*Achukizwa siasa za chuki, ubaguzi
*Afurahishwa na kasi ya maendeleo
Na Salha Mohamed, Singida
THOMAS Kongoro ambaye ni baba mkubwa wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amemuahidi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Kongoro aliyasema hayo juzi wakati akimsubiri Rais Dkt. Samia kwenye uzinduzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi na Mkalama mkoani Singida.
Alisema wakazi wa Singida hawataki siasa za matusi kwa sababu hazijengi nchi bali wanatasa siasa safi zinazojenga hoja kama anavyofanya Rais Dkt. Samia.
“Tunashukuru sana kwa mawendeleo ambayo tumeletewa na Rais Dkt. Samia, wanachotaka wananchi ni maendeleo sio maneno ambayo hayana maana yeyote.
“Tunahitaji maendeleo yanayoonekana kwa Rais wetu Dkt. Samia, anajitahidi sana kutupigania Watanzania, hiki kijiji chetu hatutaki siasa za ubaguzi.
Alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuleta maendeleo si katika kijiji chao tu, bali nchi nzima ambapo wananchi wanafurahia amani, upendo na mshikamano uliopo.
“Mahambe kwa ahadi tulizopewa, tunaamini hata maji masafi tutayapata, Rais Dkt. Samia, mimi nazungumza kwa moyo safi, sisi tunakushukuru sana,” alieleza.
Alieleza kuwa, awali shule ilikuwa mbovu lakini sasa madarasa mapta yamejengwa mapya, Rais Dkt. Samia ametengeneza barabara hivyo kuchochea maendeleo.
Kwa upande wake, baba mdogo wa Lissu, Jackson Mghwai Muro, alisema Rais Dkt. Samia amegusa watu wote kwenye suala la maendeleo.
Alisema ujio wa Rais Dkt. Samia mkoani Singida ni furaha kubwa kwa wananchi kutokana na uongozi wake kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
“Hii yote inatokana na busara zake, tunaomba aendelee kuwekeza kwenye elimu, barabara, yote ni maendeleo na leo tupo hapa ili kumpongeza,” alisema.
Mkazi wa Kijiji cha Nyahati, Suleiman Tandu, alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa maendeleo yanayopatikana kuanzia ngazi ya kijiji.
Alisema katika kijiji chao kuna zahanati ambayo Rais Dkt. Samia alitoa sh. milioni 154, wanawake wamekuwa wakipata huduma hasa za kujifungua, awali walikuwa wakitumia km 10 kufata huduma za afya.
Licha ya uwepo wa zahanati, kuna mradi mkubwa wa maji, zaidi ya watu 60 wamevuta maji katika nyumba zao.
Akizungumzia elimu, alisema ipo shule ya sekondari Nyahati, madarasa yamejengwa na kukamilika kwa asilimia 100 na wanafunzi wapo wa kutwa, bweni.
“Hivi karibuni Rais Dkt. Samia alitoa sh. milioni 25 za kukamilisha majengo mawili, tuseme nini kwa Mama Samia.
“Alipozaliwa Lissu (Mahambe), Rais Dkt. Samia amepeleka maendeleo bila hiana, madarasa mawili yamekamilika, kuna mradi mkubwa wa maji Matare ulizinduliwa na mbio za Mwenge ambao ulikuwa kitendawili,” alisema.
Alisema Rais Dkt. Samia ni wa mfano wa kuigwa kwa viongozi, amefanya maendeleo makubwa , Wilaya ya Ikungi inakwenda kuneemeka.
Mjumbe wa Kamati ya Shule ya Msingi Mahambe, Chiku Selemani, alisema shule hiyo ndiyo aliyosoma Lissu lakini hajawahi kuifanyia matengenezo licha ya kuwa Mbunge wao kwa miaka tisa Singida Mashariki.
Shule hiyo ina upungufu wa madarasa, miundombinu pamoja na matundu ya vyoo vya wanafunzi na ilianzishwa mwaka 1979.
Alisema kuna fedha ya Mfuko wa Jimbo ambazo zingetumika kuleta mabadiliko jimboni lakini imekuwa tofauti, aliahidi kujenga jiko lakini halijajengwa.
Alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwaona, kwa sasa kuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na kipindi ambacho Lissu alikuwa mbunge.
“Hivi sasa kuna Hospitali ya Wilaya, barabara za kiwango cha lami zinaendelea kujengwa, tunatarajia maendeleo makubwa katika uongozi wa Rais Dkt. Samia,” alisema.
Fatma Hassan kutoka Kata ya Unyahati, alisema anafurahishwa na maendeleo yanayoletwa na Rais Dkt. Samia kwa kujenga kituo cha afya, shule ya sekondari pamoja na Hospitali ya Wilaya.
Alisema amefurahi kupata huduma ya shule karibu na makazi yao, hivi sasa wanafunzi hawasumbuki kwenda umbali mrefu kupata elimu kwa sababu serikali imejanga shule kwenye vijiji vitano vya kata hiyo.
“Kutoka kijiji ninapoishi hadi kufika Ikungi unatumia saa moja na dakika 20 kufika hospitali, kwa sasa natumia dakika kumi tu, tuna maji ya kutosha, tunamtakia mema MamaSamia azidi kutuletea maendeleo,” aliongeza.
Kwa mujibu wa ndugu wa Lissu, wanasema hawajawahi kumpigia kura licha ya undugu walionao kwani amekuwa akifanya siasa za chuki, matusi na kuwagawa watu.