Samia anavyoutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa

Na Daniel Mbega,

Kisarawe

JUMATATU, Agosti 21, 2023, wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) jijini Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema bayana kwamba, hakuna mwenye misuli wala ubavu a kuligawa Taifa la Tanzania.

Akasisitiza kwamba, hakuna mtu mwenye uwezo wa kuvuruga wala kuharibu amani na usalama wa Taifa hilo.

“Baba Askofu, nimeisikiliza risala yako kwa umakini, niliamua kunyamaza kimya na naomba niwahakikishie kuwa, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili, kuuza taifa hili wala kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye Taifa hili,” akasema Rais Samia baada ya kusikiliza kwa makini hotuba ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Frederik Shoo, ambaye aliitaja Misingi Mikuu ya Kanisa ambayo ilijumuisha Usalama, Amani, Umoja na Muendelezo wa Taifa na akawaomba viongozi wapya watakaochaguliwa kuendeleza misingi hiyo Mikuu ya Kanisa. 

Kauli hii ya Rais Samia ni muendelezo wa jitihada zake njema za kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa, ambao misingi yake iliwekwa na waasisi wa Taifa hilo, mahayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Rais Samia amekuwa imara katika kuhakikisha misingi hiyo iliyoifanya Tanzania iendelee kudumu hadi sasa haiyumbishwi na mtu awaye yote.

Hata wakati wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mashujaa, Jumanne, Julai 25, 2023 kwenye Mji wa Serikali Mtumba katika Uwanja wa mpya wa Mashujaa jijini Dodoma, Rais Samia aliwasisitiza Watanzania kuilinda na kuienzi misingi hiyo muhimu ambayo ndiyo inayodumisha utaifa wetu.

Aliwataka Watanzania kutokubali kugawanywa kwa kisingizio chochote na kwamba Tanzania ni moja na haitagawanyika, huku akihimiza Watanzania kuwaenzi mashujaa, kudumisha amani, umoja, mshikamano, utulivu wa nchi na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

“Kamwe tusikubali mtu yeyote au kikundi cha watu kutugawa kwa kisingizio chochote kile, Tanzania ni moja na kamwe haitagawanyika,” alisema.

Rais Samia amedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kulinda tunu za taifa na kuendeleza amani, utulivu wa nchi, umoja wa kitaifa ili kufikia maendeleo ambayo wananchi wa Tanzania wanayaangalia na kuyategemea kutoka kwake.

Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa ni mradi mkubwa ambao Mwalimu Nyerere aliuanzisha, aliusimamia, ingawa tunaona sasa unavyoporomoshwa na baadhi ya wachache na kuliacha taifa letu mashakani.

Mwalimu alijenga misingi imara ya Ujenzi wa Umoja Wa Kitaifa (Nation Building). Kuijenga jamii ya Watanzania yenye kuamini kwenye ukweli kuwa sisi sote ni ndugu. Kwamba nchi yetu haina dini. Yenye kupiga vita ubaguzi wa aina zote, iwe wa rangi, kabila au dini. Ilimchukua Mwalimu na taifa letu miaka mingi sana kuijenga misingi hiyo iliyowawezesha pia Watanzania kuwa na mioyo ya uzalendo kwa Taifa lao.

Tunaona sasa kazi hiyo iliyochukua miaka mingi, kutokana na ubinafsi na uroho wa madaraka ya baadhi ya wanasiasa wetu, wanapelekea kubomoka kwa misingi hiyo na kuliacha taifa letu kwenye hatari ya kuangamia.

Ndiyo, msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa niaba yetu, na tamaa ya madaraka mwa wale walio kwenye miamvuli ya vyama vya siasa wanaotaka kwenda Ikulu kwa ‘gharama yoyote ile’, ikiwemo kuleta taharuki kwa Watanzania kwa kusambaza maneno yenye chuki dhidi ya Serikali iliyoko madarakani.

Ni hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi na wanasiasa, hasa wanaharakati wa kisiasa kutoka upinzani, kuishiwa chembe chembe za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.

Ni watu wenye kulinda maslahi yao na ya wanaowazunguka au wanaowatuma – mabeberu. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza malengo yao. Baadhi ya Watanzania sasa wanapoteza moyo wa uzalendo kwa nchi yao.

Kuna hata wenye kufikia kutamka; ‘Nchi hii ina wenyewe’. Kuna anayetamka hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali.

Hizi si dalili njema kwa taifa. Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua kali. Hakuna anayewagusa. Ukiuliza utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”. Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii, hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao.

Ni hatari. Tuna lazima ya kuwa na ujasiri wa kupigania maslahi ya nchi yetu. Ni heri kufa kwa kupigwa risasi kuliko fedheha ya kufa kwa kuumwa na mbu wa Malaria katika nchi ambayo ina rasilimali za kutuwezesha kujenga uwezo wa kuangamiza Malaria.

Mwalimu Nyerere aliliona hili mapema, akalikemea, akachukua hatua stahiki na kukita misingi inayowafanya hata hao wanaofanya uchochezi watembee vifua mbele kwa sababu kuna amani na utulivu.

Tunapaswa kuijenga Tanzania imara, yenye maelewano na mshikamano. Siyo Tanzania yenye mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbali mbali wenye kwenda kwa staili ya ‘kila mtu na lwake’. Idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi, hasa wanasiasa.

Rais Samia ameliona hili, ndiyo maana anaendelea kusimamia Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa.

Katika salamu zake wakati wa Maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Jumatano, Aprili 26, 2023, Rais Samia aliwataka Watanzania kudumisha umoja, amani na ustawi kama ilivyokuwa ndoto ya waasisi wa Muungano.

Muungano huo unatokana na maono ya waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume.

“Nawatakia nyote kheri tunapoadhimisha miaka 59 ya Muungano, imekuwa miaka 59 ya umoja yenye amani na ustawi kama ilivyokuwa ndoto ya waasisi wetu, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Tuendelee kuidumisha tunu hii adhimu na ya kipekee kwa taifa letu,” alisema Rais Samia.

Kuliombea Taifa

Katika kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Taifa, Samia amekuwa akihimiza makundi mbalimbali, wakiwemo viongozi wa dini, kuliombea Taifa na kudumisha amani na mshikamano, kwani anaamini ujenzi wa Taifa ni wa kila mmoja wetu.

Mnamo Mei 31, 2023, Rais Samia alipiga simu wakati kongamano la viongozi wa dini likiendelea mjini Mbeya likiwahudhurisha waumini zaidi ya 800 kutoka madhehebu mbalimbali, ambapo alisisitiza amani, utulivu na utengamano wa kisiasa na kiuchumi.

Rais Samia akasema anatambua kazi kubwa ya viongozi wa dini na kuwaomba kuendelea kuliombea Taifa kuwa na amani na mshikamano akieleza kuwa mchango wa viongozi wa dini ni mkubwa kwa maendeleo ya nchi.

“Nawashukuru sana kwa mchango wenu, niwaombe muendelee kuliombea Taifa letu tuzidi kuwa na amani, upendo na mshikamano wafikishieni salamu zangu kwa wananchi na Watanzania wote,” alisema.

Katika kongamano hilo, viongozi hao walimuombea mwaka 2025 kushika nafasi hiyo tena kutokana na nchi kuwa salama, kuwa na amani na maadui wanaoitakia ubaya Tanzania wameshindwa.

Kuhusu Haki

Rais Samia amekuwa akisisitiza kudumisha misingi ya haki na ndiyo maana, Septemba 4, 2023, kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa maafisa wakuu waandamizi wa jeshi la polisi Tanzania, jijini Dar es Salaam, alilitaka jeshi hilo kusimamia haki, usalama kwenye chaguzi zinazotarajiwa kufanyika nchini pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria haraka dhidi ya mtu ama kikundi chochote kitakachovunja sheria za nchi kwa kisingizio chochote.

Alisema, mwaka 2024 kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo Polisi wanapaswa kulinda amani pamoja na Uchaguzi Mkuu, mwaka 2025.

“Mwakani kuna uchaguzi wa serikali za mitaa, tunataka jeshi la polisi liwe makini kweli kweli huko kusimamia haki itendeke, kusimamia usalama katika chaguzi zetu kuhakikisha zinakwenda kwa njia ya usalama na vile vile mwaka 2025,” alisema.

Rais Samia alisema, kama kutakuwa na mtu atakayevunja sheria za nchi basi anapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Kama wanavunja sharia za nchi huyo anavunja sheria za nchi na lazima ashughulikiwe kama mvunjaji wa sheria za nchi,” alisema.

Alilitaka jeshi hilo kuimarisha dhana ya ulinzi shirikishi itakayojengeka na kuimarika miongoni mwa wananchi ili kila mmoja ajione ana jukumu la kuhakikisha usalama mahali alipo unamtegemea yeye.

“Tunataka wananchi wawe huru kutekeleza majukumu ya kujenga taifa bila hofu,” alisema.

Alisema serikali imejidhatiti na kuendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha ulinzi na usalama nchini kwa kuendelea kuwezesha vikosi mbalimbali.

Alisema Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya jeshi hilo, maslahi na stahiki za askari, kuimarisha mazingira ya kazi na makazi, kuongeza zana na vitenda kazi, kuhamasiaha matumizi ya Tehama pamoja na mafunzo kwa askari.

Rais Samia alisema bado kuna malalamiko ya rushwa kutoka kwa wananchi kwa baadhi ya askari hasa wa usalama wa barabarani ambapo teknolojia itamaliza tatizo hilo.

Alisema bado anapokea vikaratasi vya malalamiko ya kubambikiziwa kesi kwenye vituo vya polisi ambalo aliomba liangaliwe kwa makini.

Rais Samia pia alikwishasema kwamba, Serikali yake imejikita katika kupitia upya mifumo ya utoaji haki iliyopo ambayo imechangia kuvuruga mifumo ya haki jinai na kupuuza mifumo ya maadili na kusababisha baadhi ya wananchi wasio na uwezo kiuchumi kupoteza haki zao.

Uhuru wa Kutoa Maoni

Rais Samia amerejesha uhuru wa kutoa maoni, ambao umeshuhudia hata vyombo kadhaa vya habari vilivyokuwa vimefutwa katika utawala uliotangulia vikifunguliwa ikiwa ni pamoja na kuruhusu mikutano ya siasa za majukwaani, ambayo ilifutwa kwa miaka sita nyuma.

Hizi zote ni harakati zake za kuhakikisha Umoja wa Kitaifa unadumishwa na wananchi wanaishi kwa amani na upendo.

Hata hivyo, Septemba 11, 2023 wakati akifungua mkutano wa Baraza Maalum la Vyama vya Siasa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia mikutano ya hadhara kutoa hoja na fikra zenye tija zinazolenga kuimarisha utendaji serikalini.

Akavitaka vyama vya siasa kutumia mikutano ya hadhara kujitangaza ili kukua kisiasa na kuutumia uhuru wa kujieleza kutoa mawazo mbadala yatakayoendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akasema, uhuru wa kutoa maoni usisababishe kudhalilisha watu wengine, kuibua hisia za kidini, ukabila au kubaguana kwa misingi yoyote ile.

Rais Samia akasisitiza kutumia uhuru huo vizuri bila kuingilia haki na uhuru wa watu wengine pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu.

“Serikali haikuruhusu mikutano ya hadhara ili watu wakavunje sheria, kutukana, kukashifu, kuchambua dini za watu. Serikali iliruhusu mikutano ya hadhara kwa lengo la kuwezesha vyama kuzungumza na kukua.

“Tulitaka vyama vizungumze, wananchi wasikie sera zao, mada zao, mipango yao ili vyama vikue na virudishe watu wao waliowapoteza … vyama viwe madhubuti tukienda kwenye uchaguzi kila chama kimejijenga vya kutosha.”

Rais wa Samia alisema kuwa falsafa zake za maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na ujenzi mpya amezichukua kama msingi unaomuongoza katika kuongoza nchi ili isonge mbele kama Taifa kwa pamoja.

“Kuna uhuru wa maoni lakini uhuru wa maoni una mipaka yake siyo tu kisheria hata kibinadamu, kama ulizaliwa ukalelewa vyema ukapitishwa kwenye masomo tunayosoma, lakini ukapitishwa kwenye masomo ya dini ukaielewa vizuri, kuna mambo huwezi kufanya tu, kama ulipata malezi mazuri ukaijua dini yako ukakua kwenye misingi mizuri kuna mambo huwezi kufanya.

“Utasikia mama una kifua unastahimili, utafanyaje? Jamani kama mwendawazimu anachukua nguo zako anaenda mbio na wewe utoke utupu, umfukuze? Mwendawazimu ni yupi? Wengine tulilelewa kwenye maadili tukapitishwa kwenye dini, huwezi kufanya hayo na mwingine kaumbwa hivyo roho yake basi tu raha yake aone ugomvi, mabishano na huyo amua leo, mimi nakupa Serikali na wenzio hao kwenye kikundi, ataunda chama kingine awapinge wale wale wenziwe aliokuwa nao.

“Na ndio tunayoyaona huko kwao, ukiona hawapo si tu kwamba kuna kununa, hakukaliki huko ndani, wengine twende wengine tusiende, sasa kwa tabia kama zile watakuwa na amani kweli?

Demokrasia na maisha ya wananchi

Jumatatu, Julai 17, 2023 akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Demokrasia Afrika uliofanyika jijini Arusha, Rais Samia alisema ili demokrasia iwe na maana kwa maisha ya wananchi ni lazima ilete matokeo katika huduma muhimu za jamii na kuboresha maisha ya wananchi.

Alisema, demokrasia lazima iwe njia thabiti iliyothibitishwa kuwaunganisha wananchi.

“Serikali kushindwa kutoa huduma kwa wananchi ndio sababu ya kuanzisha kwa mifumo ya kuwasilisha mahitaji ya wananchi kama uwepo wa wanaharakati, maandamano kushinikiza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi na hapa ndipo uhuru wa kujumuika na kutoa maoni unapotumika tofauti,” alisema.

Alisema, haoni mbadala wa demokrasia kama nchi za Afrika hazitakuwa na mikakati ya kuwa na maendeleo endelevu na uchumi imara akisisitiza demokrasia ina uhusiano mkubwa na masuala ya amani na ukuaji wa kasi wa uchumi.

Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kutembea katika nyayo za Mwalimu Nyerere katika kuhakikisha kwamba Mradi wa Ujenzi wa Taifa unaendelea na kufanikiwa.

0629-299688

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *