Samia azindua shule 302 za Msingi, Sekondari

*Ni kupitia mradi wa Boost, Sequip

*Zimegharimu bil. 230/-, asema…

Na Waandishi Wetu, Dar na Singida

RAIS Dkt, Samia Suluhu Hassan, jana Jumapili, Oktoba 15, 2023 amefungua Shule ya Msingi Imbele, Sekondari Mwanamwema mkoani Singida kwa niaba ya shule mpya 302 zilizojengwa nchi nzima.

Shule hizo zimejengwa kupitia Mradi wa Uhimarishaji Ufundishaji na Ujifunzaji (BOOST) pamoja na Mradi wa Kuimalisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambayo imegharimu sh. bilioni 230.

Baada ya uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka wototo shule ili waweze kutimiza ndoto zao.

Rais Dkt. Samia alizindua shule hizo jana wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Singida akitokea Manyara na kusema Serikali imedhamiria kuboresha elimu na kumuandaa mtoto kuanzia awali hadi elimu ya juu.

Shule ya Msingi Imbele ipo Manispaa ya Singida na Sekondari ya Mwanamwema ipo Halmashauri ya Singida.

Akizungumza na wananchi baada ya uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia alisema shule hizo zimejengwa Tanzania nzima, kuwataka wazazi kuwasomesha watoto wao, kuhakikisha wanakwenda shuleni.

“Tulianza kujenga madarasa hayo kuanzia elimu ya awali, tunataka kumuandaa mtoto akiwa na miaka mitatu hadi minne, ombi langu kwa wazazi wenzangu, hakikisheni watoto wanakwenda shule,” alisema Rais Dkt. Samia.

Aliongeza kuwa, amefurahishwa na watoto wa Shule ya Msingi Imbele wakati wakimuimbia nyimbo, wakitambua matunda ya ujenzi wa shule hizo kwani zitawanufaisha.

Alieleza kuwa, shule na miradi hiyo ni ya Watanzania wote hivyo inatakiwa kulindwa na kutunza ili iendelee kuwanufaisha watoto ambao watasoma katika shule hizo.

Awali akisoma taarifa ya miradi hiyo, Ofisa Elimu Mkoa wa Singida, Dkt. Elipidius Baganda, alisema ujenzi wa miradi hiyo umekamilika kwa asilimia 100, halmashauri  za Wilaya zote mkoani humo kila moja ilipokea sh. milioni 493.6.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu alisema shule hizo zimepunguza utoro kwa wanafunzi kwa sababu wako jirani nazo.

Awali walikuwa wakitembea umbali mrefu na kutumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hizo.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia aliwapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa kulima na kupata mafuno, chakula cha kutosha ambapo mbaazi, mahindi, alizeti zililimwa kwa wingi.

Alisema Singida haipo kwenye mikoa inayosumbua kwenye suala la lishe bora.

Rais Dkt. Samia aliendelea na ziara yake kwa kukagua barabara yenye urefu wa kilometa 59.9 inayotoka Mkiwa, Itigi hadi Nolanga, mkoani Mbeya.

Pia alifungua Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi na Mkalama na kusema serikali itajenga barabara ya km 10 kwa kiwango cha lami itakayogharimu sh. bilioni 67.2 na dola za Marekani milioni 1.01.

Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Makongorosi hadi Mkiwa yenye km 413 ambayo inaunganisha na Uhororoba wa Tanzania na Zambia.

Alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa Mkoa wa Singida, Mbeya na Tabora ambazo zitaunganisha kanda mbalimbali na Ukanda wa SADC.

Kukamilika kwa barabara hii kutachochea shughuli za uzalishaji, biashara kwa kurahisisha usafiri, usafirishaji wa bidhaa za kilimo, madini, misitu.

Alisema Serikali imejidhatiti kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja nchini kote ambapo miradi mingi imekamilika ikiwemo Daraja la Sibiti lenye mita 82, Manyoni Itigi-Chaya km 85.

Pia Tabora-Nyahuya-Chaya km166.5 , Tabora-Koga- Mpanda km 360, Nzega-Tabora km 116, Tabora-Urambo km 87, Dodoma-Mayamaya-Mela km 47.  

Alisema maendeleo ni hatua inayotegemea uwepo wa rasilimali fedha inayohitaji hatua nyingine zaidi ndiyo maana changamoto zinashindwa kuisha.

Aliwahakikishia wananchi kuwa, serikali imejizatiti kutekeleza maendeleo yatakayokwamua wananchi.

Aliongeza kuwa, Wilaya ya Manyoni ina changamoto ya umeme, serikali imetenga sh. bilioni 32 kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo (sub-station) Manyoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *