Hotuba ya Nyerere kwa Wazee wa Dar Novemba 5, 1985 baada ya kung’atuka

Na Daniel Mbega
MNAMO Novemba 5, 1985, siku tisa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu (Jumapili Oktoba 27, 1985) uliomweka madarakani Rais wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikutana na Wazee wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee kuagana nao, na kuwaaga rasmi Watanzania baada ya kung’atuka.
Hiyo ilihitimisha uongozi wake wa miaka takriban 23 akiwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimsingi, Mwalimu Nyerere alikuwa amedhamiria kung’atuka baada ya mwaka 1980 alipochaguliwa na mkutano mkuu maalumu wa CCM uliokutana Alhamisi Septemba 25, 1980, kuwa mgombea pekee wa kiti cha Rais katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 26 mwaka huo.
Wakati huo aliweka bayana kwamba huo ndiyo ungekuwa uchaguzi wake wa mwisho hata kama wangependekeza tena jina lake.
Hapa nimewaletea hotuba yake kwa Wazee wa Dar es Salaam, Novemba 5, 1985:
“Mimi nimeanza siasa na Wazee wa Dar es Salaam; na Wazee wa Tanzania. Nimeanza nao mapema sana; mapema kweli.
Nilirudi kutoka masomoni, Uingereza Oktoba 1952 – miaka 33 nyuma. Wakati huo nikiwa kijana mdogo wa miaka thelathini na kidogo hivi.
Niliporudi nikakubaliana na wamisionari hapo Pugu (sekondari), nifundishe shuleni kwao. Lakini nikiwa shuleni – Chuo Kikuu – nilijua. Niliishaamua kwamba maisha yangu yatakuwa ya siasa.
Niliamua hivyo: Nitafundisha kwa muda wa miaka mitatu, nione hali inavyokwenda na kuzoeana na wenzangu kabla ya kuanza maisha ya siasa.
Niliporejea nchini hapo Oktoba, nikaenda Butiama.
Januari nikarudi Dar es Salaam. Nikaanza kazi.
Nikataka kujua habari za African Association.
Mzee Mwangosi anakumbuka. Yeye ndiye aliniambia habari za African Association. Aliisha niambia habari hizo tangu nikiwa Makerere – Chuo Kikuu – nikiwa mwanafunzi.
Pale, mimi na wanafunzi wenzangu tulikuwa tumeanzisha chama kinachoitwa Tanganyika African Welfare Association (TAWA) cha wanafunzi wa Tanganyika; mimi nikiwa katibu wao. Hapa tukaona mambo yanakwenda vizuri kidogo.
Tukaona kwanini TAWA iwe ya wanafunzi peke yao na siyo Tanganyika nzima.
Kwa hiyo nikawaandikia baadhi ya watu Tanganyika. Nikasema, jamani ee, tumeanzisha chama, kwanini msianzishe huko matawi ya chama hicho?
Ndugu Mwangosi akapata barua hiyo. Alikuwa miongoni mwa waliopata barua hiyo.
Akaniandikia – nikiwa Makerere – akasema: “Wewe kwanini unataka kuanzisha chama kipya? Kipo chama. Kipo chama cha TAA (Tanganyika African Association).
“Kwa hiyo la maana siyo kuanzisha matawi, maana chama kipo na matawi yameenea; la maana ni kwamba hicho chama chenu mfute, na muanzishe tawi la Tanganyika African Association.”
Hivyo ndivyo tulivyofanya.
Kwa hiyo mimi nikawa katibu wa katawi ka TAA hapo Makerere.
Niliporudi Tabora na kuanza kufundisha pale St. Marys (sasa inaitwa Sekondari ya Milambo) nikachaguliwa katibu wa TAA wa jimbo ambalo makao yake makuu yalikuwa Tabora.
Ulipofanyika mkutano wa TAA mjini Dar es Salaam, nilihudhuria nikiwa mjumbe kutoka Tabora.
Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association.
Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA.
Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam.
Nikauliza nani wanaongoza TAA? Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.
Nilipelekwa na Kasela Bantu – ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano).
Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo.
Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation).
Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.
Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari.
Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Arnautoglo.
Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa Rais wao – wa TAA.
Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee.
Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo, Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.
Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni.
Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA.
Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.
Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina Abdul Sykes.
Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).
Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi.
Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.
Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana.
Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abbas Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.
Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: “Wazee na Ndugu zangu!”
Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo!
Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.
Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi.
Akina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.
Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.
Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu.
Huko wazee walinipokea na kunielewa.
Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima.
Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.
Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: “Unatafuta nini?”
Nikawaambia natafuta uhuru.
Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari.
Tulifanya mkutano wa makini kweli.
Wakauliza: “Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?”
Tulielezana.
Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.
Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi.
Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organization – UNO) umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile.
Sisi siyo koloni lao. Wamepewa dhamana tu.
Kwa hiyo nikawaambia wazee, hakuna haja ya kumwaga damu. Tuwaseme tu!
Tuwashitaki kwa waliowaleta hapa kwamba hawafanyi kazi yao; wamesahau kabisa!
Wazee wakauliza: “Eh, inawezekana?”
Nikasema inawezekana.
Kazi yetu ya kwanza ilikuwa kuwaambia watu kwamba uwezekano wa kujitawala upo. Hilo lilikuwa la kwanza.
Wazee walijua maana ya kujitawala. Walitamani kujitawala, lakini hawakujua waanzie wapi.
Vijana hawakuwa na habari kwamba kujitawala kunawezekana.
Kwa hiyo kwa wazee sikuwa na matatizo.
Wao hawakuwa na kazi; hawakumwogopa Mwingereza.
Hawakuogopa kufukuzwa kazi. Baadhi walikuwa wafanyabiashara.
Mzee John Rupia alikuwa mfanyabiashara na kaidi kidogo.
Aliwahi kutishwa na kunyang’anywa leseni yake ya biashara.
Akaambiwa akiendelea kushirikiana na kijana mwendawazimu (Julius Nyerere), atanyang’anywa leseni moja kwa moja.
Rupia aliwajibu: “Potelea mbali!”
Nasema yote haya ikiwa njia ya kutoa shukrani kwa wazee na imani yao kwa vijana wakati huo.
Imani hujenga imani. Na mambo haya makubwa ya nchi, kama hayana baraka za wazee hayaendi. Magumu sana.
Wanasema ngoma ya watoto haikeshi!
Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani. Tangu awali kabisa.
Siku moja, Dosa akanifuata Magomeni.
Akasema: “Leo wazee wanakutaka”.
Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku.
Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda.
Nikakuta wazee wameshakaa; wameniita kijana wao kuniombea dua.
Mimi Mkristo, wao Waislamu watupu.
Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.
Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka.
Zilipomalizika zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee – za jadi.
Walikuwa na beberu la mbuzi. Wamechimba shimo.
Wakaniambia “Simama!” Nikasimama.
Beberu akachinjwa, huku anaambiwa, “Twainingi (Twining) umekwisha!” (Edward Twining alikuwa Gavana wakati huo).
Ndipo nikaambiwa: “Tambuka!”
Nikavuka lile shimo.
Hapo nikaambiwa na wazee: “Basi nenda zako; tangu leo Twainingi amekwisha!”
Sasa mimi Mkristo; hao Waislamu. Na mimi mkorofi-korofi katika mambo haya (ya kutambika).
Lakini tulikuwa tunaelewana na wazee wangu hao.
Kwa hiyo nilitambuka pale na kuambiwa: “Nenda nyumbani salama. Twaining hawezi tena!”
Wazee wangu wengine wanakumbuka tulikuwa tunakwenda Bagamoyo. Kwenye makaburi kule (ya Kaole)! Tunapiga dua huko kwenye makaburi na wazee wangu.
Baadhi yetu mtakumbuka safari moja jamaa wa Kenya, hawa akina Tom Mboya walishitakiwa.
Tukasema tuwasaidie. Tuwasaidie vipi?
Tukasema tufunge. Tukaomba nchi nzima kufunga siku hiyo.
Tufunge! Tukafunga. Hakuna kula.
Na siku ya kufunga tulikuwa na mkutano Bagamoyo. Tukaenda huko.
Tukafanya mkutano hadi saa 12 jioni.
Baada ya mkutano tukaenda nyumbani kwa Mzee Mohamed Ramia.
Hapa ndipo tulikuwa tumefikia. Mimi nikamuuliza mzee: Sheikh, una Aspro?
Akajibu: Kwa nini unataka Aspro?
Nikajibu kuwa kichwa kinaniuma kwelikweli.
Akasema subiri.
Tulisubiri hadi saa ya kufuturu. Tukafuturu vizuri.
Mzee Ramia akaniuliza: bado unataka Aspro?
Nikajibu kichwa sasa hakiumi.
Kumbe ilikuwa njaa.
Nawaelezeni haya kwa sababu huko tulikotoka, tulishikamana sana.
Tulishirikiana sana na wazee.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *