukaguzi barabarani.

Zambia ilikubali kutumia Ofisi jijini Dar es Salaam inayotolewa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya maofisa wa uondoshaji wa mizigo ya Zambia kuanzia Desemba 31, 2023 ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kuondoa msongamano wa magari mpakani.

Kwa ujumla, changamoto zilizoondolewa zitaongeza ufanisi wa utoaji huduma na kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Lakini si hayo tu, Tanzania na Zambia zina maeneo mengi ya ushirikiano, ambayo yanazidi kuimarishwa kwa ziara hii ya Rais Samia.

Maeneo hayo ya ushirikiano ni pamoja na Siasa, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje, Uhamiaji, Fedha na Uchumi, Sheria, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Miundombinu, Uchukuzi na Usafirishaji, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo, Uvuvi, Mazingira na Maliaasili, Afya, Elimu, Vijana na Michezo na Jinsia.

Mnamo Jumanne, Agosti 2, 2022, katika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia na Rais Hichilema walikubaliana maeneo saba ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha uhusiano wa ujirani mwema kama ulivyohimizwa na waasisi wa mataifa hayo mawili. Hii ni wakati Rais Hichilema alipofanya ziara ya siku mbili nchini Tanzania.

Wakizitambua hekima za waasisi wa mataifa hayo mawali, Mwalimu Julius Nyerere rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa na mwenzie Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda, marais hao wa sasa wanaona kwamba kuna wakati uhusiano wa kidugu wa pande hizo mbili ulipitia katika nyakati za milima na mabonde, lakini wakati umefika wa kuzienzi fikra za waasisi wake.

Rais Samia aligusia kiini cha makubaliano hayo ikiwamo kurejesha upya uhusiano wa kidugu hasa kwa kutambua kwamba raia wa pande zote mbili wamekuwa wakiingiliana karibu kila uchao kupitia eneo la Tunduma kwa upande wa Tanzania na lile la Nakonde upande wa Zambia.

Wakaafikiana kupanua ushirikiano kwenye sekta ya usalama na mkazo ukiwekwa zaidi katika eneo la kukabiliana na vitendo vya kigaidi.

Uimarishaji wa sekta ya miundombinu kupitia reli ya Tazara ni eneo lingine ambalo wakuu hao wa nchi wanaona linapaswa kupewa msukumo na Rais Samia akasema jambo linalopaswa kutupiwa macho ni kuona reli hiyo inaboreshwa kufikia viwango vya kisasa.

Kwa upande wake, Rais Hichilema alisema Tanzania na Zambia ni mataifa ndugu yanayopaswa kuendelea kunufaishana katika sekta za kijamii na biashara.

Akasema hakuna haja kwa pande hizo kuendelea kutoleana macho bali kinachopaswa ni kuendelea kuilinda misingi iiyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili na hilo litafanikiwa kwa kuendelea kufungua milango ya fursa kwa wananchi wa pande zote.

Tanzania na Zambia mataifa ambayo pia yamepitiwa na Ziwa Tanganyika wakati fulani yalijikuta yakiingia katika hali ya sintofahamu baada ya madereva wa malori wa Tanzania kupigwa marufuku kuingia nchini Zambia, mzozo ambao hata hivyo baadaye ulitafutiwa ufumbuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *