Samia ataka kasi usambazaji maji

*Bil. 24.47/- kutoa maji Ziwa Victoria

*Azungumzia neema nishati ya umeme

Na Salha Mohamed, Singida

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Maji na wakandarasi kuongeza kasi ya usambazaji maji ili yaweze kuwafikia wananchi zaidi kwa wakati.

Alisisitiza umuhimu wa matumizi ya mita za maji kama suluhu ya malalamiko ya ubambikizaji gharama za maji kwa watumiaji.

Rais Dkt. Samia aliyasema hayo jana wakati akizindua mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya Mji wa Shelui katika hafla iliyofanyika kwenye Kijiji cha Kizonzo, Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.

“Huu mradi umegharimu sh. ilioni 24.47, bado sh. bilioni 16 zimebaki, zinaenda kutumika katika usambazaji maji katika maeneo mengine,” alisema Rais Dkt. Samia.

Alisema matumizi ya mita za maji yatawawezesha wateja kutumia maji kadri ya malipo na yakiisha maji yanakata.

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kabla ya kufika mwaka 2025, Mkoa huo na kila eneo ndani ya mipaka ya Tanzania litakuwa imeunganishwa na nishati ya umeme.

Rais Dkt. Samia alimaliza ziaraya kikazi mkoani Singida, iliyodumu kwa siku mbili tangu Oktoba 15-17, 2023 na kuanza ziara ya siku mbili mkoani Tabora.

UZINDUZI CHUO

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia jana aliweka jiwe la msingikatika Chuo cha VETA wilayani Igunga, akiwa katika ziar ya kikazi mkoani Tabora.

Alisema Serikali itajenga vyuo 64 vya Ufundi Stadi (VETA) nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya serikali kujenga vyuo hivyo kila Wilaya.

“Chuo hiki ni sehemu ya jitihada ya serikali kuwapa vijana elimu ya amali ili waweze kujiajiri au kuajiriwa,” alisema Rais Dkt. Samia.

Aliongeza kuwa, mikakati ya serikali ni kuhakikisha kila mkoa nchini kunakuwa na Chuo cha VETA cha Mkoa, lengo ni kuwawezesha wananchi kuwa na ujuzi wa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.

Aliwataka wananchi wa Tabora kulima kwa juhudi kwani masoko ya mazao yao ni ya uhakika na kwamba serikali inaendelea na juhudi za kuwatafutia masoko nje ya nchi, pindi masoko yanapokuwa changamoto serikali itayanunua mazao yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *