Simba yaupiga mwingi ikitoka sare ya 2-2 na Al Ahly

Na Badrudin Yahya

MCHEZO wa ufunguzi wa michuano ya AFL kati ya wenyeji, Simba SC dhidi ya Al Ahly, umemalizika kwa timu hizo kufungana mabao 2-2 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, ilihudhuriwa na wageni mbalimbali duniani akiwemo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, Rais wa CAF, Patrice Motsepe, Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, Mwamuzi Mkongwe wa Italia, Pierluigi Collina na viongozi mbalimbali wa soka na serikali.

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa soka, Al Ahly ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika za majeruhi kuelekea mapumziko lililofungwa na Reda Slim baada ya kutumia pasi Safi ya Mohamed Kahraba.

Hadi mwamuzi wa kati anapuliza filimbi ya mapumziko, Al Ahly walikuwa wakiongoza kwa 1-0 huku pia wakitawala mchezo kwa kiasi kikubwa.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira “Robertinho” alifanya mabadiliko ya kuwaingiza Sadio Kanoute na Jean Baleke waliochukuwa nafasi za Mzamiru Yassin na Luis Miquissone ambao waliongeza kasi ya mashambilizi ya Simba.

Mabadiliko hayo yaliwaamsha Simba na dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili, Simba walichomoa kupitia kwa Kibu Denis ambaye alifunga kwa kichwa akimalizia pasi ya Cloutas Chama.

Wakiwa bado wanajiuliza Al Ahly, walijikuta wakitanguliwa kwa bao la pili dakika ya 56 likifungwa na Kanoute ambaye aliunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Saido Ntibanzonkiza.

Bao hilo lilipokelewa kwa shangwe kutoka kwa mashabiki wa Simba wakiongozwa na Rais wao wa Heshima, Mohamed Dewji ‘MO Dewji’ aliyekaa sambamba na Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro.

Hata hivyo bao hilo, halikudumu kwani Kahraba alisawazisha dakika tatu mbele baada ya walinzi kushindwa kuokoa hatari ambayo ilikuwa inazagaa golini kwao.

Matokeo hayo yanawalizimu Simba kwenda kutafuta ushindi nchini Misri kwenye mechi ya marudiano ambayo itachezwa Oktoba 24 ili kuweza kufuzu hatua ya nusu fainali.

Kabla ya mchezo huo kuanza, ilishuhudiwa shamrashamra za ufunguzi ambazo zilipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo shoo kutoka kwa Msanii nyota nchini, Ali Kiba.Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi alikuwa ni miongoni mwa wageni wakubwa waliohudhuria mchezo huo uliovuta hisia za wengi.Mbali na Dkt. Mwinyi, wageni wengine mashuhuri walikuwa ni Rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi Chapwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *