TIB yaanika mafanikio, yampa kongole Samia

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam

BENKI ya Maendeleo (TIB) inajivunia kufanya uwekezaji wenye thamani ya sh. bilioni 980.7 ambapo asilimia 93 ya uwekezaji huo umefanyika katika miradi ya sekta binafsi, asilimia saba sekta ya umma, asilimia 80 ni miradi ya muda mrefu zaidi ya miaka mitano.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Lilian Mbassy, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati katika kikao kazi kati ya Wahariri na benki hiyo.

Kikao kazi hicho ni muendelezo wa vikao ambavyo vinaratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa taasisi na mashirika yaliyo chini ya ofisi hiyo, kuelezea majukumu waliyonayo na mafanikio yaliyofikiwa.

Alisema benki hiyo ni mshirika muhimu wa maendeleo ya nchi na Watanzania ikiwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, wa kati kwa maendeleo ya kiuchumi.

Mbassy alisema, TIB ilianzishwa mwaka 1970 ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kujenga Taifa ambalo linalojitegemea kwa kutumia rasirimali zake.

Majukumu ya benki hiyo ni pamoja na kusimamia mifumo kama inavyohitajiwa na serikali, kutoa msaada wa kiufundi na ushauri ili kuwezesha maendeleo ya viwanda, kuendeleza shughuli nyingine za maendeleo kadiri zinavyohitajika ili kuwezesha benki kutumiza malengo ya kuanzishwa kwake.

Akizungumzia matokeo ya uwekezaji wao, Mbassy alisema, miradi 253 inayohusu sekta ya kilimo, usindikaji mazao ya kilimo imekopeshwa fedha na benki hiyo.

Aliongeza kuwa, sh. bilioni 334.7 zimewekezwa katika sekta ya kilimo, mikoa iliyonufaika na uwekezaji wa benki hiyo ni 23, Wilaya 76.

Mbassy alisema, zaidi ya wananchi 10,230 wamepata ajira kupitia sekta ya kilimo ambapo taasisi za fedha 12, SACCOS 78, kampuni 128 zimekopeshwa.

Pia miradi 66 ya maji imekopeshwa zikiwemo mamlaka sita za maji, jumuiya 60 za watumiaji maji vijijini ambapo sh. bilioni 14.9 zimewekezwa katika sekta ya maji na usafi wa mazingira.

Mikoa iliyonufaika na uwekezaji huo ni Dodoma, Singida, Shinyanga, tanga, Mtwara, Iringa, Morogoro na Ruivuma ambapo wananchi 750,000 wamenufaika.

Mbassy alisema, miradi sita imenufaika na uwekezaji wa TIB katika sekta ya nishati ambapo benki hiyo imewekeza sh. bilioni 12.03 katika sekta hiyo, mikoa iliyonufaika ni Dar es Salaam, Iringa, Ruvuma, Pwani na Manyara.

Megawati 8.84 zimezalishwa na kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa, kaya 500,000 zimenufaika na mradi wa UNIDO wa matumizi ya rthano kama chanzo mbadala cha nishati ya kupikia.

Miradi mikubwa ya kimkakati iliyowezeshwa na TIB ni wa TPDC na Wentworth kwenye gesi asilia, TANESCO (mitambo ya usambazaji umeme wa msongo mkubwa Somanga-fungu).

NHC-mradi wa nyumba za makazi, Kagera Sugar Ltd- mradi wa  kiwanda cha sukari, Amiri Hamza Ltd-mradi wa kuchakata kahawa, CATA Mining Co. Ltd-mradi wa uchimbaji na uchenjuaji madini ya dhahabu.

Pia TTCmradi wa uimarishaji miundombinu ya mawasiliano, Pipes Industries Co. Ltd-kuwezesha ujenzi, ununuzi wa mitambo, mashine za kufanyia kazi.

Msagara Investment Company Limited-kuwezesha ununuzi wa laini ya uzalishaji ‘gauze’, pamba maalumu  zinazotumika katika masuala ya upasuaji.

Faida ya uwekezaji uliofanywa ni pamoja na kuongezeka ajira zaidi ya 30,00 kwa Watanzania kutokana na uwekezaji uliofanywa na TIB.

Kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali, kuongeza mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Matrekta 249, ‘Combined harvesters 6’ na ‘Power Tillers’ 137 zimefadhiliwa kupitia dirisha la kilimo, kurahisisha upatikanaji malighafi za viwanda, kuongeza uzalishaji wa bidhaa, kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Pia misaada kwa jamii kama ujenzi wa zahanati, madarasa, miundombinu. Mfano Kagera Sugar imejenga zahanati ya kisasa wilayani Misenyi na Kampuni ya Amir Hamza (T) Ltd  imejenga barabara kwenye eneo la mradi.

Kuhakikisha upatikanaji maji safi na salama kwa kutibu maji kabla ya matumizi, kuboresha afya kutokana na matumizi ya maji safi na salama, kuimarisha ufanisi wa makusanyo ya mauzo ya maji kupitia mfumo wa malipo kabla.

Matumizi ya umeme jua yanayopunguza gharama za uendeshaji miradi ya maji katika jumuiya za maji vijijini kwa kuondoa gharama za kununua dizeli, matengenezo ya mara kwa mara ya genereta, kupunguza gharama za usimamizi.

Kuzijengea jumuiya za maji utamaduni wa kuchangia na kukopa benki ili ziweze kujitegemea na kuipunguzia serikali mzigo wa kuzihudumia.

Huduma nyingine zinazotolewa na TIB ni pamoja na usimamizi wa mifuko ambapo moja ya jukumu lao ni kusimamiafedha za uwakala.

Fedha hizo zinasimamiwa na TIB kwa niaba ya Serikali na mawakala wa miradi ya maendeleo, miradi hiyo haipo kwenye mizania ya Benki (off balance sheet) ambapo hadi Septemba 30, 2023, benki hiyo inasimamia mifuko minane yenye thamani ya sh. bilioni 197.12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *