Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akijadiliana jambo na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, mara baada ya kuwasili katika Jengo Maalum la kupokelea wageni wa Kitaifa Hyderabad House New Delhi Nchini India Oktoba 9, 2023.
Na Daniel Mbega,
Dar es Salaam
USHIRIKIANO katika Kufanikisha Malengo kwa dhamira ya kuimarisha mbinu za utekelezaji na kuhuisha ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ni Lengo Namba 17 la Umoja wa Mataifa miongoni mwa malengo 17 (SDGs) yaliyopitishwa Septemba 25, 2015.
Wakati wakuu wa nchi 193 walipokutana kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Septemba 25, 2015 ili kupitisha malengo hayo waliazimia mataifa yote yachukue jukumu la utekelezaji katika mpango kabambe wa miaka 15 baada ya kukamilika kwa miaka 15 ya awali (2000-2015) iliyokuwa na Malengo 7 ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).
Licha ya kwamba Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia yalipitishwa 2015, lakini kwa kipindi cha takriban miaka mitano iliyofuata, Lengo la 17 halikuweza kutekelezwa ipasavyo hadi Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021.
Na kwa sasa Rais Samia analitekeleza lengo hili kwa vitendo baada ya kubonyesha kitufe na kuirudisha Tanzania katika uga wa diplomasia ya kimataifa kama ilivyokuwa awali.
Miaka ya nyuma kabisa, kulikuwa na usemi uliovuma sana kimataifa, kwamba: “Wakati Tanzania inapozungumza, ulimwengu mzima unatulia na kusikiliza.”
Hiki ndicho kiwango na ushawishi wa Nguvu Laini ya kidiplomasia ambayo Tanzania imekuwa ikiitumia kwa miaka mingi katika ulingo wa kimataifa tangu kupata Uhuru kutoka kwa Uingereza zaidi ya miongo sita iliyopita.
Ushawishi wa kipekee wa Tanzania wa kijiografia na kisiasa duniani unaweza kufuatiliwa tangu zama za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alilifikisha taifa hilo la Afrika Mashariki katika hadhi ya dunia kama Makkah ya harakati za ukombozi wa Afrika na sauti ya adili duniani kote.
Kuingia madarakani kwa Rais Samia kumefuta kitu ambacho baadhi walikiita ‘Missing in Action’ katika ushirikiano wa ngazi za juu kimataifa, kwani kabla yake, uongozi wa Serikali ilitotangulia ulifuata sera ya mambo ya nje yenye sura ya ndani kwa kiasi fulani.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Rais Samia ameshiriki mikutano isiyo na idadi ya kidiplomasia na kiuchumi katika miji mikubwa, ikiwemo Addis Ababa, Accra, Bujumbura, Cairo, Kampala, Kigali, Kinshasa, Maputo, Washington, New York, Wisconsin, Johannesburg na kufanya ziara nyingi zenye kuakisi Lengo la 17 la Maendeleo la Dunia.
Rais Samia amekuwa mkiongozi mwenye malengo madhubuti hasa kwa kukarabati uhusiano wa zamani na kuimarisha uhusiano uliopo huku akijenga ushirikiano mpyaa.
Katika ipindi hiki kifupi ameongoza kwa ustadi wajumbe wa Tanzania kwenye mikutano yenye nguvu ya juu yenye umuhimu wa kidiplomasia na kiuchumi duniani, hivyo kurejesha kwa ufanisi nafasi ya Tanzania kama nchi yenye nguvu ya kijiografia na kidiplomasia duniani.
Akiwa katika ziara ya siku nne nchini India aliyoianza Oktoba 8 na kutarajia kuhitimisha kesho Jumatano, Oktoba 11, 2023, Rais Samia anaendelea kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kibishara na kiuchumi baina ya Tanzania na India
Kumbukumbu zinanyesha kwamba, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na India ulianza tangu mwaka 1961, ambapo India ilifungua Ubalozi wake mwaka 1961 na Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini India mwaka 1962.
Tanzania na India zinafurahia urafiki na udugu wa kihistoria wa muda mrefu, uliojengwa juu ya dhamana thabiti ya ushirikiano.
Historia ndefu ya biashara ya bidhaa mbalimbali za anasa pamoja na watu waliofanywa watumwa iliweka eneo hili katikati ya mitandao ya kimataifa ya mabara, kuunganisha Pwani ya Uswahilini na Rasi ya Uarabuni, China, India, na Cambodia, miongoni mwa maeneo mengine. Katika karne ya 15, Ulaya – kupitia uvamizi wa Wareno na baadaye Waholanzi na Waingereza – waliingia kwenye eneo hilo la Afrika Mashariki, hasa katika Bahari ya Hindi, kama maharamia na kama watawala wanaotafuta ukiritimba wa biashara kwa sababu Ulaya haikuwa na chochote cha thamani kubwa kufanya biashara.
Kama nilivyosema, uhusiano wa Tanzania na India ni wa karne nyingi zilizopita, wakati biashara kati ya watu wa Pwani ya Waswahili (pamoja na Zanzibar na Tanganyika) na Pwani ya Mto Mandovi ya Gujarat iliandikwa.
Kipindi hicho kilishuhudiwa ujio wa wafanyabiashara wa Kihindi, wengi wao kutoka pwani ya Gujarat hadi katika mwambao wa Zanzibar na badaye Tanzania Bara.
Kupitia pepo za msimu wa masika, wafanyabiashara na mabaharia kutoka Ulaya wanaopitia Afrika walitegemea upepo huu unaotegemewa kufanya safari ya kwenda na kurudi katika Bahari ya Hindi kila mwaka.
Kwa Tanzania na India, mtandao ulivyokua na nguvu, mwingiliano kati ya watu wa Pwani ya Uswahilini na wenzao wa India ulizidi kuimarika.
Bila shaka huu ndio mfumo wa zamani zaidi wa njia za biashara, ulikusanya Mtandao wa Bahari ya Hindi wa wafanyabiashara wanaotumia jahazi, wakisafiri kutoka sehemu mbalimbali za Afrika (pamoja na Tanzania ya sasa), Uajemi, India, na Kusini-Mashariki mwa Asia.
Leo hii, Tanzania na India zinaendelea kufurahia uhusiano mzuri na wa kirafiki wa kidiplomasia unaojengwa juu ya nia ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii ambao ulianza karne nyingi zilizopita.
Nchi hizo mbili zina nia ya kutumia na kuongeza maono yao ya pamoja ya maendeleo, kukabiliana na changamoto za kila siku za ukuaji wa uchumi, na kutambua fursa za ubunifu kwa nchi kufanikiwa.
Kwa sasa, India ni mshirika wa nne wa kibiashara wa Tanzania, ikiwa na kiasi cha biashara takriban Dola za Kimarekani bilioni 6.5 mwaka 2022/23 (kulingana na takwimu za India) na Dola bilioni 3.1 mwaka 2021-2022 (kulingana na takwimu za Tanzania) ikilinganishwa na Dola bilioni 2.6 mwaka 2017/18.
Vile vile, India ni miongoni mwa vyanzo vitano vya juu vya uwekezaji nchini Tanzania. Katika mwaka 2021/22, miradi 630 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola bilioni 3.7 ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Bila kuachana na kanuni za msingi za Sera ya Mambo ya Nje, Rais Samia ameweka msukumo zaidi katika maeneo mapya ya ushirikiano kwa kutumia Tume ya Pamoja ya Kudumu na marafiki na washirika wetu, India ikiwa ndiyo kuu.
Tanzania na India zinashirikiana katika sekta za kimkakati kama vile maji, afya, kilimo, Tehama, uchumi wa buluu, elimu, biashara na uwekezaji na kilimo, na kukuza fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania ili kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDIs) hasa kutoka India.
Samia na diplomasia ya uchumi
Kimsingi, ziara ya Rais Samia ni mwendelezo wake katika kuipambania na kutekeleza kwa vitendo diplomasia ya uchumi, kwani itaendelea kufungua fursa nyingi za kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Mikakati hii ya Serikali ya Samia sasa itawafanya Mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuacha kuhudhuria hafla tu na badala yake sasa watakuwa na shughuli ya kutangaza bidhaa za Tanzania na kutafuta masoko.
Kwa hakika, Rais Samia anafanya vizuri katika diplomasia ya uchumi na ameonyesha dhahiri anavyotaka wanadiplomasia waende na wakati.
Mabalozi ni wawakilishi binafsi wa Rais, hivyo wanapokwenda kule serikali ya kule inawpokea na kuwapa hadhi nzuri tu, lakini pia kazi yako nyingine ni kusaidia Watanzania walioko katika nchi husika pamoja na kutazama fursa zilizopo huko au zilipo Tanzania na kuzinadi ili wafanyabiashara waje wawezeke kwa ustawi wa Tanzania.
Ikumbukwe kuwa, nchi nyingi duniani zilishaanza kutekeleza diplomasia ya uchumi, sasa ili diplomasia hiyo itekelezeke kama Rais anavyotaka ni lazima kuwe na utayari wa kuanzia wizara na wafanyabiashara ili kuhakikisha Tanzania inazalisha bidhaa bora zinazokubalika kimataifa.
Kwa sasa kuna ushindani mkubwa baina ya nchi na nchi kama Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Botswana, Namibia na nyinginezo ambao wakiuza bidhaa zao zinakuwa za viwango vya juu, sasa lazima na Watanzania tuwe na huu utayari wa kukabili ushindani.