- Rais Samia asema mikataba imezingatia maslahi ya Watanzania
- Asema, maoni yaliyotolewa na wananchi yamezingatiwa
- Ni kwa miaka 30, mapato kufikia Shs. 26.7 bilioni kwa mwaka
HATIMAYE kimeeleweka. Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Serikali ya Tanzania na Dubai kusaini mikataba mitatu ya uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Katika tukio hilo lililofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, jana Jumapili, Oktoba 22, 2023, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema mikataba hiyo ya uwekezaji na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam imezingatia maslahi ya Watanzania kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa.
Pia mkataba huo wa miaka 30, utaongeza mapato ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kutoka Shs. trilioni 7.8 zinazokusanywa eneo la bandari pekee mwaka 2021-2022 hadi Shs. trilioni 26.7 mwaka 2032.
Hayo yalibainishwa wakati wa uwekaji saini wa mikataba mitatu ya uendelezaji wa bandari kati ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema Watanzania wanajua kuwa bandarini kuna changamoto ambazo hutofautiana namna ya kuzitatua ambapo wapo wanaoamini bila mbia zinaweza kutatuliwa licha ya kuwa mbali kiuhalisia.
“Na njia hiyo itachukua muda mrefu sana kufika wakati dunia inakwenda mbio sisi tungekuwa bado, isitoshe tulishajaribu lakini hatukufanikiwa.
“Mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa kwa kupitia mmoja mmoja na makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na sheria na taratibu zote za nchi.
“Niwape uhakika watanzania maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa, hakuna atakayepoteza kazi bandarini kutakua na kufuata mfumo ili viwango vikae sawa viendane na dunia, kukzua ufanisi na baishara na mapato ya nchi yetu,” alisema.
Alisema bandari ndiyo kiunganishi muhimu cha biashara na kuhudumia shehena kubwa ya mizigo kutoka nchi jirani na mataifa ya mbali.
Rais Samia alisema maboresho yatakayofanywa kupitia uwekezaji huo yatakuza biashara za ndani na nje na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani itakayoongeza maapto ya serikali na kukuiza uchumi wa taifa kwa ujumla.
Alisema kwaupande mwingine Serikali inatekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2025 iliyoagiza kushirikisha sekta binafsi katika kuchagiza maendeleo na shughuli za uchumi.
“Hafla ya leo ni mwendeleo ya kutekeleza mikakati ya CCM ambapo kila tunapoendelea mbele tutazidi kuona ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi katika uwekezaji na ufanyaji wa biashara,” alisema.
Alisema kuwa mikataba hiyo imezaliwa kutoka kwenye makubaliano ya awali na ilivyoridhiwa na Bunge na kulishukuru kwa ushauri makini na kuridhia azimio la makubaliano ya awali ya ushirikiano na uendeshaji wa bandari Juni 10, 2023.
“Nalishukuru Baraza la Mawazi kwa kubariki mikataba mitatu iliyosainiwa kwa mazingatio ya kifungu cha pili cha sheria ya ubia namba 6 ya mwaka 2023 na kifungu cha pili cha sheria ya ununuzi wa umma namba 5 ya mwaka 2003,” alisema.
Aliishukuru Serikali ya Falme za Kiarabu kwa kuridhia matakwa ya Tanzania kama yaliyobainishwa kwenye mikata hiyo yaliyozingatia matamanio ya Wananchi wa Tanzania na maslahi mapana ya nchi.
“Bandari ya Dar es Salaam ni malisili, ni jaha, hidaya adhimu tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
“Ni lango la biashara na nchi zinazotuzunguka, bandari hii kuungwa na kuwekwa kwetu Tanzania inatupa wajibu wa kuhudumia nchi jirani wanaoitegemea,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano ya umoja wa mataifa, nchi zenye mlango banari zinawajibu wa kuhudumia na kuhakikisha ustawi wan chi zisizo na milango bahari.
Alifafanua kuwa katika kutekeleza wajibu huo, Serikali imewekeza kwenye kuunganisha nchi na nchi zingine zinazotuzunguka kupitia barabara, vituo vya utoaji huduma mipakani, reli, usafiri wa maji na usafiri wa angani.
“Ni lazima kukuza uwezo na ufanisi wa bandari yetu iweze kusafirisha mizigo mingi zaidi ili kukamilisha mnyororo wa biashara na nchi jirani,” alisema.
