Samia atunukiwa PhD ya heshima India

Na Mwandishi Wetu,

New Delhi, India

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mwanamke wa kwanza kutunikiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (PhD) na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na kuitoa shahada hiyo kwa watoto hususan wa kike wanaoishi katika mazingira magumu nchini Tanzania.

Akiipokea Shahada hiyo jana Jumanne, Oktoba 10, 2023 jijini New Delhi, ambayo ni ya kwanza kwake kutoka ugenini, Rais Samia amekishukuru Chuo hicho kwa heshima hiyo kubwa na kusema anaitunuku kwa watoto wa kike wa Tanzania wanaoishi katika mazingira magumu, akiwasihi kutokata tamaa kutokana na mazingira waliyopo na kuitaka jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.

Ameeleza kuwa ameitoa tuzo hiyo kwa watoto hao kutokana na mazingira halisi aliyopitia tangu akiwa shule ya msingi hadi kufikia nafasi aliyonayo nayo sasa.

“Mimi ni matokeo ya jozi nyingi za macho na mikono ya watu walioona uwezo ndani yangu wakanilea na kunishika mkono,” alisisitiza Rais Samia.

Pia alisema anawashukuru watu mbalimbali wakiwemo wazazi wake, familia, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa mchango wao uliomwezesha kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.

“Shahada hii inanikumbusha mbali nikiwa mtoto mdogo nikienda shule katika kijiji nilichozaliwa cha Kizimkazi huko Unguja, Zanzibar, huku mama yangu akiwa ni mama wa nyumbani na baba mwalimu.

“Nawashukuru kwa kunipatia muda ulioniwezesha kufikia ndoto zangu za elimu, siasa na hatimaye kufikia nafasi niliyo nayo sasa” amesema.

Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (JNU) kimempa Rais Samia shahada hiyo ya heshima kwa kutambua mchango wake katika kuchochea maendeleo ya watu nchini Tanzania.

Mara ya kwanza alitunukiwa udaktari wa heshima Novemba 30, 2022 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akitangaza kumtunuku Rais Samia shahada hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, Santishree Dhulipudi Pandit amesema: “Kwa mamlaka niliyopewa mimi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru, ni heshima kwangu kumtunuku udaktari wa heshima (Honoris Causa) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, sasa Dk Samia Suluhu Hassan kwa uhusiano wa Tanzania – India na uhusiano wa India – Afrika.”

Baada ya kutangaza kumtunuku shahada hiyo, Pandit alimkabidhi Rais Samia cheti, nishani na vazi maalumu kama ishara ya kumtunuku udaktari wa heshima kiongozi huyo ambaye ndiyo mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania.

Pandit alisema mwaka 1995, chuo hicho kilimtunuku Mwalimu Julius Nyerere udaktari wa heshima, hivyo, Rais Samia amekuwa kiongozi wa pili wa Tanzania kutunukiwa hehima hiyo na chuo hicho.

“Chuo chetu kimetoa washindi wawili wa Tuzo za Nobel na wote ni katika uchumi. Pia, chuo hiki kipo katika nafasi 10 bora ya vyuo vikuu bora duniani katika masomo matano,” alisema makamu mkuu wa chuo.

Pandit alisema Chuo hicho kimemtunuku Rais Samia shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo ya udaktari wa heshima, Rais Samia alikishukuru Chuo cha Jawahalal Nehru kwa kumtunukia shahada hiyo akieleza kwamba hiyo imeongeza kitu katika historia yake.

Alisema siyo mara ya kwanza kwenda India, alikwenda kwa mara ya kwanza mwaka 1998 alipokuwa akisoma katika Chuo cha Teknolojia na Utawala cha Hyderabad, lakini amerudi tena nchini humo akiwa kama Rais wa Tanzania.

“Mmenibadilisha kama familia na kunitunuku shahada ya heshima (honoris causa), sasa nimesimama hapa kama mmoja wa familia ya Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru na siyo kama mgeni wa kawaida. Asanteni sana,” alisema Rais Samia.

Alikishukuru chuo hicho kwa kumpa heshima hiyo na kwamba anaikubali kwa kuwa anathamini uhusiano wa Tanzania na India na pia imeongeza kitu kwenye historia ya maisha yake.

“Shahada hii ya heshima itakuwa daima katika historia yangu kwa kuwa ya kwanza kutolewa kwangu na nchi ya kigeni. Ninayo moja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini hii itakuwa ya kwanza kupewa na chuo cha nje,” amesema Rais Samia.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Subrahmanyam Jaishankar alisema elimu na kujenga uwezo ni moja ya vipaumbele katika uhusiano wa Tanzania na India ambapo zaidi ya Watanzania 5,000 wamepata mafunzo katika taasisi za elimu za India hasa kwenye teknolojia.

Jaishankar alisema wameamua kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT) huko Zanzibar na ratiba kwa ajili ya watahiniwa wa kwanza inaandaliwa na mwezi huu wataanza maomo yao.

“Taasisi hii (IIT) ina fursa ya kuwa kituo kikuu cha elimu ya teknolojia kwa bara zima la Afrika. Ni ishara ya ushirikiano wetu na dunia ya kusini na ni farahi kwangu kuwahi kwenda Zanzibar katika shughuli zangu,” alisema.

Waziri huyo alisisitiza kwamba ziara ya Rais Samia ni ya kwanza kwa kiongozi wa Afrika kuitembelea India tangu Umoja wa Afrika (AU) ilipoingizwa kwenye umoja wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda duniani (G20).

Taarifa kutoka chuoni hapo zinasema kuwa, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, ni viongozi wengine ambao wamewahi kutunukiwa shahada hiyo ni Rais wa Russia Vladmir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan hayati Shinzo Abe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *