Haya ndiyo mambo yaliyozingatiwa mkataba wa uwekezaji Bandari Dar

Na Daniel Mbega,

Dar es Salaam

HATIMAYE Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jumapili, Oktoba 22, 2023 ilitiliana saini mikataba mitatu na Mamlaka ya Dubai kupitia kampuni ya DP World kwa ajili ya ukodishaji na uendeshaji wa maeneo kadhaa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mchakato huo umechukua muda mrefu huku kukiwa na vipingamizi kadha wa kadha, na ndiyo maana wakati wa utiaji saini, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kwamba, haikuwa kazi rahisi kufikia hatua waliyoifikia.

Mkataba huo wa miaka 30 utaongeza mapato ya Serikali kutoka Shs. trilioni 7.8 zinazokusanywa eneo la bandari pekee mwaka 2021-2022 hadi Shs. trilioni 26.7 mwaka 2032.

Haya yatakuwa mafanikio makubwa kiuchumi hasa baadaya kuongezeka kwa ufanisi kwenye bandari hiyo inayotegemewa na mataifa mengine kama Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi, Rwanda na Zambia.

Kama alivyosema Rais Samia, mpaka kufikia hatua ya kusaini mikataba hiyo, Serikali imezingatia maoni ya wananchi kwa kuwa Bandari ni maliasili na hata uwekezaji ni kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa kwa kupitia mmoja mmoja na makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na sheria na taratibu zote za nchi.

“Niwape uhakika Watanzania, maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa, hakuna atakayepoteza kazi bandarini kutakua na kufuata mfumo ili viwango vikae sawa viendane na dunia, kukuza ufanisi na baishara na mapato ya nchi yetu,” alisema.

Siyo siri, bandari ndiyo kiunganishi muhimu cha biashara na chanzo kikubwa cha mapato, hivyo hata maboresho yatakayofanywa kupitia uwekezaji huo yatakuza biashara za ndani na nje na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani itakayoongeza maapto ya serikali na kukuiza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Tangu Bunge la Jamhuri ya Muungano liliporidhia Azimio la Makubaliano ya Awali ya Ushirikiano na Uendeshaji wa Bandari Juni 10, 2023, baadhi ya wananchi wakichagizwa na wanaharakati walikuwa wakipinga kwa kudhani Bandari zetu zinauzwa.

Lakini hali imekuwa tofauti, kwa sababu Serikali ilikwishasema kwamba, haiwezi kuuza Bandari, bali ilikuwa inatafuta namna ya kukuza uwezo na ufanisi wa bandari hiyo iweze kusafirisha mizigo mingi zaidi ili kukamilisha mnyororo wa biashara na nchi jirani.

Katika kuondoa mashaka ya baadhi ya watu, mikataba mitatu iliyosainiwa, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, imezingatia mambo kadhaa muhimu ambayo ni:

Mosi, Mikataba inahusisha baadhi ya magati ya Bandari ya Dar es Salaam (Gati namba 4 hadi 7) na siyo maeneo yote ya Bandari ya Dar es Salaam na mikataba hiyo haihusishi bandari nyingine za mwambao na maziwa.

Naam. Tofauti na ilivyokuwa inaelezwa na wanaharakati awali kwamba DP World walikuwa wakikabidhiwa bandari zote za Tanzania, mikataba hii imeainisha kwamba kampuni hiyo imekodishwa kuendesha magati manne tu kwenye Bandari ya Dar es Salaam, maeneo ambayo huenda ndiyo yenye changamoto kubwa ya msongamano wa mizigo kwa sasa.

Pili, Mkataba huo una ukomo wa miaka 30 na utakuwa ukirejewa kila baada ya miaka 5 ikiwa ni pamoja na kurejea mpango wa uwekezaji.

Hii imewaumbua waliokuwa wakisambaza uongo kwamba, DP World wamekabidhiwa Bandari kwa miaka 100, jambo ambalo siyo kweli.

Tatu, Kutakuwa na kampuni ya uendeshaji ambayo TPA itamiliki hisa.

Hii ni njia nzuri ya uwekezaji kwa maana ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi (Public Private Partnership – PPP), ambayo hata ‘binamu’ zetu Wakenya wametangaza kuitumia watakapompata mwekezaji kwenye bandari zao za Mombasa na Lamu.

Nne, Kuwekwa kwa viwango vya utendaji (key performance indicators) ambavyo mwekezaji anapaswa kuvifikia.

Kipengele hiki ni cha muhimu sana, kwa sababu kama malengo yetu ni kuongeza ufanisi, na kama wawekezaji wenyewe wamesema mapato yatafikia Shs. trilioni 26.7 kwa mwaka ifikapo mwaka 2032, basi tunataka tuone matokeo.

Hii pia itawafanya wawekezaji hawa kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha wanayafikia malengo na kujitofautisha na waliotangulia, lakini pia ufanisi wao utaifanya Serikali iendelee kuwaamini na kuendelea na mkataba.

Tano, Watumishi wa sasa wa TPA wamepewa nafasi ya kuchagua kubaki TPA au kuhamia kwa mwekezaji.

Maslahi ya watumishi wa sasa wa TPA yamezingatiwa na watakuwa na nafasi ya kuchagua kubaki TPA au kuhamia kwenye kampuni ya ubia na DP World, ambayo itahitaji rasilimali watu kutoka hapa nchini, kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa.

Sita, Jukumu la ulinzi na usalama katika eneo lote la Bandari na yaliyokodishwa kwa Kampuni ya DP World litaendelea kubaki Serikalini. Hii nayo imeondoa mashaka ya baadhi ya watu waliokuwa wanahisi kwamba mwekezaji ndiye atashughulikia, hali ambayo ingekuwa na walakini kiusalama.

Saba, Mwekezaji atalipa kodi na tozo zote za Serikali kwa kuzingaia Sheria za Tanzania.

Nane, Sheria za Tanzania zitatumika katika utekelezaji wa Mikataba hiyo.

Awali baadhi ya wanaharakati walikuwa wanavumisha kwamba, ukodishaji wa Bandari hiyo haufai kwa sababu Sheria zitakazotumika ni za kimataifa, kwa hiyo itakuwa vigumu kumbana mwekezaji hata kama atashindwa kutekeleza vipengele vya mkataba. Lakini kwa taarifa hizi maana yake Bandari yetu iko salama na Tanzania iko salama.

Tisa, Kutakuwa na fursa za Watanzania kushiriki katika uwekezaji huu kupitia vifungu vya Sheria vinavyolinda maudhui ya ndani ya nchi (local contents).

Haya ni mazingatio ya Sheria za Kimataifa za uwekezaji, kwamba mwekezaji anaweza kuja na watalaamu wake, lakini nafasi nyingi za chini zitashikwa na wazawa.

Haijuzu eti hata mtu wa kuendesha Crane atoke nje wakati tunao Watanzania wengi wenye ujuzi wa kuendesha mitambo hiyo tena wazoefu.

Kumi, Haki ya Serikali kujiondoa katika Mikataba hiyo imezingatiwa.

Hii maana yake ni kwamba, ikiwa Serikali itaona hakuna haja ya kuendelea na mkataba huo, kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, inaweza kujiondoa.

Kwa kifupi, uwekezaji huu una manufaa makubwa kwa Taifa kuliko watu walivyokuwa wanapotosha – kwa maslahi yao au ya wale walio nyuma yao.

Baniani mbaya, kiatu chake ni dawa! Tumkribishe DP World atufungulie fursa kwenye Bandari yetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *