Na Daniel Mbega,
Kisarawe
JUMATANO, Januari 27, 1960, wakati anazaliwa katika Kijiji cha Kizimkazi, Makunduchi kisiwani Unguja, si baba Mwalimu Suluhu Hassan au mama ambaye alijua kwamba, binti huyo angeweza kuja kuongoza Taifa kubwa kama Tanzania lenye watu takriban milioni 62.
Hapa namzungumzia Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye siyo tu amekuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi za juu za uongozi wa Serikali, kuanzia Makamu wa Rais hadi Rais kamili, lakini ameudhihirishia ulimwengu kwamba yeye ni jasiri, mwenye uwezo wa kuongoza, asiyeyumbishwa na mwenye maono ya maendeleo.
Namtazama Rais Samia kama kiongozi mahiri aliyekuja takriban miaka 410 baada ya mtawala maarufu zaidi katika historia ya Wahausa wa Nigeria ya sasa, Malkia Amina wa Zazzau.
Uwezo wa uongozi wa Rais Samia katika kusimamia maendeleo, kutanua huduma za kijamii, kuchochea uchumi kwa wananchi na kuimarisha uhusiano na mataifa ya kigeni nauchukulia kama ustadi wa Amina wa Zazzau, ingawa Mama Samia yeye hatumii silaha wala hatumii silaha na hateki ngome za adui kutanua himaya yake.
Naomba nimwelezee, japo kwa ufupi huyu Malkia Amina, mwanamke mwenye nguvu na mbinu kali za vita kutoka Ufalme wa Zazzau, ambao kwa sasa unafahamika kama Mji wa Zaria, kaskazini-magharibi mwa Nigeria, katika Jimbo la Kaduna.
Amina alizaliwa mwaka 1533 kwa baba Mfalme Nikatau, mtawala wa 22 wa Zazzau, na mama Malkia Bakwa Turunku. Alikuwa na mdogo wake wa kike aliyeitwa Zaria, ambaye ndiye chanzo cha Mji wa Zazzau kuitwa Zaria mwanzoni mwa Karne ya 20 na watawala wa Kiingereza.
Amina alikulia katika mikono ya babu yake, aliyempenda sana na kuanza kumfundisha utumiaji wa silaha mbalimbali za kivita tangu akiwa mdogo. Akiwa na miaka 16, Amina akaitwa Magajiya (mrithi dhahiri wa Ufalme), na akapewa watumwa wanawake (kuyanga) 40. Tangu utotoni, Amina alikuwa na wachumba kadhaa waliojaribu kumuoa. Jaribio la kukubaliwa lilijumuisha “ofa ya kila siku ya watumwa 10” kutoka Makama na “watumwa 50 wa kiume na watumwa wa kike 50 pamoja na mifuko 50 ya nguo nyeupe na bluu” kutoka Sarkin Kano.
Baada ya kifo cha wazazi wake takriban mwaka 1566, kaka yake Amina, Karami, ndiye akawa Mfalme wa Zazzau. Wakati huo, Amina alikuwa amejipambanua mwenyewe kuwa “shujaa mkuu katika wapanda farasi wa kaka yake” na akapata sifa kubwa kwa ustadi wake wa kijeshi. Bado anaadhimishwa leo katika nyimbo za kitamaduni za sifa za Kihausa kama “Amina binti Nikatau, mwanamke mwenye uwezo kama mwanamume aliyeweza kuwaongoza wanaume vitani.”
Baada ya kifo cha kaka yake mwaka 1576, Amina akatawazwa kuwa Malkia. Zazzau ilikuwa mojawapo ya Majimbo saba ya awali ya Hausa (Hausa Bakwai), mengine yakiwa Daura, Kano, Gobir, Katsina, Rano, na Garun Gabas. Kabla ya Amina kushika kiti cha enzi, Zazzau ilikuwa mojawapo ya majimbo makubwa zaidi kati ya haya. Pia kilikuwa chanzo kikuu cha watumwa ambao wangeuzwa katika soko la watumwa la Kano na Katsina na wafanyabiashara wa Kiarabu.
Kwa miaka 34 Amina alitawala Zazzau na akautanua utawala wake kwa kuwapiga na kuwanyang’anya ardhi wale wote waliojaribu kumchokoza.
Naam. Huyu ndiye Amina wa Zazzau aliyeibuka katika kipindi ambapo kila kitu kiliendeshwa na wanaume. Akaongoza jeshi kubwa lililonyakua maeneo mengi na kuweza kuupanua ufalme wake.
Wengi walimwita: ‘Amina, mwanamke kama mwanaume!’
Hii ni kwa sababu kila kitu alichokifanya kama malkia kilizidi kile walichokifanya watangulizi wake wa kiume. Na sasa jina lake linatumika kuwakilisha nguvu na uwezo wa mwanamke.
Alifungua njia za biashara na inaaminika alianzisha ulimaji wa njugu za kola katika maeneo aliyokuwa akiyadhibiti.
Sultan wa Pili wa Sokoto (Ufalme wa Wafulani katika eneo ambalo sasa ni nchi za Cameroon, Burkina Faso, Niger na Nigeria), Mohammed Bello, ambaye pia alikuwa mtoto wa Usman dan Fodio, mpiganaji maarufu aliyeeneza dini ya Kiislamu, alimuandika kwa mara ya kwanza katika kitabu chake ‘Infaku’l Maisuri’.
Kulingana na kitabu hicho, Amina alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha utawala kama unavyojulikana sasa katika jamii za Hausa, na pia alikuwa na kipaji cha pekee cha uongozi.
Ukimtazama Rais Samia utakubaliana nami kwamba naye anapita katika njia zile zile za Malkia Amina wa Zazzau.
Kwanza, kama nilivyosema awali, Mama Samia ndiye mwanamke wa kwanza tangu Tanzania (Tanganyika) ilipopata Uhuru kuwa Makamu wa Rais na amepanda hadi kuwa rais kamili.
Katika utawala wake tunaona alivyo na uwezo na anafanya mambo mengi kwa umahiri mkubwa kama au zaidi ya wanaume ambavyo wangeweza kufanya.
Mama Samia amewatia ujasiri wanawake ambao sasa wanajiamini. Anazingatia matamko ya kimataifa ya kuwapa nafasi wanawake katika uongozi na ukiangalia kuanzia kwenye Baraza lake la Mawaziri na nafasi mbalimbali za uteuzi wapo wanawake wengi ambao wanafanya vizuri kwenye uongozi kama au kuliko wanaume.
Lakini zaidi tunaona jinsi anavyohamasisha wawekezaji kutoka nje waje wawekeze nchini na kuwarejesha wale waliokuwa wamefunga biashara zao.
Tunaona jinsi anavyojitahidi kuwatafutia fursa za masoko wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania.
Tunaona jinsi anavyoweka utaratibu hata kwa wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) akitaka waende katika maeneo maalum yaliyotengwa, ambayo licha ya kugharimu mabilioni ya fedha, lakini Wamachinga wameyakimbia na badala yake wanapanga bidhaa zao barabarani na kusababisha kero kubwa.
Mama Samia nsiye mwenye mamlaka, kiongozi shupavu, imara, mkakamavu, mweledi, nayewaongoza Watanzania kwa kuzingatia misingi ya haki na demokrasia huku akisisitiza umoja, Amani na mshikamano katika kujenga umoja wa kitaifa.
Awali nilipata shida sana ya kuandika ili kumwelezea Mama Samia. Mara kadhaa nilikuwa naandika, halafu nafuta… naandika, halafu nafuta. Kila wakati nikitafuta pembe nzuri ya kuanzia.
Naamini hata wakati huu nimeandika zaidi ya mara kumi na kufuta, na sina uhakika kama sitafuta tena wakati nitakapoweka nukta baada ya kumaliza kuandika makala haya.
Si kwamba hakuna cha kuandika, La hasha! Kuna mengi ya kuandika kumhusu rais huyu wa tatu mwanamke katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na wa nne barani Afrika baada ya Sylvie Kinigi, Agathe Uwilingiyimana na Ellen Johnson Sirleaf.
Awali Sylvie Ntigashira Kinigi alikuwa Waziri Mkuu wa Burundi kabla ya kukaimu urais kuanzia Oktoba 27, 1993 hadi Februari 5, 1994 alipompisha Cyprien Ntayamirwa, akiwa mwanamke wa kwanza na wa mwisho kushika nyadhifa hizo nchini humo.
Madame Agathe Uwilingiyimana alikuwa Waziri Mkuu wa Rwanda na kaimu rais kutoka Julai 18, 1993 hadi alipouawa Aprili 7, 1994 mwanzoni mwa mauaji ya kimbari.
Ellen Eugenia Johnson-Sirleaf ndiye alikuwa rais wa kuchaguliwa wa kwanza mwanamke barani Afrika wakati aliposhinda kwa mara ya kwanza uchaguzi Januari 16, 2006 kuchukua nafasi ya Gyude Bryant hadi alipompisha mwanasoka nguli George Oppong Weah Januari 22, 2018. Katika uchaguzi wa 1997 alishika nafasi ya pili nyuma ya Charles Taylor.
Rais Samia, katika kipindi cha miaka miwili na miezi sita ya utawala wake amefanya mambo makubwa mengi ya kuwaletea Watanzania maendeleo, kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, kuboresha elimu, afya, miundombinu na mambo mengi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Ukimwacha Amina wa Zazzau, binafsi namweka Rais Samia miongoni mwa machifu wanawake mashujaa waliopata kutokea Afrika.
Kama Malkia Makeda wa Sheba
Ukisoma vitabu vya dini vya Kiyahudi, Kikristo na Kiislamu Malkia wa Sheba anatajwa kwa mapana, ingawa kumekuwa na ngano tofauti kuhusu ni wapi hasa ilipokuwepo Himaya ya Sheba.
Wachache wanasema Sheba inamaanisha kwamba ni Himaya ya Saba ambayo ndiyo Yemen ya sasa.
Lakini ngano zilizotawala na zinazoaminiwa hata leo ni kwamba, Sheba ndiyo Ethiopia ya sasa na Malkia Makeda ndiye mama wa Mfalme wa kwanza wa Ethiopia, Menelik I, wakati huo ikiitwa Himaya ya Solomon (Solomonic Dynasty), na baba yake ni Mfalme Suleiman wa Israel.
Ukweli huu unathibitishwa na harakati kadhaa za kuwarejesha Waethiopia wenye asili ya Uyahudi zilizopewa majina kama Operation Moses na Operation Solomon katika miaka ya 1988 hadi 1991, zikitiliwa nguvu na Sheria ya Kurejea (Law of Return) iliyopitishwa Israel mwaka 1950 kuwapa uhuru Wayahudi wote duniani warejee nchini humo kama wahamiaji.
Waethiopia wanaamini kwamba Makeda alitawala juu ya utawala unaoitwa Saba, na kwamba alikuwa Malkia wa Kibiblia wa Sheba. Wanamrudisha mwanzo wa uongofu wa Uhabeshi kutoka kwa uhuishaji hadi uaminifu wa kimungu; Makeda kwa Kihabeshi inamaanisha “Si hivyo,” kwa sababu malkia aliwaagiza watu wake kwamba “sivyo hivyo ni vizuri kuabudu mungu jua, lakini ni sawa kumwabudu Mungu.”
Malkia Makeda, akiwa binti mdogo na tajiri kweli kweli, alipenda kujifunza hekima ili aweze kuwaongoza watu wake, ndiyo maana aliposikia kuna mfalme mmoja mwenye hekima kuliko wanadamu wote waliowahi kuzaliwa, Mfalme Suleiman, akaamua kwenda Yerusalemu kujifunza, wakati huo alikuwa ametawala Sheba kwa miaka mitano tu.
Alitumia miezi sita huko Yerusalemu jinsi ya kutawala kwa haki na kwa busara kutoka kwa Suleiman, japo mkutano huo ndio ulioleta matunda ya ujauzito na hata akazaliwa Menelik I.
Hekima ndiyo huimarisha ufalme. Tunaona jinsi Mama Samia, baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita, alivyojitahidi kupata ushauri kwa wazee waliomtangulia, kama marais wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa hekima zake binafsi alizojaliwa na Mwenyezi Mungu, pamoja zile alizozipata kwa wazee, tunaona namna anavyoiongoza Tanzania kwa adili na siyo siri kwamba kila mtu anaufurahia utawala wake.
Kama Kimpa Vita
Huyu tunaweza kumwita Mama wa Mapinduzi na Umoja wa Afrika kwa sababu ndiye aliyeanzisha harakati za kidemokrasia huku akipinga utumwa enzi hizo.
Kimpa Vita alijaribu kuunganisha Ufalme wa Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya sasa hadi sehemu ya Angola) kupitia Ukristo wa Kiafrika. Alifanikiwa lakini kwa muda mfupi kwani aliuawa akiwa na miaka 22 tu.
Alifahamika kwa majina kama Dona Beatriz Kimpa Vita, Kimpa Mvita, Tsimpa Vita au Tchimpa Vita. Jina la Beatriz alibatizwa na Watawa wa Kikatoliki.
Alizaliwa mwaka 1684 katika eneo la Mlima Kibangu katika Ufalme wa Congo, eneo ambalo leo hii ni sehemu ya Angola.
Kimpa Vita anasemekana aligeukia maisha ya kiroho baada ya ndoa zake mbili kuishia kwenye talaka. Lakini pia inaripotiwa kuwa alikuwa na maono ya kimiujiza tangu umri mdogo.
Tunaweza kusema Mama Samia anatembea katika nyayo kama hizo za kuhamasisha demokrasia, anawaunganisha Watanzania na anaimarisha uhusiano wa kidiplomasia na jumuiya za kimataifa.
Kama Malkia Tassi Hangbe wa Dahomey
Bahati mbaya ni kwamba, watoto wetu sasa hawafunzwi historia kama tulivyosoma sisi na mengi kati ya mambo ninayoyaandika hapa yanaweza kuwa mageni kwa wengi.
Ufalme wa Dahomey ulikuwa maarufu sana kati ya Karne ya 17 hadi ya 19 katika eneo ambalo linajulikana kama Benin ya leo.
Lakini siri ya ustawi wa ufalme huo ilitokana na kikosi cha mashujaa wanawake kilichoitwa Dahomey Amazons.
Wafalme 15 tofauti walitawala Dahomey, lakini kwa bahati mbaya hakuna rekodi za kumbukumbu zinazotaja majina ya wanawake wa ufalme huo.
Ni ukweli usiopingika kwamba wanawake walichangia sana kuuimarisha ufalme huo, na mwanamke mmoja, Tassi Hangbe, alikuja kutawala.
Tassi Hangbe alikuwa mpiganaji wa kwanza wa Amazons. Huyu alikuwa binti mfalme Houegbadja, mwasisi wa Ufalme wa Dahomey, na pacha wa Mfalme Akaba.
Mnamo mwaka 1708 mfalme Akaba alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu. Tassi Hangbe akateuliwa kama mkuu wa jeshi. Baada ya hapo aliondoka na kwenda kupigana vita. Aliporudi vitani, ndipo akatangazwa rasmi kama Malkia wa Dahomey.
Licha ya kwamba alitawala kwa miaka mitatu pekee, Tassi Hangbe alifanya mengi kuwainua wanawake. Aliwapa jukumu la kuwinda na kutunza mashamba. Kabla ya hapo, kazi zote hizo mbili zilizoeleka kufanywa na wanaume. Pia aliendeleza kilimo, na kusambaza maji ya kunywa bure kwa watu wake wote.
Mara tu baada ya kutawazwa, Tassi Hangbe alihisi kuwa hataweza kufanya kila anachotaka, kwa hivyo aliunda kikosi cha wanawake watupu waliokuwa na ushujaa wa hali ya juu. Wapiganaji hao waliojulikana pia kama Agoodjie kwa lugha ya Fon (jina linalomaanisha kikosi cha mwisho cha ulinzi kabla ya kumfikia malkia), walianza kupewa mafunzo tangu wakiwa watoto.
Na mafunzo hayo yaliyokuwa na ufanisi mkubwa, yaliwajenga na kuwa wapiganaji mashujaa kuliko wanaume wengi.
Wakiwa vitani, wanawake hao hawakuwa na huruma. Na aliyethubutu kutaka kuwapinga alikatwa kichwa.
Tunamfananisha Mama Samia na Tassi Hangbe kwa ushujaa wake na umahiri wake wa uongozi na jinsi anavyowaamini wanawake na kuwapa majukumu – siyo ya kuua na kukata vichwa – bali kuwaletea Watanzania maendeleo.
Kama Malkia Abla Pokou
Abla Pokou alizaliwa mwanzoni mwa karne ya 18. Alikuwa ni mpwa wa kike wa Mfalme Osei Tutu – mwanzilishi mwenza wa Himaya ya Ashanti eneo ambalo ni Ghana hivi sasa. Alipofariki, kulizuka vita vya kuwania kiti cha ufalme. Na Dakon, kaka yake wa pili Abla Pokou ambaye alikuwa mmoja wa warithi wa ufalme huo, aliuliwa. Abla Pokou aliamua kukimbia, akihofia maisha yake na ya familia yake.
Historia inaeleza kuwa, Abla Pokou ni malkia aliyeuongoza msafara wa watu wake kutoka Gold Coast hadi Upper Volta (Ghana na Ivory Coast za sasa). Alianzisha taifa la watu wa Baoule mwaka 1770.
Abla Pokou aliondoka na wale wote waliokuwa watiifu kwa kaka yake Dakon, na ambao hawakutaka kumuona OPokou Ware akichukua ufalme. Aliongoza msafara mkubwa kuelekea eneo ambalo linajulikana sasa kama Ivory Coast.
Kulingana na simulizi tofauti, wakati wakiwa njiani, Malkia Abla Pokou na wafuasi wake walishindwa kuendelea na safari walipofika katika Mto Comoe, ambao ni mpaka kati ya Ghana na Ivyory Coast kama zinavyojulikana sasa.
Mto ulikuwa umefurika maji kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha kwa wingi, na hivyo ilikuwa vigumu kwao kuuvuka.
Malkia Abla Pokou alishauriana na watu wenye busara aliokuwa amefuatana nao kwenye msafara huo, na walimwambia miungu ya mto huo inadai kafara ya mtoto mwenye damu ya kifalme ili waweze kuvuka mto huo. Na hivyo Abla Pokou anadaiwa alimrusha mtoto wake kwenye mto na akamezwa na maji.
Na kulingana na simulizi hizo, miti ya pembezoni mwa mto iliinama na kutengeneza njia mfano wa daraja ili msafara huo uweze kuvuka na kuendelea na safari yao.
Baada ya kuvuka mto, Abla Pokou alipiga mayowe na kusema “Bâ wouli” maneno yanayomaanisha “Mtoto amefariki”. Sentensi hiyo inaaminika huenda ndiyo chimbuko la jina la watu wa Baoule, wanaoishi hivi sasa nchini Ivory Coast.
Malkia Abla Pokou aliishi Namounou katika eneo la Bwake ambalo haliko mbali na kijiji cha Akawa nchini Ivory Coast. Maana ya Namounou ni “Mtunze Mama”. Kijiji hicho kilipewa jina hilo kuwasisitiza watu wanaoishi hapo wamtunze mama yao Abla Pokou.
Kama Binti Mfalme Yennenga
Yennenga hakuwa binti mfalme wa kawaida. Alikuwa ni shujaa wa kivita na mwenye uzoefu mzuri wa kuendesha farasi. Anakumbukwa hadi leo Burkina Faso kutokana na ujasiri wake.
Huyu ndiye aliongoza Himaya ya Mossi, kabila ambalo hadi leo linaunda asilimia 51 ya makabila yote nchini humo. Makabila mengine ni Wafula (8.4%), Wagurma (7%), Wabobo (4.9%), Wagurunsi (4.6%), Wasenufo (4.5%), Walobi (2.4%), Watuareg (1.9%) na Wadioula (0.8%).
Baba yake alikuwa Mfalme Naba Nedega na mama yake Napoko. Wengi wanaamini Binti Mfalme Yennenga alizaliwa kati ya karne ya 11 na 15 na alikuwa mtoto wa kike kipenzi wa Mfalme Nedega aliyetawala Ufalme wa Dagomba, eneo linalojulikana leo kama taifa la Ghana.
Simulizi za kimila nchini Burkina Faso zinasema, Yennenga alikuwa na farasi ambaye alimpenda sana tangu utotoni. Baada ya kujaribu sana, Yennenga alimshawishi baba yake amruhusu kumpanda farasi huyo. Hakikuwa kitu cha kawaida, kwani katika ufalme huo, ni wanaume tu waliokuwa wakiruhusiwa kupanda farasi. Bintimfalme huyo alikuja kuwaonyesha kwamba si tu mwendesha farasi mahiri, bali pia ni shujaa wa kivita.
Alijifungua mtoto wa kiume baada ya kupendana na mwindaji msituni. Mtoto huyo alipewa jina la Ouedraogo (jina analoitwa farasi mwanaume). Walifanya hivyo kwa sababu ni farasi wa Yennenga aliyewakutanisha wapenzi hao wawili. Ouedraogo ni chimbuko la mababu wa watu wa Mossi, kabila kubwa zaidi nchini Burkina Faso.
Kuhusu asili ya mpenzi wake, kuna wanaosema alikuwa ni mwindaji kutoka Mali. Hili linaweza kuelezea kwa nini watu wa Mossi wana asili ya Mali.
Msanii Yili Nooma wa Burkina faso anamuelezea Yennenga kama “Mwanamke shupavu na asiye na woga, Amazon, shujaa ambaye sisi wanawake, tunataka kufanana naye. Kutumia jina la bintimfalme huyo kuiita albamu yangu ya kwanza ilikuwa ni njia ya kusema kwamba, “sisi ndiyo kina Yennenga wa leo”.
Malkia huyu anakumbukwa kupitia tuzo ya “The Golden Stallion of Yennenga”, inayotolewa katika tamasha la sinema Afrika (FESPACO) linalofanyika kila baada ya miaka miwili.
Kuna mji mpya unaojengwa kwa jina la Yennenga, pamoja na timu ya mpira wa miguu ya Ligi Kuu ya Burkina Faso, iitwayo Association Sportive du Faso-Yennenga (ASFA Yennenga). Jina la timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Burkina Faso – Stallions – pia linatokana na farasi huyo wa Yennenga.
Nilitaka nifute na hapa … lakini hapana. Rais Samia ni ‘Malkia wa Kipekee’!
Simu: 0629-299688