Wakimuona Rais Samia tu, wanayeyuka kama barafu

Na Daniel Mbega

JUMAPILI, Oktoba 15, 2023, Thomas Kongoro, baba mkubwa wa mwanaharakati wa kisiasa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alimuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kongoro aliyasema hayo wakati akimsubiri Rais Samia, ambaye alikuwa ziarani mkoani Singida, kwenye uzinduzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi na Mkalama mkoani humo.

Akionekana kukosoa mwenendo wa Lissu, alisema, wakazi wa Singida hawataki siasa za matusi kwa sababu hazijengi nchi bali wanataka siasa safi zinazojenga hoja kama anavyofanya Rais Samia.

“Tunashukuru sana kwa maendeleo ambayo tumeletewa na Rais Samia, wanachotaka wananchi ni maendeleo siyo maneno ambayo hayana maana yoyote. Rais wetu Samia anajitahidi sana kutupigania Watanzania, hiki kijiji chetu cha Mahambe hatutaki siasa za ubaguzi,” alisema na kuongeza kwamba, Samia ameleta maendeleo siyo katika kijiji chao pekee, bali nchi zima na wananchi wanafurahia amani, upendo na mshikamano uliopo.

Lakini katika kuonyesha kwamba, ngome imara ya Lissu imebomoka, baba yake mdogo aitwaye Jackson Mghwai Muro naye alisema Rais Samia amegusa watu wote kwenye suala la maendeleo.

Alisema ujio wake mkoani Singida ni furaha kubwa kwa wananchi kutokana na uongozi wake kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.

“Hii yote inatokana na busara zake, tunaomba aendelee kuwekeza kwenye elimu, barabara, yote ni maendeleo na leo tupo hapa ili kumpongeza,” alisema.

Mkazi wa Kijiji cha Nyahati, Suleiman Tandu, alisema katika kijiji chao kuna zahanati ambayo Rais Samia alitoa Shs. milioni 154, wanawake wamekuwa wakipata huduma hasa za kujifungua, awali walikuwa wakitembea kilomita 10 kufuata huduma za afya.

Licha ya uwepo wa zahanati, kuna mradi mkubwa wa maji, ambapo zaidi ya kaya 60 zimevuta maji katika majumbani.

“Kwa upande wa elimu, ipo shule ya sekondari Nyahati, madarasa yamejengwa na kukamilika kwa asilimia 100 na wanafunzi wapo wa kutwa na bweni. Hivi karibuni Rais Samia alitoa Shs. milioni 25 za kukamilisha majengo mawili, tuseme nini kwa Mama Samia.

“Kijijini alikozaliwa Tundu Lissu (Mahambe), Rais Samia amepeleka maendeleo bila hiana, madarasa mawili yamekamilika, kuna mradi mkubwa wa maji Matare ulizinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru ambao ulikuwa kitendawili,” alisema.

Kitendo cha baba wawili wa Lissu, wakiongozwa na Mzee wa Kijiji hicho, Suleiman Mohamed, kutangaza hadharani kumuunga mkono Rais Samia kwa kuleta maendeleo makubwa kwenye kijiji chao kinadhihirisha bayana kwamba, ngome ya Lissu aliyokuwa akiitegemea imebomoka rasmi.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kuzibomoa ngome za wapinzani, kwani matukio kama hayo yametokea sehemu mbalimbali nchini alikofanya ziara zake.

Kwa kifupi, kila mahali anakoonekana Rais Samia, wapinzani wanayeyuka kama barafu kwenye jua la jangwani.

Na hawayeyuki tu, bali wanafuata mkondo kwa kumuunga mkono kutokana na utekelezaji wake wa shughuli za maendeleo kwa jamii.

Ni dhahiri kwamba, kwa sasa Rais Samia amekuwa tishio kubwa kwa vyama vya upinzani nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 kutokana na umati mkubwa wa watu anaovutia katika ziara zake za mikoani.

Popote aendapo kwenye ziara zake za mikoani, Rais Samia amekuwa analakiwa na umati mkubwa wa watu na kuwafanya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini kutabiri kuwa Rais Samia atashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kada mbalimbali za wananchi, ikiwemo madereva vijana wa bodaboda, kina Kama Lishe, wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wamekuwa wanajitokeza kwa wingi kupokea Rais Samia kwa umati ambao haujawahi kutokea.

Ingawa bado ni mapema na Rais Samia mwenyewe hajatangaza hadharani kuwa atagombea urais 2025, lakini anaonekana kwa sasa kuwa ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika vyama vyote vya siasa nchini na ni turufu kubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akiwa mkoani Singida, Rais Samia aliwataka Watanzaniakuchagua viongozi sahihi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 ambao ni wazalendo wa kweli huku akiongeza kuwa, matokeo ya uchaguzi huo ndiyo yatatoa taswira ya Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika mwaka 2025.

Aliwataka washiriki wa nafasi mbalimbali za uongozi kuacha kuhubiri chuki, kugawa wananchi inapotokea wameshindwa katika chaguzi.

“Nawasihi wagombea wa nafasi za uongozi, tujitahidi kuepuka makundi, uchaguzi una mkono wa Mungu, ukikosa usilete chuki na kusababisha makundi ya kuwagawa watu.

“Makundi yanachangia mgogoro katika chama chetu, kukwamisha maendeleo na kujenga chuki, tusifike huko, tudumishe amani, upendo na mshikamano,” alisema Rais Samia.

Ametekeleza kwa vitendo

Katika ziara zake za hivi karibuni kwenye mikoa ya kusini na sasa katikati ya Tanzania kwenye mkoa wa Singida, Rais Samia amekuwa akivutia umati mkubwa wa wananchi wenye shauku ya kumuona, huku wakimshangilia.

Umati mkubwa wa maelfu ya watu umekuwa ukijaza viwanja vya mipira, mikutano ya hadhara na hata barabarani Rais Samia anaposimama kuwasalimia wananchi.

Wananchi wengi wameonesha kuvutiwa na uongozi mahiri wa Rais Samia tangu aliposhika madaraka Machi 2021 baada ya kifo cha Rais John Magufuli.

Rais Samia alishika uongozi wakati nchi imekumbwa na janga hatari la COVID-19 na akaonesha ujasiri mkubwa kukabiliana na changamoto hiyo ya dunia huku akiwashangaza watu wengi kwa uongozi wake usiotetereka.

Kwenye uongozi wa Rais Samia, siyo tu aliendeleza bali aliongeza kasi ya miradi yote mikubwa ya maendeleo aliyoikuta chini ya Magufuli, ikiwemo ujenzi wa reli ya SGR, ujenzi wa bwawa la umeme la JNHPP, ununuzi wa ndege za ATCL, ujenzi wa barabara, vivuko na madaraja ikiwemo daraja la Kigongo-Busisi la Mwanza.

Pamoja na yote hayo, Rais Samia ameongeza kasi ya ujenzi wa shule, zahanati, hospitali na miradi ya maji kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu tupate uhuru.

Rais Samia pia ameagiza Serikali yake iwekeze kwenye sekta ya Kilimo kwa kuongeza bajeti maradufu na kuvunja rekodi nchini ili kuwafikia wananchi wa chini.

Zaidi ya hayo, Rais Samia amepanua uga wa demokrasia, uhuru na haki nchini na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa, pamoja na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kasi yake inawatisha wapinzani

Siyo siri, kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na Rais Samia na ukamilishaji wa vipaumbele vikuu sita vilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, imekuwa ni ‘kimbunga’ ambacho wapinzani nchini wameshindwa kukihimili.

Hali hiyo imewafanya wengi wao kushindwa kujenga hoja katika kuikosoa Serikali ama kupinga utekelezaji huo, badala yake wamekuwa wakitumia hoja za nguvu, propaganda hasi, dharau na kejeli katika kukwamisha maendeleo.

Rais Samia amefanikiwa kutekeleza vipaumbele vikuu sita kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kusimamia kwa vitendo Ilani hiyo, akiwa na dhamira ya kuifanya Tanzania iendelee kupaa kiuchumi.

Vipaumbele vikuu sita vinavyoendelea kutekelezwa na Rais Samia ni pamoja na kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Rais Samia anaendelea kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.

Aidha, Rais Samia ameleza mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.

Program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) iliyowakusanya vijana kwenye kilimo cha pamoja cha umwagiliaji ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vikuu sita vinavyotajwa kwenye Ilani.

Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini kwa kujenga shule bora, zahanati, vituo vya afya na hospitali pamoja na kununua vitendanishi na kuongeza ajira katika sekta hizo.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, Serikali zote za CCM zimeendelea kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira zisizopungua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.

Serikali ya Rais Samia imeendelea kujenga mazingira wezeshi kwa asasi za kiraia, kidini na vyombo vya habari kustawi ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa, jambo ambalo wapinzani walikuwa wakilipigia kelele na sasa wamizibwa midomo.

Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha huduma na kulinda haki kwa makundi maalum wakiwemo wanawake, vijana, wazee, watoto na watu wenye ulemavu, ambapo Rais Samia aliamua kuunda wizara maalum ya Maendeleo ya Jamii kushughulikia masuala hayo.

Kwa upande wa kukuza uchumi wa kisasa, serikali imeendelea kujenga na kukuza uchumi shindani hususan kupitia sekta za viwanda na huduma za kiuchumi utakaowezesha ustawi wa wananchi wote.

Kuhusu kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi, serikali ya CCM imejikita kuhakikisha uzalishaji unaongezeka katika mazao ya chakula, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula na lishe bora, na tayari Rais Samia amekwishaagiza kwamba wakulima wasiuze chakula nje ili kujiwekea akiba ya kutosha.

Katika uimarishaji upatikanaji wa huduma bora za Afya, Elimu, Maji, Umeme na Makazi vijijini na mijini, serikali imeongeza kasi ya usambazaji majisafi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini kwa upande wa Tanzania Bara ifikapo mwaka 2025, na zaidi ya asilimia 95 kwa upande wa Zanzibar.

Aidha, inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu ili uweze kuzalisha wataalam mahiri zaidi wenye uwezo katika sayansi, teknolojia, ufundi na nyanja nyingine ambao wanaweza kujiajiri na kuajirika ndani ya nchi na mahali popote duniani.

Kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi ni kipaumbele muhimu ambacho Rais Samia ameahidi kukisimamia kwa kuimarisha na kuhuisha taasisi za utafiti, sayansi, teknolojia na ufundi ili ziweze kubuni nyenzo za kuongeza tija katika sekta za uzalishaji na huduma.

Katika hili alitangaza ufadhili (scholarship) maalum kwa wanafunzi wa kidato cha sita watakaofanya vyema kwenye masomo ya sayansi ambao watagharimiwa elimu yao ya juu.

Kwa upande wa ajira milioni nane, Serikali inaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi ikiwa ni pamoja na utalii.

Katika misingi hiyo, Serikali itawawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali, ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu.

Mafanikio haya, ikiwemo azma ya Serikali kuhakikisha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati inaajiri vijana wengi zaidi wa Kitanzania, yamekuwa mwiba kwa wapinzani nchini ambao sasa wanaweweseka na kupinga kila jambo la maendeleo.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba, kwa utendaji huu wa Serikali, CCM itaendelea kuongoza nchi, kwa sababu inaendelea kuleta ustawi wa Watanzania wote na kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wanawake, vijana, watoto, wazee, pamoja na watu wenye ulemavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *