RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shs. bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Kisasa la Nzega Parking mkoani Tabora ili kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwenye mazingira mazuri.
Rais Samia alitoa alitoa fedha hizo alipotembelea soko hilo kufuatia ombi la Mbunge wa Nzega na Waziri wa Kilimo kumuomba kutembelea soko hilo.
Katika mazungumzo yake akiwa sokoni hapo, Rais Samia aliwaomba wafanyabiashara hao kupisha ujenzi na kumuelekeza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kuhakikisha soko likikamilika wafanyabiashara waliopisha ujenzi wanapewa kipaumbele.
Akiwa katika skimu ya umwagiliaji akiweka jiwe la msingi katika shamba la kuzalisha mbegu wilayani Nzega mkoani Tabora, Rais Samia aliahidi kuzifanyia kazi changamoto za wafanyakazi wa mradi wa shamba la kuzalisha mbegu na kuweka msisitizo ifikapo 2030 nchi iwe imejitosheleza kwa mbegu.
Akizungumzia Mradi huo Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema shamba hilo limeitwa ‘Samia Block Farm’ lina hekta 1,102 na bwawa lenye ukubwa wa hekta 140 na hifadhi yake ni hekta 97.
Alisema eneo linalofaa kwa ajili ya umwagiliaji ni zaidi ya hekta 860 ambapo aina nyingine ya shamba kama hilo lipo Arumeru.
Alisema kwa sasa mahitaji ya Mbegu ni tani 120,000 na mahitaji wa shamba ya serikali na binafsi ni zaidi ya tani 40,000 ili nchi ijitosheleze ambapo nchi inahitaji hekta 30,000 ili kuondoa changamoto ya mbegu hadi kufikia 2030.
Alisema mbegu za Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA) na wakala wa Taifa wa uzalishaji na uendelezaji wa mbegu (TARI) ni tani 17,000.
Akiwa katika Kijiji cha Puge Wilaya ya Nzega, Mbunge Jimbo la Nzega Vijijini, Hamis Kigwangala alisema Mkoa wa Tabora hawana malalamiko.
“Sisi wananchi wa Nzega na Tabora, hatuna malalamiko, tuna shukrani zaidi ya malalamiko tuna pongezi zaidi ya malalamiko tunakushukuru kwa miradi ya maendeleo iliyofika katika Jimbo letu la Nzega vijijini na Halmashauri yetu ya Wilaya ya Nzega,” alisema.
Alisema wakati akiingia kwenye Jimbo hilo kulikuwa na majimbo mawili ambapo walikuwa wakipata sh milioni 400 kwenye sekta ya maji kwa Wilaya nzima ambapo tangu Rais Samia kuingia madarakani wamepokea miradi ya maji ya sh bilioni 19.3 katika kipindi cha miakam miwili.
Alisema kwenye sekta ya elimu waannchi walishiriki wenyewe kujenga sekondari zao za kata lakini alipoingia madarakani sekondari mpya 2 zimejengwa.
Alisema upatikanaji wa maji ulikuwa nia silimia 28 na sasa upatikanaji wakeni zaidi ya asilimia 79 na kufikia 2025 itavuka asilimia 90.
Alisema vijiji vyote katika Jimbo hilo vimepata umeme na vituo vya afya vimejengwa vinavyotoa huduma kwa wananchi.
Rais Samia alisema serikali imejipanga kujenga skimu za umwagiliaji maji, kutoa ruzuku za pembejo za kilimo na mboleo, mbegu kwa bei ya chini hivyo aliwataka wananchi kulima kwa nguvu kubwa na kupata mavuno na kulisha nchi na dunia.
“Sasa hivi hakuna lugha ya mazao ya biashara na mazao ya chakula mazao yote ni biashara na ni chakula,” alisema.
Alisema Serikali inatarajia kuweka viwanda vidogo, vya kati katika mazao yote ili kuongeza thamani ya amzao hayo ili kuuza ndani nan je ya nchi.
“Siku hizi hatusemi tu kilimo, ila tunasema kilimo biashara niwaombe tuweka amani, utulivu mshikamano na umoja ndani ya nchi yetu twende tukafanye kazi tupate mavuno mengi, tuchimbe madini mengi tuuze tupate fedha ili maendeleo yaje kwa haraka zaidi makubwa kuliko haya tunayoyasikia leo,” alisema.