Na Daniel Mbega,
Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) imeonyesha mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mitatu 2020/21 hadi 2022/23, imeweza kuingia mapato ya Shs. bilioni 68.65.
Hayo yameelezwa jana Oktoba 19, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, CPA Habibu Suluo, katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini ukiwa ni mfululizo wa vikao vinavyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
CPA Suluo alisema, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shs. bilioni 28.53 mwaka 2021/2022 hadi Shs. bilioni 34.17 mwaka 202/2023 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shs. bilioni 5.64 sawa na ongezeko la 20%.
Aidha, alisema, katika kipindi cha miaka mitatu (3) ya utekelezaji wa majukumu ya Latra, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shs. bilioni 25.95 hadi Shs. bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shs. bilioni 8.22 sawa na ongezeko la 32%.
Latra ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, ya mwaka 2019, Sura 413 ili kudhibiti huduma za usafiri ardhini katika Sekta za Reli, Barabara na Waya.
Sheria hiyo ilifuta Sheria Na. 9 ya mwaka 2001 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
“Vyanzo vya mapato ya Mamlaka vinatokana na mapato yatokanayo na kutoa leseni mpya na kuongeza muda wa leseni zilizoisha, mapato ya ushuru kutoka kwa watoa huduma, malipo au mali kwa Mamlaka zitokanazo na shughuli za Mamlaka, michango na misaada inayotolewa kwa Mamlaka, na fedha nyingine zozote zinazopatikana kisheria kutokana na Mamlaka kutekeleza majukumu yake,” alisema Suluo.
Alisema, mapato yatokanayo na adhabu yamepungua na mapato yatokanayo na leseni yameongezeka na hivyo Mamlaka inaendelea kufanikiwa kujenga tabia ya utii wa Sheria na kupunguza adhabu kwa watoa huduma za usafiri ardhini nchini.
Alisema, katika mwaka wa fedha 2020/21, mapato yatokanayo na Ada ya Leseni yalikuwa Shs. 16,648,057,000, Ushuru wa Watoa Huduma Shs. 454,219,000, na mapato mengineyo Shs. 8,843,227,000.
Mwaka 2021/22, mapato ya Ada za Leseni yalikuwa Shs. 17,082,484,000, Ushuru wa Watoa Huduma Shs. 479,941,000, na Mapato Mengineyo Shs. 10,966,529,000.
Kwa mwaka 2022/23, mapato yatokanayo na Ada za Leseni yalikuwa Shs. 23,525,008,000, Ushuru wa Watoa Huduma Shs. 563,133,000, na Mapato Mengineyo Shs. 10,080,587,000.
CPA Suluo alisema: “Mamlaka hupaswa kuchangia asilimia 15 ya mapato yake ghafi kwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (Consolidated Fund) kwa mujibu wa Kifungu cha 11(3) cha Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348 (Public Finance Act, Cap. 348).
“Aidha, Mamlaka hutakiwa kuchangia asilimia 70 ya fedha za ziada (surplus funds) kila mwisho wa mwaka wa fedha kwenda katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 42 cha Sheria ya Bajeti, Sura ya 439.”
Katika kipindi cha miaka mitatu (3), alisema, Mamlaka imeweza kuchangia Shs. bilioni 14.21 katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Akasema, Mamlaka pia imeweza kuchangia taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa kwa niaba ya Serikali ikiwa ni sehemu ya matumizi yake.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC), Tume ya Ushindani (FCC), Baraza la Ushindani Tanzania (FCT), Jukwaa la Afrika la Wadhibiti wa Huduma (African Forum for Utilities Regulators – AFUR) na Umoja wa Taasisi za Reli Kusini mwa Afrika (Southern Africa Railways Association, SARA).
Akizungumzia kuhusu majukumu ya Mamlaka, CPA Suluo alisema, Latra ina wajibu wa kutekeleza majukumu ya sheria za kisekta, kutoa, kuhuisha na kufuta leseni za usafirishaji, ambapo kwa kuzingatia sheria za kisekta, husimamia viwango vya ubora wa huduma na usalama katika sekta zinazodhibitiwa, kusimamamia viwango na masharti ya utoaji wa huduma zinazodhibitiwa, pamoja na kudhibiti viwango vya tozo za huduma.
Majukumu mengine ni kuratibu shughuli za usalama wa usafiri ardhini, kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafiri kibiashara, kuhakikisha na kuthibitisha hali ya usalama wa vyombo vya usafiri kibiashara, kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa sekta zinazodhibitiwa kwa kuangalia viwango vya uwekezaji, gharama, upatikanaji na ufanisi wa huduma, kushughulikia na kuwezesha utatuzi wa migogoro na malalamiko, na kuelimisha umma kuhusu kazi na wajibu wa Mamlaka.
“Mamlaka inao wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji, hivyo Mamlaka hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara. Leseni hizi hutolewa baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma husika. Leseni hizo hutumika kutambua idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa,” alisema Suluo.
Katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, alisema, idadi ya leseni za usafirishaji ziliongezeka kutoka 230,253 hadi 284,158 sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.
Katika jitihada za kulifungua jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine Tanzania Bara, Latra imeanzisha njia za daladala ili kufika maeneo yasiyofikika kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Aidha, alisema katika Jiji la Arusha, Latra ilifanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa za mzunguko kwa lengo kupanua upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji ambayo hayakuwa na huduma.
Suluo alisema, kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (1) (e) cha Sheria ya Latra Sura 413, pamoja na Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Wahudumu, 2020, Mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa.
“Lengo la kuthibitisha madereva ni kupata madereva wenye sifa na weledi kuendesha magari yanayotoa huduma kwa usafiri wa umma kwa kupima umahiri wao hasa maarifa waliyopata ili kuimarisha usalama.
“Katika hatua ya kutimiza jukumu hilo la Kisheria, Mamlaka imekuwa ikiwasajili madereva na baadae kuwafanyia ithibati,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa, hadi kufikia Septemba 30, 2023, madereva 17,990 wamesajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya Mamlaka ambapo madereva 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa na Latra.
Miongoni mwa madereva hao, alisema, madereva wa mabasi wapatao 645 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (Vehicle Tracking System – VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button).
Alisema, matumizi ya kitufe hicho ni kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo VTS.