Alisema, kwa kuzingatia hilo, ilifaa kupata mwekezaji wa kushirikiano nae si tu kuongeza upatikanaji wa mizigo au mizigo kuingia na kutoka nchini, lakini kuongeza ufanisi utakaofanya gharama kuwa shindani na bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, alisema uboreshaji wa sehemu ya bandari itapunguza gharama ya kusubiri meli nangani ya sh milioni 58 kwa siku.
Alisema dhamira ya uboreshaji wa bandari inaongeza uwezo wa utoaji huduma kwa ufanisi, kupunguza gharama, kuinua uchumi, ukuaji wa uwekezaji, biashara, kuongeza ajira, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi pamoja na kutumia fursa ya kijiografia ya nchi katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Aliongeza kuwa bandari za hapa nchini zinaendeshwa kwa hali ya ushindani kama zilivyo bandari zingine duniani yanayochagizwa na ukuaji wa mabadiliko ya sekta ya usafirishaji majini, teknolojia na ukuaji wa uchumi.
Mbossa alisema TPA imekasimishwa jukumu la umiliki, uendeshaji, uendelezaji na usimamizi wa bandari nchini inajukumu la kutoa huduma sambamba na kasi ya mabadiliko hayo.
“Katika kuendana na mabadiliko hayo, moja ya miakakti ambayo ilibainishwa katika mpango kabambe wa uendelezaji wa bandari Tanzania wa mwaka 2009 ambao ulifanyiwa marejeo mwaka 2022 ulitoa mapendekezo kwamba serikali itafute namna ambayo inaweza kufikia azma ya TPA kuwa mmiliki na mwendelezaji wa bandari nchini na kukasimisha shughuli za uendeshaji bandari kwa sekta binafsi ili kuishirikisha na kuongeza ufanisi wa bandari za Tanzania,” alisema.
Alisema pamoja na hatua mbalimbali za maboresho ya bandari kuchukuliwa bado ufanisi wa utoaji huduma za bandari haujafikiwa viwango vya kimataifa.
Mbossa aliongeza kuwa hali ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda ambapo meli nyingi husubiri kuhudumiwa.
“Hadi leo tuna meli 29 ambazo zimetia nanga zikisubiri kuingia bandarini lakini katika gati 12 ambazo tunazo katika Bandari ya Dar es Salaam tuna meli 12 zikihudumiwa,” alisema.
Alisema wastani wa meli kusubiri nangani ni siku 5 hadi 10 ikilinganishwa na bandari za nchi nyingine kama Kenya ambao huwa wastani siku 1.25.
Aliongeza ufanisi mdogo wa bandari ya Dar es Salaam kumetokana na kukosekana kwa mifumo ya kisasa ya Tehama inayoweza kusomana, kutokuwepo kwa maeneo ya kutosha ndani na nje bandari kwa ajili ya kuhifadhi shehena za mizigo,uchache wa magati.
Pia kukosekana kwa mitambo ya kisasa ya kuhudumia shehena ambayo teknolojia yake hubadilika mara kwa mara jambo linalosababisha kuwa na gharama kubwa za utumiaji wa bandari hiyo.
Aliongeza kuwa athari ya kutokuwa na ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam ni meli kusubiri muda mrefu nangani kunakosababisha kuongezeka gharama ya kutumia bandari hiyo ambayo ni sawa na sh milioni 58 kwa siku.
“Maana yake kwa meli 30 tulizonazo kwa mwezi tunalipa dola milioni 22.5 kuitokana na meli kusubiri nangani ambazo hulipwa na wale wasafirishaji wa mizigo,” alisema.
Alisema muda wa kupakua mzigo kwenye gati ni siku 5 ukilinganisha na siku moja inayokubalika kimataifa kunakotokana na uduni wa vifaa vilivyopo.
Aliongeza kuwa hali hiyo pia husababisha meli kubwa kutoingia katika bandari ya Dar es Salaam kwasababu huduma hutolewa kwa muda mrefu na kusababisha bandari ya Dar es Salaam kulishwa na bandari nyingine.
Alisema katika kutekeleza mkakati wa kuimarisha shughuli za bandari ya Dar es Salaam, serikali imesaini mkataba wa uwekezaji na uendeshaji bandari hiyo ambao ni wa nchi mwenyeji.
Alisema mkataba huo ni wa ukodishajhi wa gati 4 hadi 7 ambapo gati namba 0 hadi 3 zitaendeshwa kati ya TPA na Kampuni ya DP World kwa shughuli za kibiashara na kiserikali.
“Mikataba hii hausishi eneo lote la bandari ya Dar es Salaam wala bandari nyingine za Tanzania,” alisema.
Alisema gati namba 8 hadi 11 mchakato wa kumpata mwendashaji mwingine unaendelea ambaye hatakua DP World.
Alifafanua kuwa katika mikataba hiyo, Serikali itakua inapata ada na tozo kutoka kampuni ya DP World ambazo zitaongeza mapato yake na kupunguza gharama za uendeshaji.
Aliongeza kuwa hapo awali serikali imekuwa ikitumia takribani asilimia 90 ya mapato yote yanayokusanywa katika uendeshaji wa maeneo yaliyokodishwa na kubakiwa na asilimia 10 pekee.
“Kutokana na mikataba hii serikali itaweza kubakia na asilimia 60 ya mapato yote kutokana na gharama yote ya uendeshaji kwenda kwa kampuni ya DP World,” alisema.
Alisema faida hiyo inayotokana na maboresho kutokana na uwekezaji huo, pia itaonekana kwa kiwango cha juu.
Alisema ufanisi huo utaongeza mapato ya TRA kutoka Shs. trilioni 7.8 zinazokusanywa eneo la bandari pekee mwaka 2021-2022 hadi Shs. trilioni 26.7 mwaka 2032.
Alisema mikataba hiyo imezingatia maono ya wananchi yaliyokuwa yakitolewa na wananchi wote kwa ajili ya amslahi mapana ya nchi ikiwemo kuhusisha maeneo ya gati za bandari ya Dar es Salaam na si maeneo yote ya bandari.
Aliongeza kuwa mikataba hiyo haihusisha mandari nginyine za mwambao wa maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyassa.
“Mkataba huu utakua na ukomo wa miaka 30 na utendaji wa DP World unakuwa ukipimwa kila miaka mitano na si miaka 100,” alisema.
Alisema, Serikali kupitia TPA itakuwa na umiliki wa hisa katika kampuni itakayokuwa ikifanya kazi katika bandari hiyo ya Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa mikataba hiyo imeainisha viwango vya utendaji kazi ambavyo mwekezaji atapaswa kuvifikia.
Aliongeza kuwa wafanyakazi waliopo sasa watachagua kubaki TPA au kuhamia kwenye kampuni ya DP World hivyo hakuna atakayepoteza kazi yake baada ya maboresho hayo.
“Mwekezaji atalipa kodi zote za serikali kwa kuzingatia sheria za Tanzania, Sheria za Tanzania ndizo zitakazotumika katika utekelezaji wa mikataba hii na itatoa fursa za watanzania kushiriki kupitia vifungu vya sheria vinavyolinda maudhui ya ndani,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali itakua na haki ya kujiondoa katika mikataba hiyo pale tu itakapoona inabidi kufanya hivyo.
Manufaa ya uwekezaji
Alisema uwekezaji huo utaongeza ufanisi wa huduma zitakazotolewa kwa meli na shehena itakayovutia meli nyingi na shehena kubwa katika bandari ya Dar es Salaam.
Pia itapunguza muda wa kuchakata nyaraka ambapo kampuni ya DP World itatumia mifumo ya kisasa ya Tehama ya bandari itakayofungamanishwa na waadu wote wa bandari.
Alisema mapato ya serikali yataongezeka kufuatia kuongezeka kwa shehena na meli, udhibiti wa udanganyifu kupitia mifumo ya kisasaa mbayo itasimikwa na kampuni hiyo na kuunganishwa na mifumo ya serikali hasa wa TRA.
Aliongeza kuwa TPA itajengewa uzoefu, kutoa ajira mpya kwa Watanzania, kupunguza gharama za kusafirisha mizigo, kupunguza muda wa usafirishaji mizigo kutoka siku 30 hadi siku 15.
Pia itachochea sekta zingine za uchukuzi kama reli, barabara kutokana na kuongezeka kwa shehena kutoka bandarini kwenda sehemu nyingine na kukuza sekta ya Kilimo, madini, viwanda na baishara.
Alitoa rai kwa wananchi kujipanga na kutumia fursa mbalimbali zitakazojitokeza kusafirisha mizigo kutoka bandarini, utengenezaji wa vifungashio vya kuhudumia mizigo na huduma za kuongeza thamani.