Samia ‘afunguka’ uchaguzi wa 2024

*Utatoa taswira ya Uchaguzi Mkuu 2025

*Avunja ukimya chuki, kugawa wananchi

Na Salha Mohamed, Singida

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzaniakuchagua viongozi sahihi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 ambao ni wazalendo wa kweli.

Alisema matokeo ya uchaguzi huo yatatoa taswira ya Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika mwaka 2025.

Rais Dkt. Samia aliyasema hayo jana katika Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida akiwa katika ziara ya kikazi baada ya kuzindua Daraja la Msingi Mkalama lenye urefu wa mita 100, lililopo wilayani Mkalama.

Aliwataka washiriki wa nafasi mbalimbali za uongozi kuacha kuhubiri chuki, kugawa wananchi inapotokea wameshindwa katika chaguzi.

“Nawasihi wagombea wa nafasi za uongozi, tujitahidi kuepuka makundi, uchaguzi una mkono wa Mungu, ukikosa usilete chuki na kusababisha makundi ya kuwagawa watu,” alisema Rais Dkt. Samia.

“Makundi yanachangia mgogoro katika chama chetu, kukwamisha maendeleo na kujenga chuki, tusifike huko, tudumishe amani, upendo na mshikamano,” alisema

Aliwataka wakulima kuongeza juhudi katika shughuli za kilimo, serikali inahangaika kusaka masoko ya uhakika.

Alisema Serikali imetengeneza mazingira mazuri ya umwagiliaji na kutoa pembejeo ambapo kama soko la nje halipo baada ya wakulima kufanya mavuno, serikali itanunua mazao yote waliyozalisha.

“Limeni kwa wingi masoko yapo, kama soko la nje halipo wakati huo serikali itayanunua mazao yote, kuyahifadhi na baadaye kutafuta masoko,” alisema.

Aliwataka watanzania kila mmoja kwa nafasi yake, kufanya kazi kwa juhudi ili kujiletea maendeleo yake na Taifa kwa ujumla ambapo wananchi waishio mabondeni, wakae kwa tahadhari kutokana na matarajio ya uwepo mvua kubwa za El-Nino kuanzia mwezi huu.

VIONGOZI KUJITATHMINI

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia aliwataka viongozi wa Wilaya ya Mkalama kujitathimini katika utendaji wao wa kazi.

Lengo ni kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka 11 iliyopita.

Alisema ujenzi wa daraja hilo ni kuvutio cha utalii, pia hutumika katika usafiri, usafirishaji kwa kuunganisha mikoa ya kanda ya kati na kanda ya ziwa, kuinganisha nchi na maeneo ya mipakani ikiwemo Sirari, Kenya.

Alieleza kuwa, mbali ya changamoto mbalimbali ambazo Serikali Kuu inazishughulikia ikiwemo sekta ya elimu, halmashauri inapaswa kushughulikia changamoto nyingine ikiwemo ujenzi wa vyoo.

“Upungufu wa walimu shule za msingi ni asilimia 40, sekondari asilimia 26 ambapo changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu, Bajeti ya 2023-24 Serikali itaenda kujikita zaidi kutatua changamoto hiyo,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mohammed Besta, alisema sh. bilioni 11.1 zimetumika kufanikisha ujenzi huo.

Fedha hizo zimetolewa na Serikali na rasirimali watu iliyotumika inatoka nchini ambapo daraja hilo lipo katika barabara ya Mkoa, linaunganisha Singida, Simiyu, Mara pamoja na Arusha.

Ujenzi huo ulisimamiwa na TECU ambayo ni taasisi ya usimamizi wa ujenzi wa madaraja na barabara kutoka TANROADS.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *