Na Mwandishi Wetu
VIJANA ni nguvu kazi ya taifa na ili izae matunda ni lazima iwe yenye uwezo, utimamu wa akili na afya kwani ndiyo vigezo muhimu vinavyomuwezesha mtu yeyote kufikia adhma ya uzalishaji mali ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Mbali na umuhimu wake bado imekuwa changamoto kubwa kwa vijana juu ya ufahamu wa mambo mbalimbali ikiwemo katika masuala ujasiriamali, kilimo, siasa pamoja na kuhakikisha wanajipambania katika kujiajiri.
Asilimia kubwa ya vijana kwa sasa utumiwa na vyama mbalimbali vya siasa ambapo uishia kuwanufaisha wengine na wao kuendelea kubakia maskini.
Vijana wanapaswa kujitambua kuona wana fursa mbalimbali ambazo wanapaswa kuzitambua na kuzitumia badala ya kubweteka na kukaa bila shughuli za kufanya huku wengine wakiishia kutumika na vyama vya siasa na makundi ya kiharakati, hali inayochangia wengi wao kujiingiza katika makundi yasiyofaa.
Shughuli za maendeleo ya vijana zinahusiana kwa kiasi kikubwa na masuala mtambuka yanayohitaji ushirikishwaji katika sekta mbalimbali ziwe za kisiasa, kijamii na hata kitamaduni.
Kundi hilo la vijana ni miongoni mwa watu ambao wanatakiwa kusaidiwa na kuzidi kusimamiwa kwa kuhakikihsa wanakuw ana muamko wa kujiajili wenyewe na kuajiri vijana wenzao na sio kutegemeza siasa pindi wanapomaliza shule.
Taasisi mbalimbali zimekuwa zikiendesha mafunzo kwa vijana ili kuweza kuwakomboa na kuhakikisha wanafika katika sehemu ambazo wanaweza kuja kujisimamia wao wenyewe na familia zao.
Lenin Kazoba, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini (TYC) anasema vijana wanapaswa kushirikishwa katika miradi mbalimbali ili kuweza kuwaletea afua katika maisha yao.
Anasema taasisi yao imekuwa ikifanya kazi na vijana kwa miaka mingi kupitia miradi mbalimbali lengo ikiwa kuwasaidia kujitambua, kujiamini na kuhakikisha wanaweza kufikia ndoto zao licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika jamii.
Lenin anasema TYC kwa sasa inatekeleza Mradi wa Kijana Nahodha mradi ambao unachukua miaka minne ulianza mwaka 2022 hadi 2026 ukilenga kuwafikia vijana 45,000 wa Zanzibar na Tanzania Bara kwa maeneo ya Ilala, Temeke na Kigamboni.
Anasema mradi huo unawalenga zaidi vijana walio nje ya mfumo wa shule ambapo mradi umejikita maeneo mahususi matatu ikiwemo kuongeza fursa za kielimu stadi za maisha na maarifa ya ujasiriamali kwa vijana na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli zinazostawisha afya ya mwili, akili na kuanzisha na kuimarisha mitandao inayosaidia maendeleo ya vijana na ushirikishwaji jamii.
“Mradi huu unalenga kuwafikia vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 25 ambao wako mashuleni na wale walioko mtaani ni mradi unaotekelezwa na mashirika matatu T Mark Tanzania, TYC, Care International, WRAP ambapo wanafadhiliwa na shirika la Kimarekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
“Mradi huu unazingatiwa kilichowekezwa katika ajira, elimu, kilimo, utawala na afya na kukielekeza kwenye mradi unaowalenga vijana ili kuwajengea uwezo katika miaka 15 hadi 25.
“Mradi huu ambao ni mahsusi kwa vijana utahakikisha kuwa wanufaika wanakwamuliwa kiuchumi lakini pia wanawezeshwa kuwa viongozi katika jamii zao kwa kuwaunganisha na maeneo ambayo maamuzi nyeti ya kimaendeleo yanafanyika,” anasema.
Anasema miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na kuweka mikakati itakayowapa vijana uwezo wa kuwa wadau muhimu na waleta chachu ya mabadiliko katika ngazi za vijiji, mikoa na taifa.
Lenin anasema, wanufaikaji wa mradi huo wa kuwainua vijana jutaweza kuwajengea uwezo na kuwapa maarifa ya kuweza kupata huduma za kiafya ikiwemo afya ya uzazi, afya ya akili, msaada wa kisaikojia, msaada wa chakula, matibabu na matumizi kwa watu wenye Ukimwi kuzingatia mienendo yao mizuri ya kiafya.
Kwa upande wake mwalimu wa masuala ya demokrasia na diplomasia na haki za vijana, Deus Kibamba, anasema kundi la vijana ni miongoni mwa kundi ambalo linamuamko mdogo katika masuala ya siasa.
Anasema vijana wana uwezo wa kujipanga katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hivyo vijana lazima wawezo manahodha wa ya michakato ya uchaguzi kwani mradi wa kijana nahodha unahitaji vijana kushika hatamu mbalimbali.
“Hivi sasa kumekuwa na shida michakato mingi ya uchaguzi haijulikani, hali ambayo vijana wanahisikia tu nakufanya vijana wengi kujitenga na masuala ya siasa kutokana na kutojua yanayowahusu,” anasema.
Anasema, ni vema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhakikisha inatengeneza mazingira rafiki kwa vijana na kuweka mfumo wa kidigitali wa kujiandikisha wenyewe kama wapiga kura wapya.
“Ni lazima kuwepo kwa mazingira rafiki kwa vijana kwani tunaona katika uchaguzi uliopita wa Mbunge wa Jimbo la Mbeya, watu waliopiga kura ni nusu ya waliojiandikisha, vijana wanahangaika wanatafuta maisha, sasa uje kumwambia akajipange kwenye msululu wa watu wengi ili wapige kura, huo ni uongo kwani hawatokei wala hawajiandikishi,” anasema.
Anasema, kuna haja ya kurahisishwa kwa mifumo hiyo kwani mfumo unaotumika sasa ni wa kizamani na vijana wengi wanajikuta wakishindwa kukaa foleni na kujiandikisha kwa kuwa wana mambo mengi.
Kibamba anasema, mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na vijana hao katika mjadala yanamuelekea wa kuhamsisha vijana wengi kuhakikisha wanashiriki katika michakato ya uchaguzi na kuja kushiriki kupiga kura.
Mwalimu Kibamba anasema endapo NEC itafanya maboresho mbalimbali katika mapendekezo hayo ya vijana ni wazi itarahisisha ushiriki wa watu wengi hususani vijana ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa muamko wa ujiandikishaji na hata kupiga kura.
Akitaja miongoni mwa mapendekezo waliyotoa vijana katika mdahalo uliowakutanisha vijana mbalimbali kutoka wilaya ya Ilala, Temeke na Kigamboni ni pamoja kuna haja ya kurahisishwa kwa mifumo hiyo kwani mfumo unaotumika sasa ni wa kizamani na vijana wengi wanajikuta wakishindwa kukaa foleni na kujiandikisha kwa kuwa wana mambo mengi.
Anasema kama mfumo utabadirika na kuwa wa kidigitali utamuwezesha kijana kujiandikisha mwenyewe kwa kutumia simu yake, badala ya kulazimika kwenda kupanga foleni ya kusubiri kuandikishwa.
“Vijana wana mambo mengi kwa hiyo suala la kupanga foleni kusubiri aandikishwe ni jambo gumu kwake, tutengeneze mfumo wa kidigitali,ambapo itakuwa ni APP itakayowafanya kujiandikisha kisha NEC sasa itakuwa na kazi ya kufatilia maelezo yaliyojazo kama sahihi,” anasema.
Anasema, NEC inapaswa kuandaa programu tumizi itakayowezesha mfumo huo kufanya kazi ingawa wapo ambao hawataweza kujiandikisha wenyewe hivyo amependekeza kuwepo kwa mawakala watakaoshughulikia kuwaandikisha watu.
Naye, Johnson Andrew, mmoja wa washiriki wa mjadala huo, anawashukuru TYC kwa kuwachukua na kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya uchuguzi ambapo kama nchi inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu.