Na Mary Geofrey,
Pemba
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabishara Tanzania (JWT), Khamis Livembe, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kusaini mkataba wa kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam na Kampuni ya DP World, wenye lengo la kunufaisha Taifa na wafanyabishara kwa ujumla.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa gazeti hili jana visiwani Pemba, Livembe alisema suala la bandari kilikuwa kilio cha muda mrefu cha wafanyabishara wengi nchini.
Alisema kutokana na kuwapo kwa kero hiyo ya muda mrefu, ilisababisha kuwapo kwa mabadiliko ya mara kwa mara ya watendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Alisema hali hiyo bado haikuridhisha kwasababu bado wafanyabishara waliendelea kupata shida na hata kuamua kushusha mizigo kwenye bandari za nchi jirani ikiwamo Kenya ili kupunguza ucheleweshaji wa kupakua mizigo, ufanisi mdogo na mizigo kupotea.
“Kwa uwekezaji huu utasaidia sana kuinua biashara zetu, kupunguza biashara za kushusha mizigo na gharama za usafiri kutokana na urahisi wa kushusha mizigo hiyo,” alisema Livembe na kuongeza kuwa,
“Tunampongeza sana Rais Samia kwa uamuzi huu wa busara na uamuzi sahihi hasa kwa kuwa kulikuwawa na kelele nyingi lakini alitulia na kufanya uamuzi huu, ambao leo tumefahamu umuhimu wa kusainiwa kwa mkataba wenye maslahi mapana kwa Taifa letu.”
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakala wa Forodha Zanzibar na Mjumbe wa JWT, Omary Hussein, alisema mkataba ambao Rais Samia ameusaini ni wa kufungua milango ya kibiashara na kiuchumi iliyokuwa imekwama.
Alisema kwa upande wa Zanzibar watanufaika na kusainiwa kwa mkataba huo kwasababu walikuwa wakitumia zaidi bandari ya Mombasa kushusha mizigo yao na kwa maboresho hayo watatumia bandari ya Dar es Salaam.
“Tumpongeze Rais Samia kwa maono yake makubwa yanayofungua uchumi wa Taifa na kurahisisha shughuli za kibiashara nchini kupitia TPA na kurahisisha shughuli za uwekezaji nchini, tunamshukuru na kumpongeza sana,” alisema Omary.
Naye Katibu wa JWT mkoa wa Tanga, Ismail Masoud, amesema kusainiwa kwa mkataba huo, unafuta mzigo wa tozo za kusubiri meli kushusha mizigo bandarini hapo.
Alisema TPA itakusanya trilioni 26 kwa mwaka baada ya kusaini mkataba huu ni jambo kubwa lililokuwa ndoto kwa Watanzania kufanya hivyo lakini kwa mkataba huu uchumi wa Taifa utastawi.
“Tunakushukuru sana Rais Samia kwa kazi kubwa uliyofanya ya kukumbukwa vizazi vyote ya kukomboa uchumi wa Taifa letu na kutuvusha sisi wafanyabishara ambao tulikuwa tunabebeshwa mzigo wa kodi zisizo na tija,” alisema.