Na Badrudin Yahya
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema lengo la kuanzisha michuano ya AFL sio kuua michuano mengine ya vilabu barani Afrika badala yake ni kuboresha.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam wakati wa kulitambulisha Kombe la michuano hiyo, Motsepe amesema klabu ambazo zimekuwa zikishiriki michuano ya Afrika zimekuwa hazijiendeshi kwa faida kutokana na gharama wanazokutana nazo wakati wa mashindano.”Tumekaa kamati ili kuona ni namna gani tunaweza kuwa na michuano ambayo inaweza kuzipatia klabu fedha nyingi na ndio maana tumekuja na AFL,” amesema Motsepe.”Nimeondoka Afrika Kusini asubuhi nimeenda kukutana na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan moja kwa moja jijini Dodoma na tuliongea kuhusu maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 na amenihakikishia Serikali itawekeza kuhakikisha inakuwa bora”.Alisema msimu ujao kutakuwa na timu 24 kwenye michuano hiyo ambapo zitapatikana kupitia viwango vya CAF pamoja na mafanikio yao katika ligi za nyumbani.Motsepe ameongeza kwa kusema kuwa baada ya kutamatika kwa michuano hii wao kama CAF watakaa kupitia upya michuano yote iliyokuwa chini yao na kuja na suluhisho zuri.Michuano ya AFL inazinduliwa leo ambapo itachezwa mechi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam baina ya wenyeji Simba SC dhidi ya Al Ahly ya Misri.Wawili hao watarudiana Oktoba 24 na mshindi wa jumla baada ya mechi mbili ataingia kwenye hatua ya nusu fainali.Mechi nyingine kwenye michuano hiyo ni TP Mazembe dhidi ya Esperance de Tunis, Petro de Luanda na Mamelod na mchezo wa mwisho ni kati ya Enyimba dhidi ya Wydad Casablanca.