Umati mkubwa wa Samia tishio kwa upinzani 2025

Na Mwandishi Wetu, Singida

RAIS Samia Suluhu Hassan ameibuka kuwa tishio kubwa kwa vyama vya upinzani nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa 2025 kutokana na umati mkubwa wa watu anaovutia katika ziara zake za mikoani.

Popote aendapo kwenye ziara zake za mikoani, Rais Samia amekuwa analakiwa na umati mkubwa wa watu na kuwafanya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini kutabiri kuwa Rais Samia atashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2025.

Kada mbalimbali za wananchi, ikiwemo madereva vijana wa bodaboda, kina Kama Lishe, wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wamekuwa wanajitokeza kwa wingi kupokea Rais Samia kwa umati ambao haujawahi kutokea.

Ingawa bado ni mapema na Rais Samia mwenyewe hajatangaza hadharani kuwa atagombea urais 2025, lakini Rais Samia anaonekana kwa sasa kuwa ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika vyama vyote vya siasa nchini na ni turufu kubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Katika ziara zake za hivi karibuni kwenye mikoa ya kusini na sasa katikati ya Tanzania kwenye mkoa wa Singida, Rais Samia amekuwa anavutia umati mkubwa wa wananchi wenye shauku ya kumuona, huku wakimshangilia.

Umati mkubwa wa maelfu ya watu umekuwa ukijaza viwanja vya mipira, mikutano ya hadhara na hata barabarani Rais Samia anaposimama kuwasalimia wananchi.

Akiwa mkoani Singida jana ambayo zamani ilikuwa ni ngome ya Tundu Lissu wa Chadema, Rais Samia amepokelewa na maelfu ya wananchi katika kijii anachotokea Lissu, kwenye kata ya Mahambe.

Wananchi hao waliongozwa na Suleiman Mohamed, Mzee wa kijiji anachotokea Lissu, Jackson Mghwai Muro, Baba Mdogo wa Lissu na Thomas Kongoro, Baba Mkubwa wa Lissu.

Wazee hao walitangaza hadharani kumuunga mkono Rais Samia kwa kuleta maendeleo makubwa kwenye kjiji chao tangu alipoingia madarakani na kumkemea mtoto wao Tundu Lissu kwa kufanya siasa za mfarakano na kutumia lugha za matusi na kejeli dhidi ya viongozi wa nchi, kinyume na utamaduni wa Tanzania.

Wananchi wengi wameonesha kuvutiwa na uongozi mahiri wa Rais Samia tangu aliposhika madaraka Machi 2021 baada ya kifo cha Rais John Magufuli.

Akiwa Rais wa kwanza mwanamke wa Afrika Mashariki, Rais Samia ameliongoza taifa kwa ushupavu mkubwa kwenye kipindi cha mpito baada ya kutokea kifo cha Rais wa kwanza nchini akiwa madarakani.

Pia, Rais Samia alishika uongozi wakati nchi imekumbwa na janga hatari la COVID-19 na akaonesha ujasiri mkubwa kukabiliana na changamoto hiyo ya dunia huku akiwashangaza watu wengi kwa uongozi wake usiotetereka.

Kwenye uongozi wa Rais Samia, siyo tu aliendeleza bali aliongeza kasi ya miradi yote mikubwa ya maendeleo aliyoikuta chini ya Magufuli, ikiwemo ujenzi wa reli ya SGR, ujenzi wa bwawa la umeme la JNHPP, ununuzi wa ndege za ATCL, ujenzi wa barabara, vivuko na madaraja ikiwemo daraja la Kigongo-Busisi la Mwanza.

Pamoja na yote hayo, Rais Samia ameongeza kasi ya ujenzi wa shule, zahanati, hospitali na miradi ya maji kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu tupate uhuru.

Rais Samia pia ameagiza Serikali yake iwekeze kwenye sekta ya Kilimo kwa kuongeza bajeti maradufu na kuvunja rekodi nchini ili kuwafikia wananchi wa chini.

Zaidi ya hayo, Rais Samia amepanua uwanja wa demokrasia, uhuru na haki nchini na kuimarisha mahusiano ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa, pamoja na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Alipoingia tu madarakani, Rais Samia aliagiza kuwa Serikali ikamilishe majadiliano na wawekezaji wa nje ambao wanapanga kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata gesi asilia (LNG) mkoani Lindi, mradi ambao utaingiza uwekezaji kutoka nje wa zaidi ya shilingi trilioni 100.

“Kwa kweli kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2025, sisi wapinzani tumekubali yaishe. Rais Samia hana mshindani, atashinda kwa kishindo kutokana na kuwekeza pesa nyingi za serikali kwenye sekta zinazowagusa wananchi moja kwa moja kama elimu, afya, maji, umeme na miundombinu. Sisi upinzani tunajipanga kwa 2030, kwani utafiti wetu wa ndani unaonesha kuwa Rais Samia atashinda kwa kishindo 2025,” alisema kiongozi mmoja wa Chadema mkoani Singida kwa sharti la kutotajwa jina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *