Ziara ya India yaleta neema

• Mauzo ya mbaazi kufikia Shs. bilioni 450
• Zao la Korosho nalo lapata soko kubwa
• Tanzania sasa kutengeneza matrekta
• Huduma za kibingwa za afya zaja

Na Mwandishi Wetu,
New Delhi
RAIS Samia Suluhu Hassan jana alihitimisha ziara yake nchini India huku matunda ya safari hiyo yakianza kufahamika.
Ziara ya Samia nchini India ilifanikiwa kupandisha hadhi ya uhusiano baina ya nchi hizo mbili kufikia kiwango cha uhusiano wa kimkakati na hatua hiyo imefungua ushirikiano na fursa kubwa zaidi kibiashara.
Baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Tanzania walizungumza na waandishi wa habari saa chache baada ya kukamilika kwa ziara na kueleza nini hasa Watanzania wamepata.
Kabla ya kuanza kwa ziara, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, alisema serikali inakwenda kujadiliana na India kuhusu suala la biashara ya uhakika ya mbaazi kwa wakulima wa Tanzania na jana Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alitoa habari njema.
Bashe alisema, Tanzania imeishawishi na kukubaliwa na India kuiuzia mbaazi kwa wastani wa tani 200,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo.
Ingawa India ni wateja wakubwa wa mbaazi, soko lilikuwa halitabiriki kwa kupanda na kushuka, lakini kwa makubaliano haya, wakulima wa mbaazi watakuwa na uhakika wa soko.
“Kwa sasa, bei ya mbaazi ni wastani wa dola moja ya Marekani kwa kilo. Kwa bei hiyo, hapa tunaongelea biashara ya thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 450 kwa mwaka,” alisema Bashe.
Eneo lingine la kilimo ambalo Bashe alisema Tanzania itanufaika ni lile la matrekta ya kilimo ambapo kampuni ya Mahindra imekubali kujenga kiwanda cha matrekta kitakachokuwa na uwezo wa kutengeneza mpaka matrekta 2,000 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Bashe, tayari upembuzi yakinifu wa jambo hilo umeanza na kwamba kama Mahindra watashindwa, kuna kampuni nyingine iko tayari kufanya kazi hiyo.
Mafanikio mengine kwenye sekta ya kilimo kutokana na ziara hiyo yapo katika zao la korosho ambapo uamuzi muhimu umefanyika.
“India ina sheria inayotoza kodi ya asilimia 35 kwa korosho iliyobanguliwa. Sasa kuna kiwanda tumefungua cha kubangua korosho na tumekubaliana ile itakayotoka kwenye kiwanja hicho haitakuwa inatozwa kodi hiyo,” alisema.
Katika sekta ya afya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, John Jingu, alisema serikali hizo zimekubaliana kufungua kituo cha huduma za kibingwa za upandikizaji wa figo na ini hapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *