Azam yakaa kileleni Ligi Kuu Bara

Na Zahoro Mlanzi

Timu ya Azam FC, imekaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutoka suluhu na Dodoma Jiji FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Matokeo hayo yameifanya Azam kufikisha alama 10 ikifuatiwa na Yanga na Simba zenye alama 9 kila moja huku Dodoma ikifikisha alama 5 ikishika nafasi ya saba sawa na Tabora United.

Mchezo huo ulitawaliwa na matumizi ya nguvu kutokana na kila upande kuikamia mechi ili kuondoka na alama tatu.

Azam itajutia nafasi iliyopata dakika ya 52 baada ya Lusajo Mwaikenda kufunga bao akiitendea haki pasi ya Idriss Mbombo lakini mwamuzi alidai ameotea na kuwafanya mashabiki wa Azam kujawa na hasira.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Bruno Ferry, amesema alitarajia kukutana na ushindani mkubwa kutoka kwa Dodoma lakini wanashukuru hawajafungwa.

“Tulijua lazima mchezo utakuwa wa kasi na matumizi makubwa ya nguvu, wachezaji walipambana lakini haikuwa rahisi kwao kuondoka na alama tatu, tunajipanga kwa mchezo ujao,” amesema Ferry.

Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope, amesema alama moja waliyopata si haba mbele ya Azam FC kwani hiyo ni miongoni mwa timu kubwa nchini.

“Tuliisoma Azam katika mechi mbili za mwisho, tukajua ni wapi wana nguvu zaidi na kwenda kufanyia kazi kitu ambacho kimetusaidia kupata alama moja,” amesema Liogope.

Ligi hiyo itaendelea Jumatano kwa mechi mbili ambapo Yanga itakuwa ugenini kuumana na Ihefu FC ikifuatiwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Namungo FC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *