Na Daniel Mbega,
Dar es Salaam
ILANI ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 inatamka bayana kwamba, katika miaka mitano ijayo, chama hicho kitahakikisha matarajio ya wananchi katika nyanja zote yanafikiwa.
Ilani hiyo, ambayo maudhui yake yamezingatia Mwelekeo wa Sera za CCM wa 2020-2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020-2050, ndiyo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mazingatio makubwa kwenye Ilani ni fursa na changamoto zinazotokana na mabadiliko mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiteknolojia yanayotokea nchini na duniani, pamoja na madhara ya janga la ugonjwa wa Corona.
Kwenye Ilani hiyo, Serikali ya CCM chini ya Rais Samia inataja vipaumbele vikuu sita kuwa ni Kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa; Kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.
Vipaumbele vingine ni Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi; na Kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini.
Ilani hiyo inasema, serikali za CCM zitachochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi; na Kutengeneza ajira zisizopungua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.
Benki ya Maendeleo TIB, kama taasisi ya umma, inashiriki kwa kiasi kikubwa kuhakikisha malengo na vipaumbele hivyo vya Serikali ya Samia vinatekelezwa kama ilivyokusudiwa.
Aidha, TIB katika utekelezaji huo wa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita, pia imetembea kwenye Malengo 6 kati ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs).
Hayo ni pamoja na Lengo Namba 2 la Kutokomeza Njaa ambapo jumla ya Shs. bilioni 334.7 kiliwekezwa, Lengo Namba 4 la Ubora wa Elimu ambako Shs. bilioni 14.8 ziliwekezwa, mfano kwenye vyuo vya TUDARCO na MUST, Lengo Namba 6 la Maji Safi na Usafi wa Mazingira ambako kiasi cha Shs. bilioni 14.9 kiliwekezwa.
Malengo mengine ni Lengo Namba 7 la Nishati Safi na ya Gharama Nafuu ambapo Shs. bilioni 12 ziliwekezwa, mfano miradi ya TANESCO TEDAP & TREEP, Lengo Namba 8 kuhusu Ajira na Ukuaji wa Uchumi ambako Shs. bilioni 558.9 ziliwekezwa hata kwenye sekta za utalii usafiri na mawasiliano, na mwisho ni Lengo Namba 11 la Miji na Jamii Endelevu lililoshuhudia Shs. bilioni 45.3 zikiwekezwa, hususan katika miradi ya NHC.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Lilian Mbassy, aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana Jumatatu, Oktoba 16, 2023 kwamba, TIB inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kwa weledi ili kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita, iliyodhamiria kuifungua nchi katika uchumi wa Dunia kupitia kuboresha mazingira ya uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu mikubwa ili kuharakisha mtiririko mzuri wa uwekezaji wa moja kwa moja wa nje (FDI) na uwekezaji wa moja kwa moja wa ndani (DDI) kwa jamii na ustawi wa uchumi wa Tanzania.
Mbassy anaeleza kwamba, wanafanya hivyo kwa kuzingatia kwamba, majukumu ya msingi ya Benki kwa mujibu wa sheria iliyoianzisha ni kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kutoa msaada wa kiufundi na ushauri kwa ajili ya kuwezesha maendeleo ya viwanda, kusimamia mifuko maalumu kama itakavyohitajiwa na serikali, na kuendesha shughuli nyingine za kimaendeleo kadiri itakavyoonekana zinahitajiwa ili kuwezesha benki kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
Anaeleza kwamba, hadi kufikia Septemba 30, 2023, Benki hiyo ilikuwa imewekeza jumla ya Shs. 980,693,206,058.64 (Shs. bilioni 980.7) ambapo 93% ya miradi ni ya sekta binafsi na 7% huku asilimia 80% ya mradi kiwa ni ya muda mrefu wa zaidi ya miaka 5.
“Mikopo iliyotolewa na TIB kwa kipindi hicho jumla yake ni Shs. 980,693,206,058.64 katika sekta mbalimbali,” anasema Mbassy.
Katika kuenenda na kasi pamoja na falsafa ya Rais Samia, Mbassy anasema, Sekta ya Kilimo na Usindikaji ndiyo imechukua fedha nyingi zaidi, ambazo ni jumla ya Shs. 334,686,590,203.02 sawa na asilimia 34.13.
Anasema, matokeo ya uwekezaji kwenye Sekta ya Kilimo yameshuhudia jumla ya miradi 253 ikikopeshwa fedha hizo ambapo mikoa 23 na wilaya 76 zilinufaika na uwekezaji.
“Zaidi ya wananchi 10,230 wamepata ajira katika sekta ya kilimo, lakini pia taasisi za kifedha 12, SACCOS 78 na kampuni 128 zimekopeshwa,” anasema Mbassy.
Sekta iliyofuatia kwa kukopeshwa fedha nyingi ni Madini na Uchakataji iliyshuhudia jumla ya Shs. 205,393,327,423.00 (20.93%), wakati sekta ya Utalii ilipata Shs. 154,959,105,050.00 (15.80%), Viwanda Shs. 119,297,697,881.00 (12.16%), Huduma nyingine Shs. 70,049,373,967.62 (7.14%), na Ujenzi na Majengo Shs. 45,338,526,515.00 (4.62%).
Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira ilikopeshwa Shs. 14,898,020,726.00 (1.52%) ambapo jumla ya miradi ya maji 66 imekopeshwa (Mamlaka za Maji – 6 na Jumuiya za Watumia Maji Vijijini – 60).
Kiasi hicho cha Shs. bilioni 14.9 kimeinufaisha mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Tanga, Mtwara, Iringa, Morogoro na Ruvuma ambapo jumla ya wananchi 750,000 wamenufaika na miradi ya maji, huku kilomita 157 za mtandao wa usambazaji wa maji zikijengwa.
Kwa upande mwingine, miradi ya Umeme na Nishati ilikopeshwa Shs. 12,037,600,747.00 (sawa na 1.23%), ambapo jumla ya miradi sita (6) imetekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Ruvuma, Pwani na Manyara.
“Jumla ya Megawati 8.84 zimezalishwa na kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Lakini pia kaya 500,000 zimenufaika na Mradi wa UNIDO wa matumizi ya ethano kama chanzo mbadala cha nishati safi ya kupikia,” anasema Mbassy.
Mbassy anasema kwamba, sekta nyingine zilizopata mikopo hiyo ni Elimu Shs. 14,823,606,477.00 (1.51%), Usafiri na Mawasiliano Shs. 5,488,118,156.00 (0.56%), na Washirika wa Kifedha Shs. 3,721,238,913.00 sawa na asilimia 0.38.
Anafafanua kwamba, miradi mikubwa ya kimkakati iliyowezeshwa na TIB ni pamoja na TPDC na Wentworth – miradi kwenye gesi asilia, TANESCO – mitambo ya usambazaji wa umeme wa msongo mkubwa (Somanga-fungu), NHC – mradi wa nyumba za makazi, Kagera Sugar Ltd – mradi wa kiwanda cha sukari, Amiri Hamza Ltd – mradi wa kuchakata kahawa, CATA Mining Co. Ltd – mradi wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu, TTC – mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya mawasiliano, Pipes Industries Co. Ltd – kuwezesha ujenzi na ununuzi wa mitambo na mashine za kufanyia kazi, na Msagara Investment Company Limited – kuwezesha ununuzi wa laini ya uzalishaji wa ‘gauze’ pamba maalumu zinazotumika katika masuala ya upasuaji.
Kimsingi, Benki ya TIB ambayo ilianzishwa mwaka 1970, ni kongwe na ina dhima kubwa katika kusukuma mbele maendeleo kwa kuzingatia kwamba ndiyo inayopaswa kutoa mitaji hasa katika uwekezaji.