Samia airejesha ATCL kwenye ndoto za Mwalimu Nyerere

Na Daniel Mbega

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) sasa limerejea katika enzi zile za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye ndoto zake zilikuwa kuona Tanzania inajiimarisha katika usafiri wa anga kwa ajili ya kukuza uchumi na kuimarisha usalama wake.

Jumanne, Oktoba 3, 2023, Tanzania iliingia kwenye orodha ya nchi za Afrika zinazomiliki ndege aina ya Boeing 737-9 Max baada ya ndege ya kwanza kati ya tatu kuwasili ikitokea Seattle nchini Marekani. Ndege nyingine mbili za aina hiyo zinaendelea kuundwa ambapo zinatarajia kuwasili nchini Desemba 2023 na mwezi Machi, 2024.

Tanzania ni nchi ya nne barani Afrika kumiliki ndege hiyo baada ya Nigeria yenye jumla ya ndege 18, Ethiopia (17) na Afrika Kusini (5).

Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 181 katika madaraja mawili ambapo Daraja la Uchumi (Economy Class) ni abiria 165 na Daraja la Biashara (Business Class) abiria 16, pamoja na uwezo wa kubeba mzigo wa tani 6 na kuruka wastani wa saa 8 huku ikisafiri hadi umbali wa kilometa 6,570 bila kulazimika kutua.

Ndege hii ya B737-9 Max ambayo toleo lake la kwanza lilitoka mwaka 2017 inatumia injini ya LEAP-1B ambayo inatengenezwa na CFM International ya Marekani. Gharama yake inatajwa kuwa kati ya Dola za Marekani milioni 128.9 hadi 135 (Shs. 323.79 bilioni hadi Shs. 339.12 bilioni).

Ina urefu wa mita 42.16 na upana wa mabawa yake ni mita 35.9 ikiwa inaendeshwa na marubani wawili na wahudumu wa ndani ya ndege wanne.

Jumla ya oda za Max 9 tangu mwaka 2017 ni 5,651 hadi Agosti 31, 2023 hata hivyo zilizokwisha kufikishwa kwa wanunuzi ni 1,298. Kwa mwaka huu tayari wamewafikishia wateja wao ndege 344 nyingi zikiwa ni Max 9.

Ujio wa ndege hiyo ni jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuliboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) katika usafiri wa anga ili kuhakikisha sekta zote za usafiri zinakidhi mahitaji.

Lakini kutekeleza yote haya, maana yake Rais Samia analirejesha shirika hilo katika maono ya Mwalimu Nyerere, ambaye tangu mwaka 1977 baada ya kuvunjika iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alitamani Tanzania itawale anga.

Ujio wa ndege hiyo ni mfululizo wa utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuimarisha ATCL ambapo Jumamosi, Juni 3, 2023 Watanzania walishuhudia kuwasili kwa ndege mpya ya mizigo Boeing 767-300F.

Julai 2021 Serikali iliingia mikataba na Kampuni ya Boeing ya Marekani ya ununuzi wa ndege nne mpya zenye teknolojia ya kisasa. Ndege hizo mbili za abiria za masafa ya kati aina ya B737-9Max zenye uwezo wa kubeba abiria 181 kila moja, ndege moja ya abiria ya masafa marefu aina ya B787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na ndege moja kubwa ya mizigo aina ya Boeing B767- 300F yenye uwezo wa kubeba tani 54, ambayo tayari ilikwishawasili na inaendelea kutoa huduma zake.

Mpago huu ni mkakati wa Serikali ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 na mpaka sasa shirika hilo linamiliki jumla ya ndege 14 katika uimarishaji wa wigo wa mtandao wa safari za ndege kwa soko la ndani, kikanda na kimataifa.

Ndege zilizoanza kununuliwa wakati huo mbili kubwa ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 262 kila moja, ndege nne za masafa ya kati aina ya Airbus A220-300 ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja.

Nyingine ni ndege tano za masafa mafupi aina ya De Havilland Canada Dash 8 Q400 Bombardier ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ndege kubwa ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.

Azma kubwa ya Rais Samia ya kukuza uchumi kupita nyanja zote kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa ardhini, majini na angani, kwahiyo kuwasili kwa ndege hiyo kunaifanya ATCL ipanue wigo wa safari zake za ndani na nje.

Kwa sasa ATCL inahudumia vituo vya ndani 14 ambavyo ni Mwanza, Bukoba, Songea, Zanzibar, Katavi, Dar es Salaam, Iringa, Geita, Kigoma, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, na Tabora.

Lakini kuwasili kwa ndege hii ya kisasa ya masafa ya kati kutaifanya ATCL kuongeza vituo vya Pemba, Tanga, Mafia, Nachingwea na Musoma kwa mtandao wa safari za ndani, hivyo kufikisha jumla ya vituo vya ndani 19.

ATCL inahudumia vituo vya kikanda na kimataifa 12 ambavyo ni Entebbe-Uganda, Nairobi-Kenya, Bujumbura–Burundi, Hahaya-Comoro, Lubumbashi-DRC, Ndola na Lusaka–Zambia, Harare-Zimbabwe, Johannesburg–Afrika Kusini, Mumbai–India, Guangzhoa–China na Dubai.

Ndege mbili nyingine zitakapowasili Desemba 2023 na Machi 2024, mtandao wa safari za nje utaongezeka ambapo ATCL itaendelea kuongeza miruko ya kwenda Mumbai-India na Guangzhou-China na kuanzisha safari mpya za Kinshasa na Goma ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Dubai, Muscat-Oman na Lagos-Nigeria.

Mwanzo wa mageuzi

Rais Samia anaendeleza pale alipoishia mtangulizi wake, Dkt. John Magufuli, ambaye alianzisha jitihada za kulifufua shirika hilo lililokuwa likikabiliwa na madeni mengi huku likiwa halina hata ndege moja.

Wapiga dili waliligeuza kitegauchumi chao, ambapo ilifikia mahali hata sare za wahudumu zilishoneshwa ng’ambo kwa mamilioni ya shilingi, fedha halali za walipa kodi na wavuja jasho wa Tanzania.

Ujio wa ndege hizi umerejesha heshima ya Tanzania katika usafiri wa anga tofauti na ilivyokuwa nyuma ambapo siyo tu serikali ilikuwa ikikosa mapato kwa kushindwa kusafirisha abiria, lakini hata kiusalama haikuwa vizuri kwa kuwa ndege zilizokuwa zikifanya safari ni za binafsi.

Leo hii Watanzania wanafurahia safari za ndani zenye uhakika, tena kwa gharama nafuu kulinganisha na mashirika ya binafsi, hatua ambayo imewafanya wawe na imani kubwa na serikali ya sasa.

Tunapaswa kujiuliza pia kama kweli shirika letu halikuwa linahujumiwa, life ili watu wengine waingize midege yao na kuchukua ukanda katika usafiri wa anga.

Twende ndani tukachunguze na kuona ni akina nani wanamiliki mashirika yaliyofumuka tangu mwaka 1997, huku ATCL ikifilisika na kukodishwa kabla ya kuchungulia kaburi.

Haitashangaza hata mara moja kukuta wapo vigogo waliopata kuwa na nyadhifa za juu za maamuzi serikalini, ambapo hata mashirika hayo ya binafsi yalianzishwa wao wakiwa madarakani.

Kumiliki ndege ni gharama, hilo halina ubishi na hasa suala la matengenezo, lakini hatuwezi kukwepa kununua ndege eti kwa sababu ya gharama, vinginevyo hatuna haja hata ya kufanya kazi au kuweka akiba kwa sababu sote ipo siku tutakufa!

Tukitaka ATCL iimarike na itengeneze faida baadaye, lazima kuja na mkakati wa kupambana na ushindani katika bei badala ya kuweka nauli za juu, kwa sababu hiyo ndiyo itakuwa silaha kubwa ya kujiendesha, achilia mbali silaha ya msingi – Uzalendo!

Ndoto ya Mwalimu

Anachokifanya Rais Samia ni kufufua ndoto ya Mwalimu Nyerere aliyelianzisha shirika hilo miaka 46 iliyopita, na kamwe hakukosea.

Ilikuwa Ijumaa, Machi 11, 1977 wakati Shirika la Ndege Tanzania (ATC) linaanzishwa, Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa na ndoto za kuona Tanzania inajiimarisha katika usafiri wa anga.

Usafiri wa anga wakati huo ulikuwa umesimama kwa muda baada ya kuvunjika kwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA) kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka huo, kwani EAA ilimilikiwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania ya Uganda.

Itakumbukwa kwamba, baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, usafiri wa anga kwa kiasi kikubwa ulikuwa mikononi mwa Kenya, wakati Tanzania yenyewe ilibaki na usafiri wa reli.

Kwa maana nyingine, Kenya, ambayo ilikuwa imeanzisha Shirika lake la Ndege (Kenya Airways), ndiyo iliyokuwa ikitawala usafiri wa anga wakati huo.

Jambo hili lilimfanya Mwalimu Nyerere aone umuhimu wa kuanzisha haraka Shirika la Ndege Tanzania na mara tu ATC ilipoanzishwa, serikali ikakodi ndege yake ya kwanza aina ya Douglas DC-9-32, 5Y-ALR (ambayo ilikuwa miongoni mwa zilizokuwa ndege za EAA) kutoka Kenya Airways.

Mwaka huo huo zikapatikana ndege nyingine ndogo mbili, DC-9-32 5Y-ALR na Fokker F27-600, PH-EXC c/n 10566 iliyotoka Schiphol, Uholanzi.

Baadaye zikapatikana ndege nyingine aina ya DeHavilland Canada DHC6 Twinn Otter 300 5H-MRB c/n 579 mwaka 1978 na Boeing 720-022 N62215 ilikodishwa mwaka 1979 kutoka Caledonian Airlines INC, lakini ATC ililazimika kuvunja mkataba huo miezi mitatu baadaye kutokana na mkodishaji kupunguza idadi ya abiria waliopaswa kusafirisha, ni abiria 28 tu.

Katika miaka hiyo Enzi za Mwalimu hasa mwaka 1980-1981, ndege za ATC zilifanya safari nyingi za kitaifa na kimataifa kwa kutumia ndege zake za Boeing 707 na 737 na Fokker kutoka Dar es Salaam hadi Athens – Ugiriki (707), Antananarivo – Madagascar (737), Bombay – India (707), Bujumbura – Burundi (737), Cairo – Misri (707), Frankfurt – Ujerumani (707), Kigali – Rwanda (737), London Gatwick – Uingereza (707), Mahe – Shelisheli (737), Maputo – Msumbiji (737), Mauritius (737), Moroni – Comoro (FKF), Muscat – Oman (737) na Rome – Italia (707).

Kuanzia kiangazi cha mwaka 1981, safari zilifanywa kwa kutumia ndege ya Boeing 707-320 (N762TW c/n 17675 “Ngorongoro Crater”) kwenda Misri-Ulaya, Dubai-Pakistan-India ingawa safari hizo zilivunjwa baada ya ndege hiyo kupata ajali kwenye uwanja wa ndege Dar es Salaam.

Kulikuwa na safari nyingi za ndani kutoka Dar es Salam hadi Bukoba (DHT), Dodoma (DHT/FKF), Iringa (DHT), Kigoma (737), Kilimanjaro (707/737/DHT/FKF), Kilwa (DHT/FKF), Lindi (FKF), Mafia (DHT), Masasi (DHT), Mbeya (DHT), Mtwara (737/DHT/FKF), Musoma FKF), Mwanza (737/FKF), Nachingwea (FKF),  Njombe (DHT), Pemba (DHT/FKF),Songea (FKF), Tabora (FKF), Zanzibar (DHT/FKF).

Safari nyingi za ndani ziliongezeka kwa kutumia ndege za Boeing 737-2R8C (Adv) 5H-ATC c/n 21710 “Kilimanjaro” na Fokker F27-600RF Friendship 5H-MPU c/n 10569 na Serikali ikaongeza ndege ya De-Havilland Canada DHC-6 Twin Otter 5H-MRC kwa ajili ya safari za ndani kutoka Kilimanjaro.

Na tunakumbuka jinsi ndege yetu ya 5H-ATC Boeing 737-2R8C ilivyotekwa mara mbili – mara ya kwanza Februari 26, 1982 kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiruka kwenda Dar es Salaam ambapo akina Mussa Membar na wenzake waliiteka kwa kutumia bastola bandia na kuipeleka London, Uingereza.

Mara ya pili ilikuwa Februari 13, 1988 wakati watekaji wawili walipoiteka kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ikijiandaa kwenda Nairobi wakitaka ndege hiyo iwapeleke Stanstead, Uingereza. Tukio hilo lilidumu kwa siku mbili na watekaji walikamatwa baada ya ndege kuzingirwa.

Baada ya Mwalimu

Tangu Mwalimu Nyerere alipoondoka madarakani na hasa baada ya ndege kadhaa za ATC kuharibika kutokana na ajali na uchakavu, shirika hilo likaanza kuyumba na kupoteza kabisa mwelekeo.

Kwanza, kati ya mwaka 1991 na 1992 Serikali ikakodisha ndege ya Boeing 767-200 ET-AIZ kutoka Shirika la Ndege la Ethiopia lakini ndege hiyo ilionekana kuwa kubwa zaidi na haikuwa na maslahi, hivyo ikabidi irudishwe kwa wenyewe.

Mnamo Desemba 12, 1993, ndege ya 5H-MPT Fokker F27 ilianguka wakati ikitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Ndege hiyo ikaondolewa kwenye orodha na ikatumika kwa vipuri tu.

Mnamo mwezi Mei 1994, kampuni ya Shannon Aerospace ya Ireland ilikodishwa kuzitengeneza ndege mbili za Boeing 737-200C, ndege tatu za De Havilland DHC-6 Twin Otter 300 na ndege tatu za Fokker F27-600.

Lengo la ATC lilikuwa kufufua ndege hizo ili zichukue nafasi ya ndege kongwe ya Boeing 737 kwa kutumia model mpya ya Fokker F27 na mbili za Fokker 50.

Wakati huo safari za kimataifa zilikuwa Bujumbura, Djibouti, Entebbe, Gaborone, Harare, Johannesburg, Kigali, Lilongwe, London, Lusaka na Muscat. Safari za Johannesburg zilifanywa na Air Malawi kwa niaba ya ATC.

Ni katika kipindi hiki ambapo ATC iliingia katika mazungumzo ya kuwa na hisa asilimia 10 kwenye Ushirikiano wa Pamoja na Shirika la Alliance Air (baadaye ikajulikana kama SA Alliance), shirika la ndege ambalo lilikuwa na makao yake kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe, Uganda.

Makubaliano hayo yakafikiwa mwaka 1994 kati ya ATC, Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na Shirika la Ndege la Uganda kwa lengo la kushindana na mashirika ya ndege ya kimataifa. Ushirika huo ulikuwa na ndege moja aina ya Boeing 747SP-44, ZS-SPA cn 211321/280 iliyokodishwa kutoka Shirika la Ndege la Afrika Kusini ambapo ilifanya safari zake kati ya Afrika Mashariki na Ulaya.

Ubia huo ulikoma Oktoba 2000, baada ya kuingia hasara ya Dola za Marekani milioni 50.

ATC ilibinafsishwa mwishoni mwa mwaka 1998 na mipango ya kuiunganisha moja kwa moja na Alliance Air ilishindikana. Shughuli za Alliance Air zilikoma mwaka 1999 kutokana na mzigo mkubwa wa madeni. Wakati huo Alliance Air ilikuwa ikifanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na London – Heathrow kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe.

Kutokana na hilo, mipango ya kulibinafsisha shirika la ATC likabaki chini ya serikali kama ilivyokuwa awali.

Wakati huo huo, ndege ya Boeing 737-200, 5H-ATC ilitakiwa kufanyiwa uchunguzi (C-check), ATC ikakodisha ndege ya Boeing 737-300 XA-SWO c/n 27284 “Ngorongoro” kutoka Transportes Aéreos Ejecutivos (TAESA) ya Brazil kwa kipindi kifupi.

Ndoa ya ATC, SAA

Mnamo Februari 2002, serikali ikaanza mchakato wa kulibinafsisha shirika la ATC kwa kutangaza zabuni kwenye magazeti ya ndani na kimataifa. Mashirika manne kati ya nane yakaingia kwenye mchakato huo ambayo ni Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), Kenya Airways, Shirika la Ndege la Comair (Afrika Kusini) na Nationwide Airlines pia la Afrika Kusini.

SAA ikashinda zabuni hiyo na Desemba 2002 wakasaini mkataba ambapo serikali ilikuwa na asilimia 51 ya hisa kwenye ATC.

Kwa bahati mbaya, ndege mbili za Boeing 737-2R8C (Adv) – 5H-ATC na 5H-MRK zikaondolewa kwenye huduma na kupelekwa Afrika Kusini. SAA ilikuwa na mpango wa kununua ndege za Boeing 737-800 lakini badala yake ikanunua ndege kuu kuu za Boeing 737-200, mbili za Fokker F-28 na mbili za De Haviland Dash 8-315.

Mnamo Januari 31, 2005, ATC ikafuta moja kati ya safari zake za kimataifa kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi kutokana na ushindani mkubwa kutoka Kenya Airways.

Mwaka huo huo ATC ikatangaza kupata hasara ya Dola milioni 7.3 katika mwaka wake wa kwanza wa ubia na SAA, hasara ambayo ilichangiwa na kushindwa kupanua safari zake kwani awali ilikuwa imepanga kupanua safari zake kwenda Dubai, India na Ulaya lakini ikashindikana kwa kuwa ndege pekee walizokuwa nazo ni Boeing 737-200 ambazo pia zilikuwa kuu kuu.

Septemba 7, 2006 Serikali ikanunua asilimia 49 kwenye ATC kwa gharama ya Dola milioni 1, hali iliyomaanisha kuvunja mkataba na SAA.

Mkataba huo ulivunjika kutokana na haja tofauti za wanahisa. Ndege mbili za Boeing 737-247 Adv, 5H-MVV na 5H-MVZ zilikuwa zimekodishwa kutoka Celtic Capital Air Corporation, Canada kwa miaka miwili kwa gharama ya Dola 50,000 kwa mwezi.

Mnamo Septemba 2007 kampuni ya Air Tanzania Company Limited (ATCL “Wings of Kilimanjaro”) ilianzishwa baada ya kuvunjwa kwa mkataba na SAA na ilikuwa na safari za Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Kilimanjaro.

Mnamo Oktoba 2007 ATCL ikakodisha ndege ya Airbus A320 kutoka kampuni ya Wallis Trading Company kwa muda wa miaka sita.

Ukodishaji huo ulikuwa sehemu ya mchakato wa ubia, ambapo ATCL ilikuwa iuzwe kwa hisa kwa kampuni ya Sonangol ya China, ambayo haikuwahi kusaini mkataba wowote rasmi wa makubaliano na serikali ingawa ilikuwa imeahidi kuinunulia ATCL ndege tano za Airbus hadi kufikia mwaka 2012 kama sehemu ya mpango wa ubinafsishaji.

Kwa kujua kwamba walikuwa wanaingia mkataba na Sonangol, menejimenti ya ATCL ikaharakisha kukodisha ndege ya A320-214 kutoka Wallis Trading, kampuni ambayo ilikuwa imedai kuwa na uhusiano na Sonangol ya China iliyoongozwa na mfanyabiashara wa Hong Kong, Sam Pa. Ndege hiyo ilikuwa imefanya huduma Liberia ambako ndiko ilikokodishwa, lakini kabla ilikuwa imekodishwa huko El Salvador.

Lakini wakati ATCL inaingia mkataba wa kuikodisha Oktoba 2007 ndege hiyo ilikuwa inatakiwa kufanyiwa ukaguzi (C-check) ndani ya miezi sita, hivyo kuingia katika hasara nyingine. Iliporejea kutoka kwenye matengenezo Mei 2008, ndege hiyo iliruka angani kwa miezi saba tu hadi Desemba 2008 wakati ilipoegeshwa ili ifanyiwe matengenezo mengine ya D-ckeck na haikuwahi kuruka tena angani, hadi ilipokodishwa na ATCL Oktoba 2011. Hiyo ilikuwa ni miaka miwili kabla ya mkataba wa ukodishaji kumalizika lakini gharama za ukodishaji zikabakia pale pale kana kwamba ndege ilikuwa ikifanya kazi katika muda wote wa mkataba.

Hali hii inadhihirisha namna ufisadi ulivyokuwa ukifanyika kiasi cha kulifilisi shirika hilo.

Mwaka 2008 ATCL ilikodisha ndege za 5H-MWH Airbus A320-214 c/n 363, 5H-MVV Boeing 737-247 Adv c/n 23520, 5H-MVZ Boeing 737-247 Adv c/n 23607, 5H-MWF De Havilland Canada DHC-8Q-311 DASH 8 c/n 475, na 5H-MWG De Havilland Canada DHC-8Q-311 DASH 8 c/n 462.

Tangu wakati huo hali ikawa mbaya zaidi kwa sababu Januari 2009 ndege mbili za Airbus A320 na Boeing 737 zikaondolewa katika utoaji huduma.

Kwahiyo, kinachofanywa na Rais Samia ni uimarishaji wa Shirika hili ambalo lilikwishakufa kwa sababu ya ‘upigaji wa dili’ na sasa heshima ya Tanzania imerejea kama Mwalimu Nyerere alivyokuwa akitamani kuliona.

Kijijini Msanga-Ngongele,

Kisarawe

0629-299688

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *